ad

ad

Wazee Wa Kimila Waanika Maajabu ya Mti Uliotoa Uhai Watu 5, Arusha







ARUSHA: Ilikuwa lazima wafe! Hivyo ndivyo walivyokuwa wakisema baadhi ya watu walioshuhudia tukio la kutisha la mti mkubwa aina ya Mkuyu kuangukia nyumba ya Jonathan Kalamboya (55) Mei 9, mwaka huu na kuua watu watano wa familia yake katika Kijiji cha Ngeresi, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.

Mti huo uling’oka saa saba usiku kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mfululizo mkoani Arusha hivyo kusababisha maafa hayo ya vifo vya watu watano wa familia ya mzee Kalamboya ambao ni Jonathan Jonathan (16) Gloria Jonathan (11) Giliad Jonathan (31), Lazaro Lomnyaki (26) na Best Jonathan (20).

UWAZI KIJIJINI NGERESI

Baada ya tukio hilo, kama kawaida yake ya kuchimba na kuchimbua, gazeti hili lilifika eneo la tukio na kufanikiwa kupata undani wa vifo hivyo kwa kuzungumza na mzee Kalamboya aliyekuwa na haya ya kusema:

“Mimi wakati janga hili linatokea nilikuwa kazini zamu ya usiku mjini Arusha katika Hospitali ya Dk. Mohammed. Mke wangu alikwenda kumsaidia mkwe wetu aliyekuwa amejifungua.

“Wakati narudi nyumbani asubuhi, nilikutana na mama mmoja akaniambia juu ya tukio hili kwani aliniambia watoto wangu wamefukiwa na mti, nilipigwa na butwaa, nikajikuta nachanganyikiwa.

“Baadaye kuna mtu tena alinipigia simu akaniambia nisubiri watakuja kunichukua na gari lakini mimi nikapanda basi, sikufika nyumbani nikakutana na ndugu na jamaa wakanipeleka kwa mjomba wangu.

“Walinipeleka kwa mjomba kwa sababu waliniambia nyumbani kwangu hakuna makazi tena na watoto wamefariki dunia, nimebaki na wawili tu. Niliumia sana, sikuweza kuamini mara moja taarifa hizo.”

MAITI ZAFUKULIWA BAADA YA SAA SITA

Mzee huyo aliongeza kuwa, alipofika nyumbani ndipo alipothibitisha kuwa, alikuwa amebaki na watoto wawili tu kufuatia wengine kufariki dunia.

Alisema maiti za watoto wake zilikaa zikiwa zimekandamizwa na mti huo kwa saa sita kwani tangu saa nane usiku hadi saa moja asubuhi ndipo walipofanikiwa kuzitoa.

POLISI NAO WALICHELEWA KUFIKA

“Polisi walifika wakiwa wamechelewa kutokana na ubovu wa barabara. Hata hivyo, waliwasifu vijana kwa ushirikiano mkubwa wa uokoaji walioufanya,” alisema.

WATOTO WALIONUSURIKA KIFO

Kwa kudra za Mwenyezi Mungu, watoto wawili wa mzee huyo walinusurika kifo baada ya mmoja anayesoma kidato cha pili, Zakayo Jonathan kuchomoka ndani na mdogo wake wakati mti ukibingirika zaidi ya mita 150 kuelekea kwenye nyumba yao.

Akilisimulia Uwazi jinsi walinyonusurika kimaajabu, mtoto huyo alisema: “Nilianza kusikia mawe yakigonga nyumba nikadhani ni tetemeko la ardhi. Harakaharaka nilimchukua mdogo wangu na kutoka ndani kupitia dirishani, baada ya sekunde chache mti mkubwa uliokuwa

 ukitoka juu ya mlima ukagonga na ukasambaratisha nyumba yetu.

“Nilianza kulia na kupiga yowe na mdogo wangu kuita majirani ambao walifika na kukuta mti umefunika nyumba yetu.

“Kilichoniliza zaidi ni kwamba nilijua mti huo umewafunika kaka zangu, hivyo kwa vyovyote nilijua wameshafariki dunia,” alisema Zakayo huku akitokwa na machozi.

WAZEE WA KIMILA NAO WANENA

Wazee wa kijiji hicho wakiwemo wa kimila waliozungumza na Uwazi kuhusu vifo hivyo walisema, mti huo kwa jinsi wanavyoufahamu, kwa kuanguka kwake ilikuwa lazima uue lakini ni tukio ambalo limewashitua sana.

Wazee hao ambao wamekula chumvi nyingi walisema kuwa, mti huo ambao unakadiriwa kuishi zaidi ya miaka 200, ulikuwa ukitumika kwa mambo ya matambiko ya kimila kwa muda mrefu kiasi kwamba wapo ambao walikuwa wakihofia kuukaribia.

“Mti huu ulikuwa ukitumika kwa mambo ya kimila, mambo ya matambiko tangu enzi za mababu, kwa hiyo unaweza kuona siri iliyopo ya vifo vya ndugu zetu hao,” alisema mzee mmoja ambaye hata hivyo hakutaka jina lake liandikwe gazetini bila kufafanua zaidi.

Alisema licha ya imani hasi waliyonayo baadhi ya watu, mambo mengi ya heri pia yalikuwa yakiombwa na wazee wa enzi hizo chini ya mti huo lakini wameshangaa ulivyokuja kupoteza maisha ya watu tena katika mazingira ya kimaajabu.

“Ajabu moja kubwa ni kwamba mti huu baada ya kung’oka ulipasuka vipande viwili, kimoja kikakwepa nyumba na kingine kikaenda kufunika nyumba.

“Umeona wale nyuki, walikuwepo kwenye mti ule kwa miaka mingi na wala hawadhuru watu, wengine huamini pia kwamba wapo kwa ajili ya matambiko,” alisema bila kufafanua.

Mwandishi wetu alipoambiwa juu ya nyuki hao aliingiwa na woga, akataka kuondoka eneo hilo lakini alihakikishiwa na wazee hao kwamba hawezi kung’atwa, hivyo hakuwa na haja ya kukimbia.

MSIKIE HUYU!

Naye kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la John, mkazi wa kijiji hicho aliliambia Uwazi kuwa, mti huo licha ya kwamba ulikuwa ukitumika kwa matambiko lakini wengi walikuwa wakiamini unafuga majini.

“Unajua hii miti yenye umri mrefu kama huu inakuwa na mambo mazito, ndiyo maana wengi wanasema ilikuwa lazima uue, ndugu zetu wamekufa vifo vibaya sana, Mungu awapumzishe mahali pema peponi,” alisema kijana huyo.

Miili ya vijana hao wa mzee Kalamboya ilizikwa Juni 13, mwaka huu huku watoto watatu wakizikwa katika kaburi moja na hakuna aliyeweza kueleza sababu ya kufanya hivyo.

MKUU WA MKOA AGUSWA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliyehudhuria mazishi hayo aliwapa pole wafiwa kwa niaba ya serikali ambayo iligharamia mazishi.

Ofisi ya mkuu huyo wa mkoa iliahidi kutoa mabati 50 na mifuko ya saruji 50, pia ilitoa shilingi milioni 3.5 ili mzee huyo aweze kukarabati nyumba yake iliyosambaratishwa na mti huo.

Yeyote aliyeguswa na habari hii anaweza kumsaidia mzee huyu kwa chochote kwa kutumia namba yake, 0766 818906 kwani sasa yeye na familia yake iliyobaki wanaishi kwa mjomba wake- Mhariri.

No comments

Powered by Blogger.