SI KITU BILA PENZI LAKO-21
NYEMO CHILONGANI
Ndege ilikuwa ikitarajiwa kuingia katika uwanja wa JFK saa tatu asubuhi lakini saa moja asubuhi tayari watu walikuwa wamekusanyika uwanjani hapo. Muda ulikuwa ukizidi kwenda lakini watu waliyaona masaa kwenda taratibu sana.
Mabango yalikuwa yametapakaa katika umati huo wa watu ambao walikuwa wakimsubiri Patrick huku idadi kubwa ya watu wakiwa wamevalia fulana zilizokuwa na picha ya Patrick. Watoto wawili ambao walikuwa na maua mikononi walikuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya kumkabishi Patrick maua hayo.
Waandishi wa habari hawakuwa mbali, walikuwa uwanjani hapo huku kamera zao zikiwa zinaendelea kufanya kazi ya kuwapiga picha watu mbalimbali ambao walikuwa mahali hapo. Eneo kubwa la uwanja ule ulionekana kujaa watu ambao walikuwa wamefika mahali pale kwa ajili ya kumpokea Patrick ambaye alitarajiwa kuingia muda mchache ujao.
Huku zikiwa zimesalia dakika kumi na tano kabla ya ndege hiyo kufika uwanjani hapo, gari la kifahari ambalo lilikuwa likiongozwa na pikipiki kadhaa pamoja na mgari mengine ya kifahari yakaanza kuingia mahali hapo. Watu wakaombwa kuachia nafasi. Magari yale yakasimama na Waziri wa Mambo ya Ndani, Bwana Thomson akateremka na kuanza kupiga hatua kule ambapo alielekezwa kwenda.
Saa tatu kasoro tano ndege ya shirika la American Airways ilikuwa ikionekana angani, watu wakajiandaa vilivyo, wale ambao walikuwa wamesimama kwa mbali wakaanza kusogea karibu na uwanja ule, Polisi ambao walikuwa mahali pale wakaanza kuwazuia watu kutokusogea karibu zaidi.
Waandishi wa habari wakaanza kuipiga picha ndege ile mpaka inatua bado zoezi lao wa upigaji picha lilikuwa likiendelea. Ndege ikasimama na abiria kuanza kuteremka, kila mtu macho yake yalikuwa makini kumtafuta Patrick.
Abiria waliendelea kuteremka zaidi na zaidi. Vanessa alikuwa amesimama huku akionekana kutokuamini kama siku hiyo ingekuwa siku yake ya kwenda kumuona Patrick ambaye alisadikiwa kufa kisiwani. Abiria wakamalizika, watu wakasimama vizuri, Patrick akaanza kuteremka.
Umati wote wa watu ukaanza kuripuka kwa furaha huku maua yakirushwa angani. Hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba Patrick, mshindi wao ndiye ambaye alikuwa akiteremka ngazi za ndege ile huku akiwa na kofia kubwa.
Watoto ambao walikuwa na maua mikononi mwao wakaanza kupiga hatua kumfuata Patrick huku wakiwa pamoja na Bwana Thomson. Patrick hakuonekana kuamini, akabaki akipunga mikono yake hewani huku kelele za shangwe zikiendelea kusikika mahali pale.
Patirick akakabidhiwa maua yae na watoto wale huku waandishi wa habari wakiendelea kupiga picha na kuchukua kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea mahali pale. Kila mtu alikuwa akitaka kumgusa Patrick lakini Polisi ambao walikuwa mahali pale walikuwa wakiwazuia watu hao.
Vanessa akapiga hatua zaidi, kutokana na Polisi kumfahamu vilivyo, wakamuachia. Vanessa akamsogelea Patrick na kumkumbatia. Machozi yalikuwa yakimtoka Vanessa, hakuamini kama alikuwa amemuona Patrick kwa mara nyingine tena.
“I cant believe...I cant believe..(Siamini...siamini...)” Vanessa alimwambia Patrick hku akimwangalia usoni na mikono yake ikiwa begani.
Bwana Thomson akampa mkono Patrick na wote kusalimiana kwa furaha na kisha kuingia garini na safafri ya kuelekea katika hoteli ya Huddlesfield kuanza mara moja. Ndani ya gari ilikuwa ni furaha tupu, muda wote Vanessa alikuwa akimwangalia Patrick huku akionekana kutokuamni kama yule ambaye alikuwa pembeni yake alikuwa Patrick.
Sherehe kubwa ikafanyika katika ukumbi wa hoteli hiyo huku viongozi wengi wa Serikali wakiwa wamehudhuria huku baadhi ya wanafunzi na walimu wa Vanguard wakiwa katika ukumbi huo. Ilionekana kuwa siku ya shangwe ambayo kwa Patrick ilionekana kuwa historia ambayo hakuwa akiamini.
Katika sherehe hiyo, Patrick akakabidhiwa ubalozi kutoka katika shirika la Umoja wa Mataifa. Kitu ambacho alitakwa kukifanya baada ya wiki kumalizika ni kutembelea katika nchi mbalimbali kwa lengo la kuwaangalia wagonjwa pamoja na watoto ambao walikuwa katika matatizo mbalimbali.
Mchungaji Smith na familia yake muda wote walikuwa wakijisikia furaha, kitendo cha Patrick kuwa mmoja wa familia yao kilionekana kuwafurahisha kupita kawaida. Muda wote Patrick alipokuwa akiongea alikuwa akimtaja mchungaji Smith na familia yake kwa kuwapa ushirikiano mkubwa katika maisha yake.
Patrick alipoulizwa kuhusu historia ya maisha yake, akaanza kueleza kuanzia mwanzao hadi katika kipindi ambacho alisafiri na kuelekea nchini Marekani. Hakukuwa na mtu aliyeamini kama duniani kulikuwa na mtu ambaye alikuwa amepitia matatizo kiasi kile. Watu ambao walikuwa na mioyo dhahifu, walikuwa wamelia kupita kawaida.
Sherehe ilichukua masaa matano, ikaisha na kisha Patrick kubaki hotelini hapo akipumzika huku ulinzi ukiwa umeimarishwa mahali hapo.
Usiku, Patrick hakulala, muda wote alikuwa akimfikiria Victoria, bado alijiona kuwa na uhitaji mkubwa wa kumuona msichana huyo ambaye alikuwa kila kitu maishani mwake. Alikumbuka mambo mengi ambayo alifanya na msichana huyo katika kipindi ambaco alikuwa nchini Tanzania.
Patrick akapania kuja nchini Tanzania ambapo angepata nafasi ya kuelekea katika kijiji cha Wami na kuonana na msichana ambaye alikuwa akimpenda kwa moyo wote, Victoria.
******
Wiki ikakatika, maandalizi ya Patrick kama balozi kutembelea nchi mbalimbali zilizokuwa na watu wengi waliokuwa na matatizo mbalimbali yakaanza. Muda wote Patrick alikuwa akionekana kuwa na furaha kupita kawaida, akili yake ilikuwa ikifikiria kwenda nchini Tanzania tu.
Katika kipindi cha mwezi huo, Patrick alitakiwa kutembelea nchi tatu za Afrika, ratiba ambayo aliletewa ilikuwa ni nchi ya Misri, Namibia na Sudan.
Patrick hakutaka kwenda peke yake barani Afrika, alitaka kwenda pamoja na Vanessa ili kumuonyeshea sehemu ambayo alikuwa ametokea. Umoja wa Mataifa haukuwa na kipingamizi, wakakubali ombi la Patrick. Bado Patrick alionekana kuhitaji uangalizi mkubwa jambo ambalo liliifanya Umoja wa Mataifa kuwaandaa vijana wawili, msichana Matilda pamoja na mvulana Simpson kwenda pamoja na Patrick barani Afrika.
Ndani ya ndege Patrick alionekana kuwa na furaha, hakuamini kama muda huo alikuwa ndani ya ndege kurudi barani Afrika. Muda wote alikuwa akijiona kuwa kama ndotoni ambako baada ya muda angeshtuka na kujikuta yuko kijijini kwao, Chibe.
Baada ya masaa kumi na mbili, ndege ikaanza kutua katika uwanja wa kimataifa wa Kairo. Watu wengi walikuwa wamesimama huku wakiwa na fulana zilizokuwa na picha za Patrick. Muda wote nyimbo mbalimbali za kiarabu zilikuwa zikiimbwa mahali hapo.
Patrick hakuonekana kuamini, idadi ya watu zaidi ya elfu tatu ambayo ilikuwa uwanjani hapo ilionekana kumshangaza kupita kawaida. Ndege ikakanyaga ardhi na baada ya muda kusimama. Patrick hakutaka kuchelewa ndani ya ndege, moja kwa moja akaanza kuteremka pamoja na Vanessa.
Watu wote wakaanza kupiga kelele za shangwe, Patrick akapiga magoti chini, akaipeleka mikono yake hewani na kumshukuru Mungu kwa kurudi Afrika kwa mara nyingine. Akaanza kushuka ngazi za ndege. Waziri Mkuu wa Misri, Abdurahiman Raziffa akaanza kupiga hatua kumfuata Patrick, alipomfikia, akamkumbatia na kisha kumbusu shavuni.
Waandishi wa habari walikuwa wakiendelea kupiga picha huku kelele za shangwe zikiwa zimetawala mahali hapo. Watu hawakuamini kama kweli wangeweza kumuona Patrick macho kwa macho maishani mwao. Kitendo cha kumuona Patrick kilionekana kuwa kama tukio la kukumbukwa maishani mwao.
Mara baada ya Patrick kuwasalimia watu waliokuwa mahali pale, safari ya kuelekea katika hospitali kuu ya hapo Misri kuanza. Garini, Patrick alikuwa amepakizwa katika gari ambalo lilikuwa wazi kwa juu, watu walikuwa wamezunguka barabara nzima kuanzia uwanja wa ndege mpaka hospitalini.
Muda wote Patrick alikuwa akiwapungia watu mikono, watu wengine walikuwa wakilia, hawakutarajia katika maisha yao kwamba siku moja wangeweza kumuona Patrick. Safari ile iliendelea zaidi mpaka katika kipindi ambacho msafara ule unaingia katika eneo la hospitali ile.
Patrick akateremka kutoka katika gari ambalo alikuwa yeye pamoja na dereva na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo la hospitali ile huku pembeni yake akiwepo Bwana Raziffa. Wote wakaanza kutembea katika chumba kimoja baada ya kingine, wagonjwa wakaonekana kupata nafuu, kitendo cha kumuona Patrick hospitalini pale kulionekana kuwafariji kupita kawaida.
Patrick aliendelea kutembea katika kila chumba hospitalini mule huku ulinzi ukiendelea kuwekwa kila alipokuwa. Kila alipokuwa akipita, waandishi wa habari walikuwa wakiendelea kupiga picha kwa ajili ya kuzionyesha katika televisheni pamoja na kuzitoa katika magazeti mbalimbali.
Patrick aliangalia wagonjwa kwa takribani masaa mawili, baada ya hapo akaanza kuelekea nje ambako baada ya muda safari ya kuelekea katika Ikulu ya nchi hiyo kuanza.
Watu wakazidi kushangilia kupita kawaida katika kipindi ambacho Patrick alikuwa akipiga hatua kuelekea nje ya jengo lile la hospitali ile huku pembeni yake akiwepo Vanessa. Bado alikuwa akiendelea kupuga mikono hewani huku tabasamu pana likionekana usoni mwake. Patrick, Vanessa, Matilda na Simpson wakaanza kupiga hatua kulifuata gari lile, walipolifikia, wakaingia ndani.
Wala hazikupita sekunde nyingi, mara mlipuko ukasikika mahali hapo, gari lilionekana kulipuka. Watu wakapiga kelele huku wakikimbia huku na kule.
“Patrick....Patrick....” Watu walisikika wakiita.
*****
Bwana Khan alionekana kukasirika, kitendo cha vijana wake kutoweza kumuua Patrick kilionekana kumuudhi kupita kawaida. Wasiwasi ukaonekana kumshika kwamba ni lazima Patrick angesema kile ambacho kilikuwa kimeendelea nchini Ujerumani, hasa mambo yake.
Kitu alichokitaka kwa wakati huo ni kumnyamazisha milele, aufunge mdomo wake na aiongee tena. Alichokifanya ni kuandaa vijana wawili ambao alikuwa akiwaamini sana katika kufanya kazi za uuaji. Akawapa pesa za kutosha na kisha kuwatuma kuelekea nchini Marekani.
Bwana Khan alitaka kumuangamiza Patrick kwa haraka sana, hakutaka kujiharibia kabisa juu ya kitu ambacho kilikuwa kinaendelea maishani mwake, alitaka siri ya kuwaua watu weusi iendelee kudumu maishani mwake.
Vijana wake, Biholf na Maxwell wakasafiri mpaka nchini Marekani. Walijitahidi kwa nguvu zao zote lakini wala hawakufanikiwa jambo ambalo lilioekana kumuongezea wasiwasi Bwana Khan. Hakuwataka vijana hao warudi nchini Ujerumani, aliwataka waendelee kubaki nchini Marekani mpaka kazi yake itakapokamilika. Aliwatumia kiasi cha fedha chochote ambacho walikuwa wakikihitaji pamoja na malupulupu mengine ili mladi tu kazi yake ikamilike.
“Anasafiri na kwenda barani Afrika” Biholf alimwambia Bwana Khan.
“Safi sana. Hiyo ndio nafasi nzuri. Ngoja niwatumie fedha za kutosha na ninyi msafiri kuelekea huko. Hakikisheni mnamuulia huko” Bwana Khan aliwaambia.
“Sawa bosi”
“Ninataka mmuue hata kwa kumpiga risasi” Bwana Khan aliwaambia.
“Hiyo naona haitowezekana bosi, naona kama atanusurika kwa kuwaishwa hospitalini” Biholf alimwambia Bwana Khan.
“Kwa hiyo ninyi mmeonaje?”
“Tumlipue na bomu”
“Itawezekana vipi?”
“Hiyo tuachie sisi. Kila kitu kitakuwa kama kilivyopangwa”
“Lakini inabidi mniambie mtafanyaje”
“Tutatega bomu katika gari atakalopanda, baada ya hapo, puuuuuuuuu...kwisha habari yake” Biholf alimwambia.
Huo ndio mpango ambao ulikuwa umepangwa. Walikuwa wakifuatilia kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea. Ratiba yote ya Patrick ilikuwa mikononi mwao. Siku mbili kabla ya Patrick kusafiri kuelekea barani Afrika nchini Misri, wakaanza kusafiri wao huku lengo lao likiwa ni kulizoea jiji la Cairo.
Baada ya kufika katika jiji hilo, wakachukua chumba katika hoteli ya Pharaoh na kisha kuanza kupanga mipango yao. Wakajadiliana kuhusu kutengeneza bomu, kutokana na mafunzo makubwa waliyokuwa nayo, wakatengeneza bomu ambalo lingelipuka mara baada ya gari kwenda chini kutokana na uzito tofauti na ule ambao ulikuwa kabla.
Siku ambayo Patrick alikuwa akiingia katika hospitali ya Taifa ya Misri, Biholf na Maxwell walikuwa wamekwishaingia. Katika kipindi ambacho Patrick alikuwa akiingia ndani ya jengo la Hospitali hiyo, Biholf akaanza kupiga hatua kulifuata gari lile ambalo alikuwa amekuja nalo Patrick, alipolifikia akalitegesha bomu ambalo lilikuwa limetegeshwa kwa mtindo wa uzito, kwamba lingelipuka mara baada ya gari kuongezeka uzito hasa baada ya mtu kuingia.
Kutokana na maaskari wa pale kuwa bize kumuangalia Patrick, hawakuona kabisa kama Biholf alikuwa amekwenda katika gari lile alilokuja nalo Patrick na kutegesha bomu. Biholf na Maxwell wakatulia ndani ya gari walilokodi huku wakifuatilia kila kitu.
Walipomuona Patrick akitoka nje ya jengo la Hospitali ile, wakaanza kuondoka mahali hapo. Wala hazikupita sekunde zaidi ya ishirini, sauti ya mlipuko mkubwa ukasikika nyuma yao kutoka hospitalini.
“Kazi nzuri” Maxwell alimwambia Biholf huku akikenua.
Patrick amelipuliwa!
Je, nini kitatokea?
Post a Comment