Kajala: Nilivuta Bangi, Kidogo Inipoteze
CONFESSION! Staa wa filamu Bongo, Kajala Masanja amevunja ‘sefu’ ya kuhifadhia siri moyoni mwake na kuweka wazi kuwahi kujihusisha na ulevi wa madawa ya kulevya, aina ya bangi, Ijumaa lina kauli yake.
Katika mahojiano na mwandishi wetu hivi karibuni, msanii huyo ambaye ukiona tabu kumuita Kajala, mtambulishe kinywani mwako kama Mama Paula alisema akiwa na umri wa kuingia usichanani kutoka utotoni, alijikuta mikononi mwa marafiki waovu, waliojihusisha na ulevi huo, ambao walifanikiwa kumteka akili na kumvutisha mmea huo wenye majina mengi likiwemo dude la kimataifa, jambo ambalo anadai kulijutia kwa kiwango kisichotamkwa.
Kajala alisema licha ya kutumia bangi katika umri huo, hakudumu sana kwani aliachana nayo kufuatia jitihada kubwa za wazazi wake, huku akimshukuru Mungu kwamba hakuwahi kutopea kwenye madawa mengine ya kulevya.
Msanii huyo mwenye figa bomba alitumia mwanya huo kuwaonya vijana kuchunga sana mzuka wa umri ambao huleta vishwishi vingi vya matamanio ya kidunia na kwamba ni vyema sana wazazi kuwa makini na watoto wanapofika katika umri wa balehe na kuvunja ungo, kwani ndicho kipindi kibaya maishani mwa binadamu na kuangalia sana aina ya watu wanaotengeneza nao urafiki.
“Unajua inafika mahali sisi kama vioo vya jamii inatupasa kuzungumza ukweli wa maisha yetu husasan ya nyuma, ili kama ni watu kujifunza iwe hivyo, binafsi nimewahi kupitia maisha ambayo naweza kuyaita ya mpito, kipindi ambacho kila mtu hupitia katika harakati za ukuaji, kwamba nilijiingiza kwenye kampani za marafiki ambao ni watumiaji wa bangi.
“Hivyo, walinishawishi na kujikuta nikijiingiza kwenye ulevi huo, kidogo nipotee ila namshukuru sana Mungu kwani sikuwahi kuvuta madawa mengine kama cocaine, heroine sijui kujidunga masindano na mambo mengine ya kufanana na hayo, lakini ukweli kabisa huwa najuta sana kwa kuvuta bangi,” alisema Kajala na kuongeza;
“Ni muhimu wazazi kuwa makini na watoto katika kipindi cha kuingia kwenye utu uzima, kwa maana ya balehe ya kuvunja ungo, ndicho kipindi kibaya sana maishani kwa binadamu katika makuzi, vishawishi ni vingi sana.”
Post a Comment