Sakata la Diamond na Shigongo Lachukua Sura Mpya, Bab Tale Aingilia Kati, Amchana Shigongo
Muda mfupi baada ya Mwandishi wa vitabu, Eric Shigongo kuandika kwenye ukurasa wake wa Facebook ujumbe aliouita 'MY CONFESSION' unaomhusu mwanamuziki Diamond Platnumz kuwa anapoelekea kuna shimo na asipoliruka atatumbukia na ndiyo utakuwa mwisho wake huku akieleza kuwa kwenye shimo hilo Diamond anapelekwa na watu watatu ambao ni NASEEB ABDUL, BABU TALE NA SALAAM, hatimaye mmoja wa mameneja wa Diamond, Bab Tale ameibuka na kutoa ya moyoni.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Shigongo ameweka alichokiandika Bab Tale ambacho kinasomeka hivi; "Kwa hiyo unataka kututoa shimoni kwa njia ya kutupost boss au ulikuwa unahitaji follow? Wasukuma bwana? haya Mungu yupo." ameandika Bab Tale huku Shigongo naye akijibu hivi;
"Tulia Tale! hujaelewa lengo, wewe mwanafasihi. Utajua nikimaliza, siwezi kumuumiza Diamond."
Baada ya kumjibu Tale, Shigongo aliandika ujumbe huu na kuendelea na CONFESSION yake;
Mawasiliano ya Shigongo na Bab Tale. |
Jana dakika chache tu baada tu ya kuposti nilichokiandika juu ya Diamond Platnumz, Babu Tale, meneja wake, alinitumia ujumbe huo hapo juu, nafikiri kwa sababu ni mtani wangu;
NAENDELEA…
Wakati fulani nilikuwa nimeandaa tamasha la bure huko Tandale, eneo la watu maskini kabisa kwa lengo la kuwafundisha mbinu mbalimbali za kujiondoa katika umaskini, nilifanya hivyo nikiamini yako mambo ambayo watu waliofanikiwa huyafanya na watu wasio na mafanikio huyaepuka.
Niliwaomba wasanii wengi sana waje kushirikiana nami katika tamasha hilo, wengi walikataa wakidai kiasi kikubwa cha fedha, waliokubali kuimba bure kwenye tamasha hilo ni R.O.M.A na Kala Jeremiah, nikiwa na idadi ya wasanii wawili tu na sitaki kutumia fedha kumlipa msanii kwenye jambo la kijamii kama hilo hatimaye niliamua kumpigia Diamond Platnumz ILI AJITOLEE NA TUFANYE KITU KWA AJILI YA JAMII.
Naomba niseme wazi, nilikuwa najaribu maana ninajua kabisa gharama zake huwa ni kubwa, nimewahi kumlipa shilingi milioni thelathini kufanya shoo moja pale Dar Live, katika hali ya kushangaza kabisa, pamoja na umaarufu wake mkubwa Diamond ALIKUBALI KUFANYA SHOO ILE BURE! Wakati msanii kama Snura aligoma.
Tukio hili lilinifanya NIMPENDE NASEEB ABDUL mara mbili zaidi ya ilivyokuwa hapo awali, ni MNYENYEKEVU, mtu wa kujishusha na asiyependa ugomvi na watu! Hakika kama mzazi ingawa sipendi sana mwanangu awe mwanamuziki, natamani kuwa na mtoto mwenye sifa hizi, sipendi majivuno, sipendi watu wanaoringa na kujiona wao ni bora kuliko wengine kwa sababu tu wana vitu fulani ambavyo wengine hawana.
Mtu yeyote akipata nafasi ya kuongea na Diamond Platnumz amuulize ni mara ngapi nimekwishaongea naye na kumshauri juu ya uwekezaji wa fedha anazozipata leo, sababu MWANADAMU HUWEZI KUWA BINGWA MILELE, siku moja lazima tu utapigwa, jua huwa haliwaki siku zote, lazima usiku utaingia, umejiandaaje kwa ajili ya usiku au siku utakapopigwa ndiyo jambo la muhimu katika maisha haya.
Upendo wangu kwa Diamond Platnumz ndiyo unaonifanya nifunguke haya ninayoyasema, maana ninashuhudia kwa macho yangu amezungukwa na watu ambao asipokuwa makini watamtumbukiza shimoni, akiwa huko shimoni watamuacha na kuchukua watu wengine tena! LAZIMA TUSEME, hata kama tutatukanwa, ilimradi tunajaribu kumsaidia mwenzetu tunayempenda.
Watu hawa watatu wanaoumzunguka DIAMOND PLATNUMZ NI BABU TALE, SALAAM, NASEEB ABDUL na hapa anaongezeka mwingine wa nne aitwaye shabiki.
Kesho nitaanza kuelezea jinsi ambavyo watu hawa wanne wanataka kumwingiza Diamond Platnumz shimoni na nini kifanyike kujiokoa.
Asanteni kwa kunisoma.
Je, confession hii ina ukweli wa jambo ndani yake au ni kiki ya kuelekea shoo ya Diamond Sikukuu ya Pasaka Dar Live? Usikose kuungana nasi kujua kinachoendelea kesho.
Post a Comment