ad

ad

SI KITU BILA PENZI LAKO-20

 
NYEMO CHILONGANI
Ilikuwa ni siri kubwa sana ambayo ilikuwa ikiendelea katika maisha ya Bruno Deutcsher. Mara kwa mara alikuwa akielekea katika kisiwa Rogen kwa ajili ya kuwawinda wanyama wadogo wadogo ambao alikuwa akiwatumia kutengenezea gundi iliyokuwa ikitumiwa sana nchini Ujerumani.
Biashara hiyo ikaonekana kumuingizia fedha nyingi kiasi ambacho alinunua nyumba kubwa za kifahari pamoja na magari kadhalika. Ingawa jina lake halikuwa kubwa kama majina ya wafanyabiashara wengine lakini Bruno alikuwa akiheshimika sana.
Mara kwa mara alikuwa akielekea katika kisiwa cha Rogen ambako huko alikuwa akiendelea kuwauwa wanyama mbalimbali na kisha ngozi zao kutengenezea gundi. Miaka yote hiyo ndio ilikuwa kazi yake kubwa, kuwauawa wanyama na kisha kutengeneza gundi.
Kitu kilichomfanya kufanya kila kitu kisiri ilitokana na serikali ya Ujerumani kuweka ulinzi mkubwa sana katika kisiwa cha Rogen. Hakutakiwa mtu yeyote kuingia katika kisiwa hicho kwani kilikuwa kisiwa chenye wanyama wakali ambao hata wengine hawakupatikana katika sehemu yoyote ya Ulaya.
Bruno hakuonekana kuogopa, bado alikuwa akielekea katika kisiwa kile huku mikononi mwake akiwa na bunduki pamoja na mikuki iliyokuwa na sumu kali. Kila mnayama ambaye alikuwa akimuona mbele yake, alikuwa halali yake.
Sauti za watu zilikuwa zikisikika kutoka katika sehemu ambayo wala haikuwa na miti mingi. Bruno akaonekana kushtuka kupita kawaida. Hakuamini kama katika kisiwa kile kungekuwa na watu wengine ambao walikuwa wakija porini pale. Maswali kibao yalikuwa yakimiminika kichwani mwake juu ya watu wae ambao walikuwa wamefika katika kisiwa kile.
Hofu ya kudhani kuwa watu wale walikuwa walinzi ikaanza kumuingia, alitamani kukimbia ili kuepuka kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Kila alipotaka kukimbia, akajikuta akisimama na kusonga mbele kuangalia ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea.
Wanaume wawili walikuwa wakionekana vizuri machoni mwake huku kijana mmoja akiwa chini akilia. Mara mlio wa bunduki ukasikika, Patrick akushika mguu wake na kuanza kulia. Risasi ilikuwa imezama mguuni mwake na kuutoboa mfupa wa ugoko wake.
Kilio kikubwa kilikuwa kikisikika kutoka kwa Patrick, kilio kile kilimfanya Bruno kushikwa na huruma kupita kawaida. Vijana wale walikuwa wakiendelea kufurahia, kilio ambacho alikuwa akilia Patrick kilionekana kuwapa furaha kupita kawaida.
“Tutaendelea kupanda juu” Sauti ya kijana mmoja ilisikika.
Akaikoki tena bunduki yake na kisha kujiandaa kumpiga tena na risasi. Mara akashtukia mkuki ukiwa umezama shingoni mwake. Kijana mwingine, hata kabla hajapata wazo la nini alitakiwa kufanya, nae akashtukia mkuki mwingine ukizama shingoni mwake.
Kutokana na sumu kali iliyokuwa imepakwa katiika mikuki ile, wakajiukuta wakianguka chini. Bruno akaanza kupiga hatua za haraka haraka kumfuata Patrick mahali pale alipokuwa. Bado Patrick alikuwa akilia kwa maumivu makali huku akiwa ameushika mguu wake, mfupa wake wa mguu wake ulikuwa umevunjika.
Kitu alichokifanya Bruno ni kuzichukua nguzo za Patrick na kuzipaka damu ambazo zilikuwa zikiendelea kuwatoka vijana wale ambao alikuwa amewapiga mikuki ya shingoni. Alipomaliza kuwapaka, akaibeba miili ile na kwenda kuificha porini zaidi.
Alipomaliza akarudi pale alipokuwa Patrick na kisha kuanza kumbeba huku akiwa mtupu. Bruno alifanya vile makusudi huku akiwa na lengo la kutaka kuwapiga changa la macho watu ambao wangefika mahali pale kwa kutaka kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimeendelea kwa kuamini kwamba watu wale walikuwa wamekuja na wenzao ambao waliwaacha katika boti yao.
Patrick alikuwa katika hali mbaya sana, mguu wake ulikuwa umejeruhiwa vibaya na risasi ile ambayo ilimuingia. Akapakiwa botini na safari ya kuelekea mjini kuanza.
Bruno alikuwa akiendesha boti kwa kasi, alitaka kufika ufukweni haraka ambako hapo angechukua gari lake na kisha kuelekea nyumbani kwake. Ndani ya dakika kumi, akawa amekwishafika ufukweni. Ukimya ulikuwa umetawala mahali hapo kutokana na njia ile ambayo mara kwa mara alikuwa akiitumia kuwa njia ya panya.
Akambeba Patrick mgongoni na kisha kumuingiza garini na safari ya kuelekea nyumbani kwake kuanza. Maswali kibao yalikuwa yakimiminika kichwani mwake, alitamani sana kumfahamu mtu ambaye alikuwa amembeba lakini kutokana na giza kuwa kubwa, wala hakuweza kumfahamu japokuwa alijua kwamba mtu yule alikuwa mweusi.
Mara baada ya geti la nyumba yake kufunguliwa, moja kwa moja akaliingiza gari lake na kisha kumshusha Patrick garini na kuanza kuelekea nae ndani ya nyumba yake huku aiwa amembeba begani mwake. Alipomfikisha katika chumba kimoja ambacho kilionekana kuwa kama zahanati ndogo, akamlaza katika kitanda.
Akachukua simu yake na kumpigia daktari wake ambaye alimtaka afike mahali hapo haraka iwezekanavyo. Ni ndani ya dakika kumi, daktari akawa amefika mahali hapo ambapo akaanza kukiosha kidonda cha Patrick na kisha kuanza kuitoa risasi ambayo ilikuwa ndani ya mfupa wake ugokoni.
“Kweli mguu utarudi katika hali ya kawaida kweli?” Bruno alimuuliza Dokta Paul.
“Utarudi, ila atachukua muda mrefu kidogo kitandani. Baada ya hapo tutampa kibaiskeli cha kutembelea huku mguu wake ukiwa kwenye P.O.P” Dokta Paul alisema.
Maisha ya Patrick yalikuwa juu ya kitanda ndani ya nyumba hiyo, hakutakiwa kutoka kwenda sehemu yoyote ile. Kila siku dokta Paul alikuwa akifika nyumbani hapo kwa ajili ya kuhakikisha matibabu kwa Patrick. Wote walikwishajua kwamba mtu ambaye walikuwa wakimtibia alikuwa yule Patrick ambaye alikuwa amechaguliwa kuwa mchoraji bora na ndiye ambaye alikuwa ametangazwa kuuawa porini kwa kuliwa na wanyama wakali.
Waliendelea kukaa na Patrick kwa muda mrefu mpaka pale alipopata nguvu ya kukaa juu ya kibaskeli na kukifanya kuwa miguu yake. Kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea ndani ya nyumba ile kilioekana kuwa siri kubwa kwani waliamini kama siri ingetoka basi mtu ambaye aliwatuma vijana wale kumuua Patrick wangefika mahali pale na kumuua.
Miezi mitatu ikakatika na Patrick kuanza kujisikia nafu, kutokana na dawa kali ambazo alikuwa amepewa, akaanza kutembea kwa kuchechemea mpaka pale ambapo akaanza kutembea kamakawaida.
Kitu ambacho alikuwa akikitaka kukifanya mahali hapo ni kumpigia simu mchungaji Smith pamoja na familia yake na kuwaambia kuwa yeye ni mzima na alitarajiwa kurudi nchini Marekani siku yoyote ile.
“Unajisikia vizuri kabisa?” Bruno alimuuliza.
“Ndio. Ninajisikia vizuri” Patrick alijibu.
“Ila kuna kitu ningependa usikiseme kwa mtu yeyote yule” Bruno alimwambia Patrick.
“Kitu gani?”
“Jinsi nilivyokuokoa kisiwani. Unajua kama utasema kila kitu, utaniweka katika wakati mgumu sana kwani serikali itanikamata kwa kuingia ndani ya kisiwa kile” Bruno alimwambia Patrick.
“Usijali Bruno. Kwa kuwa umeniokoa katika mdomo wa kifo, amini kuwa sitoongea kitu chochote kile” Patrick alimwambia Bruno na kisha kuchukua simu kumpigia mchungaji Smith pamoja na Vanessa kuwataharifu juu ya uwepo wake.
*****
Furaha haikupatikana kwa Vanessa, kila siku alikuwa mtu wa majonzi. Moyo wake ulikuwa umeumia kupita kiasi. Maisha kwake pasipo Patrick yalionekana kuwa ya kinyonge kupita kiasi. Vanessa alikuwa katika wakati mgumu kupita kawaida, machozi ndio ilikuwa sehemu ya maisha yake.
Furaha yote ambayo alikuwa nayo katika kipindi alichokuwa na Patrick ikaonekana kupotea. Afya yake ikaanza kuonekana kudhoofika kutokana na mawazo aliyokuwa nayo juu ya Patrick ambaye hadi katika kipindi hicho, kila mtu alikuwa akijua kwamba alikufa kisiwani.
Siku nyingine Vanessa hakuwa akielekea shuleni, kila alipokuwa akiziangalia sehemu ambazo mara kwa mara alikuwa akipenda kukaa pamoja na Patrick, alionekana kuumia kupita kawaida. Maisha yake yakaonekana kubadilika, Vanessa yule ambaye alikuwa katika kipindi kile cha nyuma pamoja na Patrick alionekana kuwa tofauti na Vanessa huyu ambaye alikuwa katika kipindi hiki.
Kila wakati Vanessa alikuwa akiangalia simu yake, jina la Patrick lilikuwa likionekana vizuri simuni mwake. Bado maumivu makali yalikuwa yakiendelea kuwepo moyoni mwake.
Miezi miwili ilikuwa imepita tangu wamazike Patrick katika makaburi ya Louis ambayo palikuwa pakizikwa watu waliokuwa maarufu. Vanessa aliyatamani maisha yake ya zamani ambayo yalikuwa na furaha lakini kila kitu kikaonekana kubadilika.
Vanessa akashtuka kutoka katika lindi la mawazo mara baada ya kuisikia simu yake ikianza kuita. Simu iliendelea kuita, Vanessa akaichukua na kuanza kuiangalia. Namba ikaonekana kuwa ngeni machoni machoni mwake, alichokifanya ni kuikata ili kumuondolea usumbufu.
Akasimama katika kiti ambacho alikuwa amekalia na moja kwa moja kuelekea katika kiti kingine darasani pale alipokuwa. Simu ile ikaanza kuita tena, wanafunzi wote wakaanza kumuangalia. Vanessa akaichukua simu ile na kuangalia tena kioo, namba ile ngeni ndio ambayo ilikuwa ikipiga tena, alichokifanya ni kuikata tena.
Vanessa alionekana kuchanganyikiwa na hali ambayo alikuwa amekutana nayo katika kipindi hicho. Hakuonekana kuhitaji usumbufu wowote ule. Alionekana kuhitaji muda mwingi wa kupumzika kuliko kuongea ovyo na watu. Kuna kipindi alikuwa akiichukia sana simu yake kwani muda mwingi ilimfanya kutokutulia kutokana na watu wengi kumpigia simu na kumpa pole kwa kile kilichotokea.
Simu ile ikaanza kuita kwa mara ya tatu, Vanessa akaiangalia simu ile na kuikuta namba ile ile ambayo ilikuwa ngeni simuni mwake. Kama kawaida yake, akaikata na kuizima kabisa simu yake. Vanessa akailalia meza yake ya kusomea na kutulia.
Mara mwalimu Kerri akaingia darasani hapo na macho yake kuanza kuangalia huku na kule hali iliyoonyesha kwamba alikuwa akimtafuta mtu fulani. Alipomuona Vanessa, akaanza kupiga hatua kumfuata huku wanafunzi wengine wakimwangalia.
Alipomfikia, akamuinua na kisha kumwambia kwamba amfuate ofisini. Vanessa akainuka na moja kwa moja kuanza kumfuata mwalimu Kerri. Vanessa hakuonekana kuelewa sababu ambayo ilimfanya mwalimu Kerri kuja kumuita na kwenda nae ofisini pasipo kuongea kitu chochote kile.
Macho yake yakatua kwa mchungaji Smith pamoja na mkewe, Rachel ambao macho yao yalikuwa yamejawa na tabasamu pana. Vanessa akaonekana kushtuka, akaanza kujiuliza maswali kibao kuhusiana na tabasamu yale lakini hakupata jibu.
“Kuna nini?” Vanessa aliuliza huku akionekana kushangaa.
“Habari njema” Mchungaji Smith alijibu.
Vanessa akaonekana kushtuka, hakujua habari njema hizo zilizozungumziwa na mchungaji Smith zilimaanisha nini kwake. Akajiona kuwa na hamu ya kutaka kuzisikia habari hizo njema ambazo mchungaji Smith pamoja na mkewe, Rachel walikuwa wamekuja nazo mahali hapo.
“Habari njema kuhusu nini” Vanessa aliuliza.
“Patrick....” Mchungaji alijibu.
Vanessa akanyong’onyea, akamuona mchungaji kumtonesha kidonda ambacho kilikuwa kimeanza kupona. Akaanza kumkumbuka zaidi Patrick ambaye walikuwa wamemzika miezi miwili iliyopita. Akayapeleka macho yake kwa walimu wengine ambao walikuwa ndani ya ofisi ile, walimu wote walikuwa wakionyesha nyuso zilizojaa tabasamu.
“Patrick anakuja. Patrick hakufa kama ilivyotangazwa. Nimeongea nae simu na amesema kwamba anakuja. Ninafikiri kwa sasa atakuwa ndani ya ndege” Mchungaji alimwambia Vanessa.
Vanessa akaonekana kushtuka, hakuamini kama kweli kitu alichokuwa akikisikia masikioni mwake kilikuwa kweli au si kweli. Alijiona kuwa ndotoni ambako baada ya muda angeamka kutoka katika usingizi mzito. Akajaribu kuyafikicha macho yake kuona kwamba alikuwa ndotoni au katika uhalisia.
“Unasemaje?” Vanessa aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Patrick anakuja. Kwani hakukupigia simu nusu saa iliyopita?” Mchungaji alimuuliza Vanessa.
Mawazo ya Vanessa yakarudi katika simu ambayo alikuwa amepigiwa katika kipindi kichache kilichopita. Akaanza kujuta kwa kitendo chake cha kutokuipokea simu ile ambayo ilikuwa ikiingia katika simu yake. Vanessa akaonekana kuumia kupita kawaida.
Akaichukua simu yake kutoka mfukoni, akaiwasha na kuanza kuitafuta namba ile ambayo ilikuwa imeingia katika kipindi kichache kilichopita. Alipoipata, akaanza kuipiga. Simu ile ikaanza kuita, iliendelea kuita zaidi na zaidi, ikapokelewa na sauti nzito kusikika.
“Patrick......” Vanessa aliita.
“Wewe ni nani?” Sauti ya Bruno ilisikika.
“Rafiki yake, Vanessa. Alinipigia simu muda mchache uliopita. Naomba kuongea nae” Vanessa alimwambia Bruno.
“Hayupo. Amepanda ndege kuja huko Marekani. Nafikiri kesho asubuhi ataingia” Bruno alimwambia Vanessa ambaye akakata simu.
Vanessa akashindwa kujizuia, machozi ya furaha yakaanza kumtoka. Hakuamini kama kweli Patrick yule ambaye alikuwa ameambiwa taarifa zake ndiye alikuwa Patrick yule ambaye alikuwa akija na ndege kutoka nchini Ujerumani.
Mwalimu mkuu akaanza kuelekea katika ofisi yake ambako akakichukua kipaza sauti kidogo na kuanza kuongea. Kutokana na vispika vidogo vilivyokuwa viemchomekwa katika kila pembe shuleni hapo, sauti yake ilikuwa ikisikika vizuri.
Taarifa juu ya Patrick ikatolewa, hakukuwa na mtu ambaye alionekana kuamini. Wanafunzi wa shule ya Vinguard waliona tukio hilo kuwa kama muujiza mkubwa ambao wala haukutarajiwa kutokea katika maisha yao. Kila mmoja akawa na kiu ya kutaka kumpokea Patrick ambaye alitarajiwa kuongia asubuhi ya siku inayofuatia.
Ni ndani ya dakika sabini tu, waandishi wa habari wakaanza kufika shuleni pale na kutaa kupata ukweli wa mambo. Kile ambacho walikuwa wamekisikia ndicho ambacho waliambiwa shuleni hapo. Taarifa ikatangazwa katika vyombo vyote vya habari nchini Marekani.
Kila mtu ambaye alizisikia habari zile alionekana kutokuamini kabisa. Watu wakajiandaa vilivyo kumpokea Patrick, watoto ambao kazi yao ilikuwa ni kubeba maua wakatafutwa. Serikali ya Marekani ikamuzandaa Waziri wa Mambo ya Ndani Bwana Thomson kwa ajili ya kusimamia mapokezi uwanjani hapo.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.