Kitambi Afunguka Kwa nini aliondoka Azam FC kwa utata?
Kitambi ambaye alikuwa kocha msaidizi, amefanya kazi na Stewart mara mbili. Awali walikuwa wote kwenye kikosi cha Azam, kisha wakakutana ndani ya AFC Leopards.
Kocha huyo msomi, anasema alisomea Mechanical Engeneering, alipomaliza mwaka wa kwanza akaona haimfai, akabadilisha, akahamia BS Physics, akasoma miaka miwili, akaona bora aingie kwenye ukocha kabisa sehemu ambayo anaamini ndiyo atatimiza ndoto zake.
Ikumbukwe kuwa, kocha huyo ndiye aliyeipandisha Ndanda kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2014/15.
Kitambi amezungumza na Championi Ijumaa, hivi ndivyo anavyofunguka zaidi:
“Niliiongoza Ndanda mechi sita za ligi kuu, nne kati ya hizo hatukufanya vizuri, wakaona matokeo hayaendani na malengo ya timu, ndiyo tukaachana.
“Baada ya hapo nikapata nafasi ya kuwa mchambuzi pale Azam TV, baada ya muda Yusuph Bakhresa akanishawishi nihamie kwenye timu yao.
“Nikakubali na nikiwa Azam FC nilikuwa msaidizi wa George Nsimbe baada ya Joseph Omog kuondoka kabla ya kuja kwa Stewart Hall ambaye nilikuwa naye kwa msimu mzima pale.
Nini kilitokea Ndanda?
“Nafikiri tulikuwa na mtazamo tofauti na uongozi, kwa upande wangu nilijua kwa misimu mitatu timu ingekuwa katika harakati za kuhakikisha inabaki kwenye ligi.
“Kwa kuwa msimu wa 2013/14, Mbeya City walipanda na kufanya maajabu, Ndanda nao wakataka iwe kama hivyo, ni nadra hali hiyo kujitokeza.
Mama yako amekuwa mstari wa mbele katika kazi zako, mfano dili lako la kutua Ndanda alihusika, kwa nini?
“Unajua mama yangu ni mpenzi wa mpira, ndiyo maana hata mimi pale nilipoondoka Chuo Kikuu cha Pretoria kule Afrika Kusini na kusema nataka niwe kocha wa mpira, wengi walimshangaa kwa nini aliendelea kunisapoti.
“Nashukuru kwa upande wake aliona mimi nataka kufanya nini na niseme kuwa bila yeye nisingefika hapa kwani amechangia katika vitu vingi sana, amenilipia masomo ya ukocha Uingereza, kuendesha tovuti yangu ya uchambuzi na kunipelekea katika michuano ya Afcon nchini Afrika Kusini.
Ilikuwaje ulipofanya kazi na kocha wa kigeni mara ya kwanza?
“Kitu cha kwanza ni shauku ya kutaka kujua, wao wanafanya tofauti na wewe, ukizingatia bado nilikuwa kocha mdogo katika timu kutokana na uwezo aliokuwa nao.
“Upande wa Stewart, ilikuwa tofauti kidogo kwa sababu alikuja na msaidizi wake, Mario Marinica, hivyo kulikuwa na mkakati wa kupelekewa timu ya vijana U20 ila baada ya kukutana naye wakati wa michuano ya Kagame, niliandika ripoti ya baadhi ya timu zilivyokuwa zinacheza kitu ambacho naamini kilimshawishi afanye kazi na mimi.
“Kazi yangu kubwa chini ya Stewart nilikuwa kama mchambuzi wa mechi za wapinzani wetu kabla ya kucheza nao, kumuandikia ripoti na ushauri wangu, nashukuru kwa upande wake kwani iliweza kunipa kujifunza mambo mengi.
“Kiukweli Stewart kwangu amekuwa ni mtu ambaye nataka zaidi muda wote kufanya naye kazi kwa sababu anaitambua vyema taaluma yake na hata Kenya amekuwa akizungumziwa hivyo.
Stewart aliondokaje Azam FC?
“Tulikuwa tunaona Simba na Yanga kuna upendeleo unafanyika upande wao hasa katika ratiba na katika msimu huo kati ya Simba na Yanga mmoja alipangiwa mechi saba mfululizo nyumbani katika kumi za mwanzo.
“Kitu kingine ilikuwa ni malengo ya timu kuwa lazima tuchukue ubingwa ila kwa bahati mbaya kazi tuliyokuwa nayo ni ya matokeo sasa inapotokea hujapata matokeo inakuwa basi na uongozi ukaona haukuridhishwa naye.
Ulikabidhiwa majukumu Azam FC baada ya Stewart kuondoka, ilikuwaje?
“Kuondoka kwake kwetu ilikuwa ni kitu cha kushtukiza sana kwa kuwa tulikuwa na mechi ya fainali ya Kombe la FA, changamoto ilikuwa kubwa hasa namna ya kuweza kuirudisha timu yote katika morali, kwani wakati huo hatukuwa na matokeo mazuri kwenye ligi.
Kwa nini uliondoka Azam FC kwa utata?
“Sikuondoka kwa utata, mkataba wangu uliisha na niliambiwa timu bado ilinihitaji, kipindi hicho walikuwa wanakuja makocha wa Hispania, ilikuwa lazima wawe na mtu ambaye ana kumbukumbu za timu na wachezaji wote.
“Nilikubali kubaki huku nikisubiri mkataba, sikupewa kwa wakati na kuna baadhi ya matakwa niliomba hawakutimiza, nikaona vema kuachana nao.
“Wakati hayo yanatokea nilikuwa tayari najiandaa kufanya kozi ya Leseni B ya CAF, sasa nikaona hata kama nitakosa basi nitakuwa naenda zangu kusoma.
“Siwezi kulalamika kuhusu wao kushindwa maana kama bado ningeendelea kuwepo basi leo tusingeongea mimi kuwepo Kenya, unajua siku zote jaribu kuangalia jema katika mabaya lililokuwepo, sina kinyongo na wao kwani naamini ipo siku tutakutana.
Ilikuaje ukaibukia AFC Leopards?
“Nilienda kusomea kozi ya ukocha Leseni B baada ya kumaliza nikawa nipo nyumbani, nikapata ofa mbili kutoka Ndanda na Majimaji lakini sikuweza kwenda kwa kuwa kuna utafiti wa masomo yangu nilikuwa namalizia, wakati huo ndiyo Stewart alikuwa amepata kazi AFC Leopards.
“Akanitafuta na kuniuliza kama nina timu, akaniomba nikawa msaidizi wake, nikakubali. Nilipofika kule utendaji haukuwa mgumu ingawa Azam ilikuwa inagombania ubingwa lakini AFC ilikuwa ni timu ambayo ilikuwa inapigania kubaki katika ligi, hivyo tukasajili wachezaji wengi kwa ajili ya kujenga timu.
“Hata suala la kiuchumi kwao hawapo vizuri kama ilivyokuwa kwa Azam ila utendaji kazi ulibaki kama ulivyo, suala la yeye kwenda Canada hilo lipo kifamilia, aliniambia hivyo kwani alitaka kuwa karibu na familia yake.
“Kitu kizuri bado tunaendelea kuwasiliana na amekuwa mshauri wangu mkubwa katika kila kitu kwa sababu hata katika mechi dhidi ya Singida alinishauri mambo mengi.”
Post a Comment