Rais Magufuli Atuma Salamu Za Rambi Rambi Kufuatia Kifo Cha Balozi Sir George Kahama
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,
ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mmoja wa Waasisi wa Taifa na
Waziri Mstaafu Bw. George Kahama kufuatia kifo cha kiongozi huyo
kilichotokea tarehe 12 Machi, 2017.
Bw. George Kahama amefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika
Salamu zake Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mmoja wa watu
waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru, maendeleo na ustawi wa
jamii ya watanzania akiwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi hususani
kuwa miongoni mwa Mawaziri katika Baraza la kwanza la Mawaziri ambapo
alishika wadhifa huo kwa awamu tatu za uongozi wa Tanzania.
“Sir
George Kahama alikuwa kiongozi shupavu, mzalendo, mwanasiasa mahiri,
aliyewapenda Watanzania na aliyejitoa kushirikiana na viongozi wenzake
akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kupigania
uhuru, kujenga misingi ya Taifa likiwemo Azimio la Arusha, kujenga
misingi ya uchumi wa ujamaa na kujitegemea na mengine mengi, kwa hakika
hatutamsahau”
“Japo
kuwa Sir. George Kahama ametangulia mbele za haki, sisi viongozi
tuliopo tutamuenzi kwa kuhakikisha tunaendeleza juhudi za kuipigania
Tanzania aliyoshiriki kuijenga, na pia tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu
aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais
Magufuli katika salamu hizo.
Pamoja
na familia ya Marehemu Bw. George Kahama, Mhe. Dkt. Magufuli amewapa
pole nyingi wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wabunge, Ndugu,
Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
Post a Comment