ad

ad

SI KITU BILA PENZI LAKO - 23 (MWISHO MWISHO)

 
NYEMO CHILONGANI
Bi Anna hakutaka kuendelea kukaa kisiwani Madagaska hali iliyompelekea mumewe kurudi nae nchini Marekani. Muda wote Bi Anna alikuwa akionekana kuwa na huzuni, hakuamini kama mtoto wake alikuwa ameauwa katika nchi ya kigeni.
Kila siku alikuwa na majonzi kupita kawaida, alitamani kumuona tena mtoto wake na kuongea nae tena. Kila siku maisha ya kinyonge ndio ambayo yalikuwa yakiendelea maishani mwake.Kila siku alikuwa akilia katika kipini ambacho Patrick alikuwa amesemekana kuuawa porini.
Baada ya miezi kadhaa kupita, Bi Anna akaonekana kuwa na furaha tena mara baada ya kusikia kwamba Patrick alikuwa hai na hivyo alikuwa nchini Marekani. Kila siku ndoto zake zilikuwa ni kuonana na mtoto wake huyo ili kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake ya nyuma.
Katika kipindi ambacho Patrick alianza ziara, Bi Anna akaonekana kuwa na furaha zaidi kwani aliamini kwa kitendo cha Patrick kuja barani Afrika basi ni lazima pia angefika nchini Tanzania, nchi ambayo alizaliwa na kukulia.
Mlipuko wa Misri ulimfanya Bi Anna kuwa na wasiwasi kwa kuona kuwa maisha ya kijana wake yalikuwa matatani. Safari ya Patrick ilipotangazwa kwamba alikuwa akitarajiwa kuingia nchini Tanzania masaa machache yajayo, Bi Anna alionekana kuwa na furaha zaid kwa kuamini kwamba ni lazima angeweza kuonana na kijana wake huyo.
Bi Anna alikuwa miongozi mwa watu ambao walikuwa wamekusanyia uwanja wa ndege wakimsubiria Patrick. Alikuwa amevalia fulana nyeupe ambayo ilikuwa na picha ya mtoto wake huyo. Kila alipokuwa akiiangalia picha ile, alifarijika kupita kiasi.
Wakati Patrick anashusha ngazi, Bi Anna alibaki akimwangalia mtoto wake, alishindwa kabisa kujizuia, akabaki akilia tu. Kila alipokuwa akimwangalia mtoto wake, maisha ya nyuma katika kipindi ambacho alikuwa kijijini yalikuwa yakijirudia kichwani mwake kama mkanda wa filamu.
Bi Anna alijitahidi kupenya penya kumfuata Patrick lakini alishindwa kabisa, hiyo ilitokana na wingi wa watu pamoja na Polisi ambao walikuwa wakiwazuia watu hao. Mara baada ya kuwapungia watu mikono mahali hapo, moja kwa moja Patrick na wenzake wakaingia garini.
Bi Anna akalifuata gari lake na kuingia. Akaanza kuufuatlia msafara ule ambao uliishia uwanja wa Taifa. Akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika uwanja ule. Maneno yote ambayo alikuwa akiyaongea Patrick yalikuwa yakimgusa kupita kiasi. Alitamani aondoke mahali hapo na kumfuata Patrick na kumwambia kwamba hakuwa ameuawa bali alikuwa hai.
Patrick bado alikuwa akiendelea kuongea mambo mbalimbali ambayo yalikuwa yametokea maishani mwake. Bi Anna akashindwa kuvumilia, kwa haraka haraka akatoka mahali hapo na kuufuata mlango wa kutokea nje. Akatoka na kuanza kuufuata mlango wa kuingilia katika uwanja wa kuchezea mpira kabisa ambao kulikuwa na majukwaa kadhaa.
“Nikusaidie nini mama?” Polisi mmoja ambaye alisimama mlangoni alimuuliza Bi Anna.
“Nataka kuongea na mwanangu”
“Kuongea na mwanao? Mwanao yupi?” Polisi yule aliuliza huku akionekana kumshangaa Bi Anna.
“Patrick” Bi Anna alijibu. Polisi yule hakuongea kitu chochote kile zaidi ya kuanza kucheka kwani alikwishamuona Bi Anna kuwa kama kichaa.
Bi Anna akaonekana kukasirika, akaanza kumfuata polisi yule. Polisi akamuwahi Bi Anna kwa kumdhibiti vilivyo. Polisi mwingine akafika mahali pale, Bi Anna alikuwa pembeni huku akiendelea kumuomba polisi yule amuachie.
“Kuna nini?”
“Huyu mwanamke. Eti anataka kuonana na mtoto wake, Patrick” Yule polisi alimwambia.
Maneno yale yalionekana kumshangaza kila mtu, wakamwangalia Bi Anna kwa macho ya mshangao huku akilia kwa kung’ang’ania kuongea na Patrick.
“Haiwezekani kabisa”
Bi Anna akaonekana kukumbuka kitu, akatoka mahali hapo na kuelekea pembeni, akachukua kipande cha karatasi pamoja na kalamu na kisha kuandika kitu fulani, akawarudia na kuwakabishi.
“Naomba mumpe hii karatasi. Naomba mumpatie” Bi Anna aliwaambia na kuondoka mahali hapo.
“Yule mwanamke unajua kama namkumbuka” polisi mmoja alisema.
“Hata mimi mwenyewe namkumbuka. Nafikiri ni yule mke wa Mheshimiwa Mayemba”
“Sawa sawa. Sasa kwa nini tumemzuia, hauoni kama inaweza kuwa tatizo hata kupoteza kazi?”
“Inawezekana. Ila tufanye kama alivyotaka. Tumfikishie karatasi hii mhusika, Patrick”
“Itawezekana vipi?”
“Hata mpambe wa Waziri tutampa ili mladi tu Patrick aipate”
“Wazo zuri”
*****
Patrick alikuwa ametulia ndani ya chumba kimoja katika hoteli ya Moven Pick. Mawazo yake katika kipindi kile yalikuwa yakimfikiria Victoria tu. Kitu alichokitaka kukifanya ni kuanza safari ya kuelekea katika kijiji cha Wami kwa ajili ya kuonanan na Victoria tu.
Huyo ndiye amsichana ambaye alikuwa kichwani mwake, alikuwa akimpenda kuliko msichana yeyote yule. Alikuwa kila kitu katika maisha yake, hakuwa radhi kumpoteza maishani mwake. Ingawa masaa yalikuwa yamekatika lakini Patrick hakuonekana kuwa na usingizi, muda wote alikuwa akijigeuza geuza tu kitandani.
Mara simu ya mezani kwake ikaanza kuita, akainuka na kuanza kuifuata, alipoifikia, akaunyanyua mkonga wa simu na kuupleka sikioni. Sauti ya Vanessa ilikuwa ikisikika vizuri masikioni mwake.
“A piece of paper? (Kipande cha karatasi?)” Patrick aliuliza kwa mshangao.
“Yeah”
“What does it say? (Kinasemaje?)” Patrick aliuliza.
“It is written in Swahili language, I dont know this language (Imeandikwa katika lugha ya Kiswahili, siifahamu lugha hii)” Vanessa alimwambia Patrick.
Patrick akakata simu, akaifuata suruali yake ya jinzi, akaivaa na kuanza kuelekea katika chumba cha Vanessa. Alipoufikia mlango, akagonga na Vanessa kumfungulia.
“Where is it? (Iko wapi?)” Patrick aliuliza.
Vanessa akakichukua kipande kie cha karatasi na kisha kumkabidhi Patrick. Patick akakaa kitandani na kuanza kuisoma karatasi ile, ghafla kama mtu aliyechanganyikiwa akasimama juu na kuana kuruka ruka kwa furaha kama mtu ambaye alishinda Bingo.
“My mother...my mother, Vanessa (Mama yangu....mama yangu, Vanessa)” Parick alimwambia Vanessa huku akiendelea kuruka ruka juu.
“You told me she died (Uliniambia alifariki)
“I think she didn’t, she is the one who wrote this (Nafikiri hakufariki, yeye ndiye aliyeandika hii)” Patrick alimwambia Vanessa.
“What does a piece of paper say? (Karatasi inasemaje?)
“I’m seeing you my son right now. You’ve grown up now. I love you more than anyone in this world. They didn’t kill me as they did to your father (Ninakuona sasa hivi mwanangu. Umekua sasa. Ninakupenda kuliko mtu yeyote katika ulimwengu huu. Hawakuniua kama walivyomuua baba yako)” Patrick alimsomea Vanessa.
Usingizi haukupatikana tena. Patrick alibaki chumbani kwa Vanessa wakipiga stori tu mpaka alfajiri. Wote wakaanza kujiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea katika hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kuwaona wagonjwa ambao walikuwa wakisumbuliwa na magonjwa tofauti tofauti.
Saa mbili asubuhi, magari saba yakafika mahali hapo huku gari a Waziri Mkuu, Bwana Peter Charles akiwa amefika hotelini hapo na gari lake. Moja kwa moja Patrick na Vanessa wakatoka. Wakaingia garini na moja kwa moja safari ya kuelekea katika hospitali ya Muhimbili kuanza.
Mawazo ya Patrick kwa wakati huo yalikuwa juu ya watu wawili tu, alikuwa akimfikiria sana mama yake pamoja na Victoria, alijua fika kwamba mama yake alikuwa ndani ya jiji la Dar es Salaam. Hakujua ni kwa jinsi gani alikuwa amefika ndani ya jiji hilo na wakati hawakuwa na ndugu yeyote mahali hapo.
Mawazo juu ya Victoria yalikuwa ni kutaka kumuona tu. Alimpenda sana binti huyo kuliko msichana yeyote yule katika dunia hii. Alihitaji kwenda kijijini Wami na kwenda kumchukua Victoria kama ambavyo alimuahidi katika kipindi ambacho alimuacha porini.
Idadi kubwa ya wauguzi walikuwa nje, tayari walikuwa wamekwishapewa taarifa kwamba Patrick angekuwa katika hospitali hiyo muda wowote. Kelele zikaanza kusikika japokuwa walijua sheria mojawapo hospitalini hapo ilikuwa ni kutopiga kelele.
Wananchi ambao walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kuwaona wagonjwa wao, wakaanza kumpiga picha Patrick ambaye aliteremka garini na kuungana na wenzake pamoja na waziri mkuu, Bwana Peter Charles. Wakaanza kuangalia sehemu mbalimbali katika hospitali hiyo huku Patrick akipata muda wa kuwaona wagonjwa mbalimbali na kuwafariji.
Kila mgonjwa alijiona kufarijika, uwepo wa Patrick mbele ya macho yake ulionekana kumfariji sana. Patrick akaendelea kupiga hatua mpaka katika wodi ambayo wagonjwa waliokuwa wakiugua Upungufu wa Kinga mwilini walipokuwa.
Patrick akajikuta akitokwa na machozi, hakuamini kama kweli katika dunia hii kulikuwa na watu waliokuwa wakiteseka namna ile. Akatumia muda wa dakika thelathini, akatoka ndani ya wodi ile huku moyo wake ukiwa umeumia kupita kiasi.
“Kuna wodi ya watu ambao wanasumbuliwa na uti wa mgongo. Kila siku idadi ya wagonjwa hao inaonekana kuongezeka” Dokta Humphrey alimwambia Patrick.
“Naomba mnipeleke huko, ninahitaji kuwaona pia” Patrick alimwambia Dokta Humphrey ambaye wala hakuleta pingamizi lolote lile.
Katika kila hatua ambayo Patrick alikuwa akiendelea kuwaona wagonjwa, waandishi wa habari bado walikuwa wakiendelea kupiga picha kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea mahali hapo. Watu wote ishirini na mbili waliokuwa pamoja na Patrick wakaanza kuelekea katika wodi ambayo kulikuwa na wagonjwa waliokuwa wakisumbuliwa na uti wa mgongo.
Binti mmoja alionekana kukaa benchini huku uso wake akiwa ameuinamisha chini. Kwa haraka haraka dokta Humphrey akaanza kumfuata binti yule, alipomfikia, akaanza kuongea nae, mara binti yule akasimama na kuanza kupiga hatua kuelekea kule Patrick, wenzake na waandishi wa habari walipokuwa.
Mara baada ya kupishana na binti yule, Patrick akasimama. Uso wake haukuonekana kuwa wa kawaida, akageuka nyuma na kuanza kumwangalia binti yule. Kila mtu akaanza kumshangaa Patrick kutokana na kusimama kwa muda akimwangalia binti yule ambaye alikuwa amepishana nao.
Mawazo ya Patrick yakarudi nyuma kabisa, tena kwa haraka haraka kwa kasi ambayo wala haikuwa ya kawaida. Alimfahamu Victoria vilivyo, alijua ni kwa mwendo gani binti huyo alikuwa akitembea, alijua mambo mengi kuhusu Victoria kiasi ambacho hata kama angekuwa mbali kiasi gani, basi ni lazima angejua kama ni yeye.
“Victoria....Victoria...” Patrick alijikuta akiita.
Hakuwa na wasiwasi hata kidogo, alikuwa na uhakika asilimia mia moja kwamba mtu ambaye alikuwa akimuita alikuwa Victoria. Victoria akasimama lakini hakugeuka nyuma hali iliyoonekana kama mtu ambaye alikuwa akijifikiria kugeuka au kutokugeuka.
Kwa taratibu Patrick akaanza kupiga hatua kumfuata Victoria ambaye bado alikuwa amesimama. Patrick alijihisi kutetemeka huku kijasho chembamba kikimtoka. Bado alikuwa akiendelea kupiga hatua kumfuata Victoria.
Kila mtu mahali pale alibaki akiwa amesimama huku akimwangalia Patrick ambaye bado alikuwa akipiga hatua za taratibu kumfuata Victoria. Vanessa alibaki kimya akmwangalia Patrick, jina ambalo alilisikia kutoka kwa Patrick wala halikuwa geni masikioni mwake, alikuwa na uhakika kwamba yule ndiye Victoria ambaye mara kwa mara Patrick alikuwa akipenda kumzungumzia nchini Marekani.
“Ni mimi, Victoria. Naomba ugeuke nyuma mpenzi” Patrick aliendelea kumwambia Victoria.
Victoria akaanza kugeuka nyuma kwa taratibu sana. Macho yake yakagongana na macho ya Patrick, Victoria akashtuka kupita kawaida, alijiona kukosa nguvu. Akabaki akiwa amesimama akimwangalia Patrick. Nae akaanza kumsogelea Patrick na wote kukumbatiana.
Kila mmoja alikuwa akitokwa na machozi. Hakuna aliyeamini kama angemuona mwenzake mahali hapo. Walikumbatiana mpaka wote kuanguka chini huku wote wakilia kama watoto wadogo. Tukio lile likaonekana kuwa tukio kubwa, waandishi wa habari wakaanza kuwapiga picha.
“Siamini. Hatimae nimekutana nawe” Patrick alimwambia Victoria huku wakiwa chini.
“Nimekukumbuka mpenzi. Nimekaa kipindi chote huku nikiamini kwamba ni lazima ningekuona tena” Victoria alimwambia Patrick.
Siku hiyo ikaonekana kuwa siku ya furaha kwa wote wawili. Kila wakati walikuwa na furaha. Patrick hakujali kama muonekano wa Victoria ulikuwa si mzuri hasa kutembea pamoja nae, kitu ambacho alikuwa akikifurahia ni kukutana na Victoria mahali hapo.
Muda wote alikuwa akiuzunguusha mkono wake mabegani mwa Victoria. Alijisikia furaha sana kukutana na msichana ambaye alikuwa akimkumbuka siku zote. Akayaona maisha yake yakianza kutawaliwa na furaha katika kipindi hicho.
Mara baada ya kumaliza kuwaona wagonjwa, Patrick hakutaka kupoteza muda, wakapanda ndege na kuanza safari ya kuelekea Shinyanga. Taarifa ya habari ikatangazwa kwamba Patrick alikuwa njiani kuelekea mkoani Shinyanga.
Ingawa habari ile ilikuwa ni ya kushtukiza lakini watu waliokuwa wakiishi mkoani Shinyanga wakakusanyika katika uwanja wa ndege wakiisubiria ndege hiyo. Saa nane kasoro kumi na mbili, ndege ile ikaanza kutua katika uwanja wa ndege wa mkoani Shinyanga.
Ndege ikatua na Patick kuanza kuteremka huku akiwa amemshika Victoria mkono. Watu wakaanza kupiga kelele za shangwe katika kipindi ambacho Patrick alikuwa akishuka ngazi. Vigelegele vikaanza kusikika, wakinamama wakaanza kuimba nyimbo za lugha yao.
Patrick akaanza kutembea kumfuata mkuu wa mkoa, Bwana Wambura. Wote wakasalimiana na kisha kuwapungia mkono wananchi ambao walikuwa wamkusanyika uwanjani hapo na kisha kuanza kuongea nao kama mtu aliyekuwa akiuhutubia mkutano.
Patrick alitumia dakika tano kuongea na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Shinyanga ambao walikuwa wamefika mahali hapo na kisha kuingia garini na safari ya kuelekea katika kijiji chao cha Chibe kuanza. Safari ilichukua dakika arobaini na tano, wakaanza kuingia katika kijiji hicho.
Wote wakateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea kule nyumba ya mwenyekiti wa kijiji, Bwana Msumari. Kila mtu kijijini alikuwa akiwashangaa wazungu wale ambao walikuwa wametangulizana na mkuu wa mkoa pamoja na Patrick.
Patrick alionekana kuwa tofauti na kipindi ambacho alikuwa nyuma, alionekana kubadilika katika kila kitu. Mara baada ya mwendo mdogo, wakafika katika eneo la nyumba ya mwenyekiti wa kijiji huku watu wakiwa wanawafuatilia kwa nyuma.
Bwana Msumari akaitwa, alipotoka, macho yake yakatua kwa wazungu ambao walikuwa mbele yake. Akaonekana kushtuka, akaanza kujiuliza maswali mengi kuhusu wazungu wale, mara alipmuona Patrick, moyo wake ukatulia.
“Karibu Patrick” Bwana Msumari alimkaribisha Patrick.
“Asante” Patick aliitikia huku akiachia tabasamu pana.
Wakaongea mambo mengi mahali hapo na kisha wote kuanza kupiga hatua kuelekea kule katika nyumba ambayo Patrick alikuwa akiish na wazazi wake. Moyo wake ukaanza kumuuma na kumkumbusaha mambo ya nyuma ambayo yalikuwa yametokea katika maisha yake.
Nyumba ilikuwa imeteketezwa kwa moto na wala hakukuwa na kitu chochote ambacho kilikuwa kimebakia. Eneo la nyumba ile ikaonekana kujaa majani. Patrick aliumia zaidi mara baada ya kupaangalia sehemu ambayo baba yake, mzee Christopher alipokuwa amelazwa na kushambuliwa.
Patick akaingia ndani, machozi yalikuwa yakimtoka kama mtoto mdogo. Moyo wake uliendelea kumuuma zaidi, kila alipokuwa akiyaangalia maisha yake ambayo alikuwa akiyaishi zamani na yale aliyokuwa akiyaishi katika kipindi hiki, aliona utofauti mkubwa sana.
“Kaburi la baba yangu liko wapi?” Patick aliuliza.
“Nifuate” Bwana Msumari alimwambia Patrick na kisha kuanza kumfuata.
Safari yao ikaishia nyuma ya nyumba ile. Patrick akaanza kuangalia katika sehemu ile, sehemu ambayo ilionekana kufukiwa kitu ilikuwa ikionekana vizuri machoni mwake.
“Hili ni kaburi la baba yako. Nilimzika peke yangu baada ya wanakijiji wote kukataa kumzika” Bwana Msumari alimwambia Patrick ambaye machozi yakaongezeka zaidi.
“Nitakichukia kijiji hiki katika maisha yangu yote” Patrick alimwambia Bwana Msumari huku akionekana kuwa na hasira.
“Usifanye hivyo mpenzi. Haitosaidia” Victoria alimwambia Patrick.
“Inaniuma Victoria. Moyo wangu unaniuma. Baba yangu niliyekuwa nampenda kwa moyo wote, amezikwa kama mnyama” Patrick alimwambia Victoria huku akiendelea kuwa na hasira.
“Kumbuka kuwa hiki ni kijiji chako na kila siku kitaendelea kuwa kiji chako. Haitosaidi kama utaendeleza chuki kwao” Victoria alimwambia Patick.
“Lak...”
“Usiseme hivyo mpenzi. Naomba uwasamehe” Victoria alimwambia Patrick.
“Nimekuelewa”
Patrick hakutaka kuendelea kukaa kijijini hapo. Alichokifanya ni kuchangia mfuko wa kijiji kwa kutoa shilingi milioni tano na kumpati Bwana Msumari kiasi cha shilingi miioni moja kama shukrani kwake na kisha safari ya kuelekea katika kijiji cha Wami kuanza.
Waliingia katika kijiji cha Wami baada ya dakika thelathini. Watu wote ambao walikuwa wakimuona Victoria walikuwa wameshtuka kupita kiasi. Victoria alionekana kuwa tofauti na Victoria yule ambaye alitoroka kijijini pale. Mavazi aliyokuwa ameyavaa, nywele zake alivyokuwa amezitengeneza zilionekana kumpendezesha sana.
Mara baada ya kumuona mama yake ambaye alikuwa nje ya nyumba yao, Victoria akaanza kumkimbilia na kumkumbatia kwa furaha. Wote walikuwa wakilia kwa furaha. Mzee Carlos akatoka ndani na kuja mahali hapo. Macho yake yakatua kwa binti yake, Victoria, uso wake ukaonyesha tabasamu pana.
“Shikamoo baba”
“Marahaba binti yangu”
Wote wakakaa chini na kuanza kuongea mambo mengi. Patrick na Victoria wakatumia muda huo kuelezea historia za maisha yaliyotokea katika maisha yao. Kila mmoja alibaki akistaajabu. Patric alionekana kuwa na bahati kupita kawaida.
“Nimeona ni bora kuja kuomba ruhusa kwenu. Ninahitaji kukaa na binti yenu hata kabla sijamuoa” patrick aliwaambia.
“Hilo hakuna tatizo. Sisi kama wazazi tunakuruhusu kwa moyo mmoja” Mzee Carlos alimwambia Patrick hali iliyowafanya kufurahia.
Walikaaa kwa takribani masaa matat na ndipo wakaondoka na moja kwa moja kupanda ndege. Safari iliyofuata ilikuwa ni kuelekea jijini Mwanza. Lengo lake kubwa lilikuwa ni kwenda katika kisiwa cha Ukerewe ili kuwaona watu ambao alikuwa amewaacha mahali huko.
Kama kawaida, taarifa ikatangazwa na watu wengi kukusanyika uwanja wa ndege. Patrick akaanza kuteremka kutoka katika ndege huku Victoria akiwa pembeni yake. Akawapungia miko watu waliokuwa mahali hapo na kisha kusalmiana na mkuu wa mkoa huo, Bwana Yusuph Kandoro na kisha kuanza kuelekea pembezoni mwa ziwa Viktoria ambapo boti nzuri ikaandaliwa na kisha kuanza kuelekea kisiwani Ukerewe.
Kutokana na mwendo wa boti ile kuwa mkubwa, ni ndani ya dakika kumi tu wakawa wamekwishafika. Wote wakateremka na kuanza kuelekea kule kulipokuwa na nyumba kadhaa za wavuvi.
“Mungu wangu! Patrick!” Fikiri alisema mara baada ya kumuona Patrick.
Wote wakaanza kumkimbilia na kukumbatiana. Kila mmoja akaonekana kuwa na furaha. Mzee Mshana akatokea mahali hapo, Patrick akamsalimia na kisha kukaa mahali hapo kwa dakika kadhaa huku akiwasimulia kila kitu kilichotokea katika maisha yake mara baada ya kutoroka na mtumbwi wao.
“Kweli Mungu alikuwa pamoja nawe” Fikiri alimwambia Patrick.
Patrick hakutaka kuondoka mahali hapo hivi hivi. Alichokifanya ni kuwaachia milioni saba kama shukrani zake kwao na kuwaaahidi kuwanunulia mitumbwi ya kisasa ya uvuaji pamoja na boti ambayo itawasaidi kuwasafirisha kutoka Ukerewe mpaka Mwanza mjini na fedha ambazo zingepatikana basi zingeyaendesha maisha yao.
“Ni msaada mkubwa sana ambao wala hatukuutarajia maishani mwetu. Tunashukuru sana” Bwana Mshana alimwambia Patrick.
“Msijali. Ninafanya hivi kwa kuwa mlinionyeshea moyo wa kunijali. Ndani ya wiki moja, kila nilichokiahidi kitakuwa kimewafikia” Patrick aliwaambia.
Patrick akaagana nao na kupanda boti na kisha kuelekea Mwanza mjini. Alionekana kuchoka sana lakini akataka kumaliza kila kitu kwa wakati huo ili hata kama angerudi Dar es Salaam basi kazi ingekuwa ni kumtafuta mama yake tu.
Watu walikuwa wamekusanyika pembezoni mwa ziwa Viktoria wakimsubiri Patrick. Kila mtu alikuwa akitaka kumuona Patrick ambaye alikuwa akitangazwa sana na vyombo vya habari. Patrick na wenzake wakateremka kutoka mtumbwini na kisha kuanza kuongea na watu waliokusanyika mahali hapo.
“Patrick...Patrick...Patrick...” Sauti ilisikika ikiita.
Ingawa Patrick alikuwa akiitwa na watu wengi tofauti mahali hapo lakini sauti hii ilionekana kuwa si ngeni masikioni mwake. Akageuka na kuanza kuangalia angalia ni nani ambaye alikuwa amemuita mahali hapo. Macho yake yakatua kwa mtu ambaye nae alikuwa muhimu katika maisha yake, katika siku zote alikuwa akifikiri kwamba mtu huyu alikuwa amefariki dunia, Azizi.
Patrick akaanza kumfuata Azizi huku akionekana kuchanganyikiwa kwa furaha, alipomfikia, akamkumbatia. Kila mtu akamuona Azizi kuwa na bahati ya kukumbatiana na Patrick. Wote walikuwa wakilia kwa furaha, hawakuamini kama kweli wangeweza kukutana.
“Ni wewe Azizi?” Patrick aliuliza.
“Ni mimi...ni mimi...” Azizi alimwambia Patrick.
“Kumbe haukufa ziwani! Au hawakukutosa majini?”
“Walinitosa. Nilipoteza fahamu. Niliokolewa na wavuvi kutoka nchini Uganda. Kipindi chote nilikuwa nikiishi Uganda. Niliposikia kuhusu wewe, nikapanga kuja kukuona. Hivi hapa unaponiona nilikuwa na safari ya kuelekea Dar es Salaam kutaka kuonana na wewe tu” Azizi alimwambia Patrick.
“Ni lazima tuondoke Aziz. Siwezi kukuacha peke yako, ni lazima niwe pamoja nawe tena. Ni lazima uishi nami nchini Marekani” Patrick alimwambia Azizi.
“Haitowezekana Patrick. Nina mchumba ambaye ni mjauzito. Ni lazima nikae nae na kumtunza” Azizi alimwambia Patrick.
“Utamtunza nchini Marekani. Wewe ni rafiki yangu. Sitokuwa tayari kukuacha uendelee kuishi huku. Sitaki upate shida yoyote ile” Patick alimwambia Azizi.
“Sawa. Tutakwenda lakini kwanza ni lazima niende nikamchukue nchini Uganda” Azizi alimwambia Patrick.
“Panda ndege. Nenda kamchukue na kisha uje nae Dar es Salaam. Sitoweza kuondoka bila wewe” Patrick alimwambia Azizi
“Kupanda ndege! Sina nauliza Patrick”
“Hilo si tatizo. Kila kitu nitagharamia mimi” Patrick alimwambia Azizi.
******
Ndege ilikuwa ikitua katika ardhi ya jiji la Dar es Salaam. Patrick akaanza kuteremka na kisha kuanza kuyafuata magari yaliyokuwa mahali pale huku akiwa na wenzake. Muda ulikuwa umekwenda sana na hakutakiwa kwenda sehemu yoyote ile zaidi ya kwenda Ikulu ambako huko chakula cha usiku kilikuwa kimeandaliwa.
Alihitajika kwenda kula pamoja na viongozi kadhaa wa nchi hii akiwepo raisi na mawaziri wote. Mara baada ya gari kusimama katika eneo la Ikulu, wote wakateremka na kuanza kuelekea sehemu iliyokuwa na viti na kutulia.
“Patrick...” Patrick alisikia akiitwa.
Akageuka nyuma, macho yake yakagongana na macho ya mama yake. Katika hali iliyoonyesha kuchanganyikiwa, akasimama na kuanza kumsogelea mama yake, Bi Anna na kumkumbatia. Wote walikuwa wakilia, familia ikaonekana kuungana mara bada ya mtawanyiko wa muda mrefu maishani mwao.
“Siamni kama ningekutana nawe mwanangu” Bi Anna alimwambia Patrick.
“Umekua mwanangu. Umekua” Bi Anna alimwambia Patrick na kumkumbatia tena.
Patrick akasimama na kuwaeleza watu kwamba yule ndiye ambaye alikuwa mama yake. Kutokana na kuwaelezea kabla historia ya maisha yake, kila mmoja alimtambua.
“Nimeolewa Patrick. Yule pale ni baba yako wa kambo” Bi Anna alimwambia Patrick huku akimuonyeshea Bwana Mayemba. Patrick akamsogelea, akamsalimia na kumkumbatia.
*****
Patrick akajisikia kuwa na amani. Staili ya maisha yake ya kubadilisha magari kila anapokwenda, haikutokea nchini Tanzania kwani aliona hata kama angeuawa nchini Tanzania, ilikuwa ni sawa kwani angeuawa ndani ya nchi yake mwenyewe.
“Tunakwenda kuanza maisha mapya Marekani” Patrick alimwambia Victoria huku akionekana kuwa na furaha.
“Sitoweza kwenda huko mpaka utakaponifanyia kitu kimoja” Victoria alimwambia Patrick.
“Kitu gani mpenzi?”
“Nataka usafirishe dada yangu akatibiwe huko. Sitaki kumpoteza katika maisha yangu. Yeye ni muhimu, kila siku nilikuwa nae akinilinda na kunilea kama mama yangu” Victoria alimwambia Patrick.
“Dada yupi?”
“Getrude ambaye nilikuwa nikiishi nae mkoani Tabora”
“Usijali. Ni hilo tu au kuna jingine?”
“Ni hilo tu”
“Tutaondoka nae. Ila ninyi inabidi mtangulie. Ninamsubiri Azizi, mfanyiwe mambo yote kuhusu hati za kusafiria, baada ya hapo mtaondoka, nami nitawakuta huko” Patrick alimwambia Victoria.
“Kwa nini hautaki kwenda nasi?”
“Si kwamba sitaki. Ila kuna nchi mbili zimebakia kwenda kuzitembelea kama balozi. Naanza nchini Namibia kisha Zimbabwe. Nitakapomaliza, nitakuja kuendelea kuishi nawe mpenzi” Patrick alimwambia Victoria.
“Utachukua muda gani?”
“Siku tano”
“Sawa”
Kila kitu ambacho kilikuwa kimepangwa ndicho ambacho kilikuwa kimetokea. Mara baada ya hati za kusafiria kupatikana, Victoria, Azizi, Getrude na mchumba wa Azizi, Mariamu wakasafiri kuelekea nchini Marekani. Getrude akapelekwa katika hospitali kubwa jijini New York na kisha kuanza kupatiwa matibabu.
Patrick hakutakiwa kuishi kwa wasiwasi tena kwani tayari aliwaambia Polisi kwamba Bwana Khan ndiye ambae alikuwa akihusika na mauaji yote ya watu waliokuwa na ngozi nyeusi nchini Ujerumani. Hukumu ya kifo ikatolewa na mzee huyo kuuliwa kwa kuchomwa sindano iliyokuwa na sumu kali.
Ilichukua miaka mitano Patrick na Azizi wakaoa pamoja katika kanisa la kilutheri nchini Marekani huku Azizi na mkewe wakiwa wamebadilisha dini zao na kuwa wakristo. Maisha mapya kama familia yakaanza nchini Marekani.
Azizi akatafutiwa kazi nzuri ambayo ilikuwa ikimuingizia kiasi kikubwa cha fedha ambazo akaaanzisha miladi mingi na baada ya miaka miwili akawa akimiliki televisheni zake mbili zlizokuwa zikirusha vipindi vyake nchini Marekani.
Bado Patrick alikuwa akiendelea kuingiza fedha kila siku katika maisha yake. Kamwe hakumsahau mama yake ambaye mara kwa mara alikuwa akielekea nchini Marekani. Patick akaingia katika orodha ya matajiri mia moja ambao walikuwa wakimiliki kiasi kikubwa cha fedha.
Miladi mbalimbali ambayo alikuwa ameianzisha ndio ambayo ilikuwa ikiendelea kumuingizia fedha kiasi ambacho alikuwa akimiliki ndege, boti kubwa, magari ya kifahari pamoja na vitu vingine vingi. Baada ya miaka miwili, akainunua klabu ya mpira wa kikapu ya Chicago Bulls na kumnunua mchezaji mdogo, Michael Jordan ambaye baadae akaja kuwa mchezaji mahili katika klabu hiyo.
Getrude hakutakiwa kurudi nchini Tanzania, alitakiwa kuanza maisha yake nchini Marekani huku akipelekwa katika chuo kimojawapo kusomea uuguzi ambako baada ya mwaka, akawa dokta katika hospitali ya jijini Los Angels.
Miaka miwili ikapita, Victoria akajifungua watoto mapacha ambao majina yao yalikuwa Octavia na Octaviana. Patrick na mkewe, Victoria walikuwa wakiishi maisha ya furaha, kila kitu ambacho kilipita katika maisha yao, walikichukulia kuwa kama historia.

MWISHO

No comments

Powered by Blogger.