Sophia Simba: Sina Mpango wa Kuiunga na Chama Chochote cha Upinzani
Aliyekuwa
mwanachama mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Umoja
wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba ambaye alifukuzwa uanachama kwa
usaliti, amezungumzia hatua aliyoichukua baada ya uamuzi huo dhidi
yake.
Wikendi
iliyopita, CCM ilitangaza kumvua uanachama Mwanasiasa huyo baada ya
kumtia hatiani, ambapo taarifa zinadai kuwa yeye alibainika kwenda
nyumbani kwa aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Edward
Lowassa hata baada ya uchaguzi mkuu akiwa amevalia hijabu kujificha.
Hali iliyotafsiriwa kuwa alikuwa akimpelekea siri za chama.
Baada
ya uamuzi huo wa CCM kutangazwa, Lowassa alimkaribisha Sophia Simba na
wenzake 12 waliofukuzwa, kujiunga na Chadema huku akiwaita mashujaa
waliokuwa wanatetea demokrasia ndani ya chama hicho tawala.
Hata
hivyo, Sophia Simba amesema kuwa hana mpango na hatahamia katika chama
chochote kwani maisha yake yote yametokana na kuitumikia CCM.
Mwanasiasa
huyo ambaye alijiunga na CCM tangu ilipozaliwa mwaka 1977 na kushika
nyadhifa mbalimbali baadae, amesema kuwa atabaki kuwa mkereketwa wa
chama hicho.
“Napenda
kuwaeleza Watanzania wote, wafahamu kuwa sina mpango wowote wa kujiunga
na upinzani. Na unajua CCM ina makundi mawili, la kwanza ni wanachama
wenye kadi na la pili wakereketwa ambao ni wengi. Na mimi nitaingia
katika kundi hilo na sio kuhama,” Sophia Simba anakaririwa na Mtanzania.
Aidha,
alikanusha taarifa zilizokuwa zimeripotiwa kwenye baadhi ya mitandao
kuwa amekutana na mwanasiasa mmoja wa upinzani. Alisisitiza kuwa
hakufanya hivyo na hana mpango huo.
Akizungumzia
tuhuma za kukisaliti chama hicho zilizopelekea kung’olewa kwake,
alikana kuwa msaliti wa chama hicho ingawa alisisitiza kuwa hataki
kulizungumzia kwa undani bali anamuachia Mungu anayeiona nafsi yake.
“Sitaki
kuzungumzia kwa udani suala la usaliti ila kwa ufupi, Mungu
anaishuhudia nafsi yangu. Jamani, hivi kweli nikisaliti chama changu
ambacho kimenilea katika maisha yangu yote!”
Katika
hatua nyingine, alisema kuwa hana mpango wa kwenda mahakamani kutafuta
haki ya kurejea ndani ya chama hicho kwani kufanya hivyo ni kukosa
fadhila kwa jinsi ambavyo chama hicho kimempa maisha.
Mwanasiasa huyo mkongwe alisema kuwa amepokea adhabu aliyopewa kwa mikono miwili na kwamba hana kinyongo.
Post a Comment