FUTA MACHOZI MPENZI - 34 (MWISHO...MWISHO)
“Mamaaaa....mamaaaa...Linda...Linda mpenziiiiii....” ilisikika sauti kutoka chumbani kwa William, saa ya ukutani ilikuwa ikionyesha kwamba tayari ilifika saa nane usiku.
Alikuwa akipiga kelele kama mtu aliyechanganyikiwa, akainuka kitandani na kuanza kukimbia huku na kule chumbani mule. Alikishika kichwa chake, aliendelea kupiga kelele, aliona kama matukio yalikuwa yakijirudia kichwani mwake, alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Alijiona akiwa ndani ya gari, aliendesha kwa kasi na baada ya muda fulani akapata ajali, alichanganyikiwa, alichokuwa akikiona ilikuwa ni vigumu kuamini kama kilikuwa kichwani mwake kwani aliona kama picha mbele yake kitu kilichomfanya kupiga kelele mno.
Mama yake akatoka chumbani kwa kasi na kwenda chumbani kwa William, akamkuta akiwa kitandani huku akipiga kelele, akamfuata na kumuuliza tatizo la kupiga kelele lakini hakutoa jibu lolote zaidi ya kulitaja jina la Linda tu.
“Nini kimetokea?” aliuliza mama yake, alionekana kuchanganyikiwa kwani alihisi tayari mtoto wake alikuwa kichaa.
“Linda mama! Linda yupo wapi?” aliuliza William.
Mama yake hakuamini, ulikuwa umepita mwaka mzima tangu William apate ajali na kusahau kila kitu, alikumbuka kwamba mara ya mwisho Linda kuwa huko ni mwaka uliopita na miezi kadhaa, alikataa kumuona na kusema kwamba hakuwa akimfahamu, sasa ilikuwaje leo hii aanze kumuulizia na wakati alimfukuza.
Hakugundua kama kijana wake alikuwa amerudiwa na fahamu. Alibaki akimwangalia kwa mshangao mkubwa, alikuwa akibubujikwa na machozi kwani kitendo cha William kumkumbuka Linda kilionekana kuwa na mafanikio makubwa kwenye afya yake.
“Mama! Linda! Mama! Linda yupo wapi? Kwa nini nipo hapa! Hapa ni wapi?” aliuliza William huku akionekana kushangaa huku na kule.
Alitulia kwa muda na jinsi chumba kile alivyokiangalia akagundua kwamba alikuwa chumbani kwake. Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilitokea kwani kumbukumbu zake zilikumbuka tukio la mwisho la kupata ajali lililokuwa limetokea.
Hakujua ni kitu gani kilitokea mpaka kuwa ndani ya chumba kile. Hakutaka kuamini kama kweli pale alipokuwa palikuwa chumbani kwake, nchini Tanzania katika Mtaa wa Tabata.
Akatoka ndani na kwenda nje, akamkuta mlinzi ambaye naye alibaki akimwangalia, alizisikia zile kelele na kuangalia kwa makini mule ndani, alitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
“Hamis! Nimefikaje hapa?” alimuuliza mlinzi huku akimwangalia kwa kumshangaa.
“Mbona upo kila siku!”
“Kila siku? Inamaana kila kitu kilichokuwa kinatokea nchini Marekani kilikuwa ni ndoto?” aliuliza William.
“Hapana!”
“Sasa imekuwaje nipoi hapa? Linda yupo wapi?” aliuliza William, wakati Hamis akitaka kujibu, mama yake akatokea na kumkonyeza kwamba hakutakiwa kujibu kitu chochote kile.
“William, njoo ndani!” alisema mama yake huku akimshika mkono.
“Mama! Nataka uniambie ukweli! Kwa nini nipo hapa? Nani anasimamia mtandao wangu?” aliuliza William huku akiendelea kupigwa na mshangao.
Mama yake akamchukua na kuelekea naye ndani, aliona jinsi kijana wake alivyokuwa amechanganyikiwa. Walipofika ndani, wakakaa kochini na kuanza kuzungumza, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumuuliza alikumbuka kitu gani cha mwisho.
“Nilipata ajali jana!” alijibu William.
“Jana? Hapana! Ni mwaka na miezi kadhaa imepita! Baada ya hapo unakumbuka nini?”
“Sijajua nini kiliendelea,” alisema William.
Mama yake hakutaka kumficha, akaanza kumuhadithia kila kitu kilichotokea baada ya yeye kupata ajali. Alimsikiliza kwa makini, moyo wake uulimuuma, maneno aliyokuwa akiongea mama yake yalimshtua sana, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyemfukuza Linda.
Alihisi kabisa kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake. Linda alimpenda, alihisi maumivu mazito baada ya kujiuliza ni maumivu makali kiasi gani aliyoyasikia mwanamke huyo.
“Mama! Mimi nilimfukuza Linda?” aliuliza William, hakuamini alichokuwa amekisikia.
“Ndiyo! Ulimfukuza. Na pia kuna mwanamke mwingine!” alisema mama yake.
“Yupi?”
“Anaitwa Kesi...”
“Cassey! Ilikuwaje? Mungu wangu! Nakumbuka nilipata ajali nikiwa namfuata huyu msichana,” alisema William huku akionekana kukumbuka kila kitu.
“Naye alikuja ila ukamfukuza.”
“Mungu wangu! Nilimfukuza na Cassey pia?”
“Ndiyo!”
“Mama! Haiwezekani! Ni lazima nirudi Marekani!”
William hakutaka kuishia hapo, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuingia kwenye mtandao wake wa MeChat kuona unaendeleaje. Hakuamini, kulikuwa na zaidi ya watu milioni mia tano waliokuwa wakiutumia. Moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama aliweza kutengeneza kitu kilichokuwa na watumiaji wengi kiasi hicho.
Hakutaka kuchelewa, alizikumbuka namba za mpenzi wake, Linda hivyo kuchukua simu na kumpigia. Siku ikaanza kuita, iliita na kuita na mwisho wa siku kupokelewa na sauti ya Linda kusikika upande wa pili.
****
Moyo wa Linda ulikufa ganzi kwani mauamivu aliyokuwa akiyasikia yalizoeleka na hivyo kuwa si maumivu tena. Aliumia, hakuamini kama kweli alifukuzwa na William na hakutaka kumuona tena.
Alijua kwamba mwanaume huyo alikuwa akiumwa lakini hilo hakutaka kulijali, alihisi kwamba alikuwa mzima na kile alichokifanya kilikuwa cha makusudi kabisa.
Alirudi nchini Marekani na kuendelea na maisha yake. Huko, aliendelea kusimamia kampuni za William na masuala yote ya kifedha kwa kuamini kwamba kuna siku mumewe angerudi tena.
Mtoto wao, William Jr aliendelea kukua kama kawaida. Maisha bila William yalikuwa magumu mno kwa Linda lakini alivumilia huku kila siku akimuombea William kwa Mungu kwamba afya yake itengemae na kukumbuka kila kitu katika maisha yake.
Baada ya mwaka na miezi mitatu, akapigiwa simu mchana wa siku moja. Alipoiangalia simu ile, code zilionyesha kwamba ilitoka Tanzania na kitu alichojua ni kwamba mama yake William alikuwa amemkumbuka hivyo kumpigia kama siku nyingine japokuwa kwa siku hiyo namba ilikuwa tofauti.
“Nani anaongea?” aliuliza mara baada ya kupokea simu.
“William!” alisema William kitu kilichomfanya Linda kuishiwa nguvu za miguu, akakaa vizuri kwenye kiti.
“William?” aliuliza.
“Ndiyo mpenzi! Ninakumbuka kila kitu! Naomba unisamehe mpenzi kwa nilichokufanyia,” alisema William huku akiwa na huzuni tele.
“Nimekukumbuka mpenzi! Nimelia sana kwa ajili yako! Nimeumia kwa ajili yako mpenzi!” alisema Linda huku akianza kulia kilio cha kwikwi.
“Ninakuja hukohuko. Ninakuja kukuona mpenzi! Ninakuja kuishi na wewe na kufunga ndoa,” alisema William.
Siku iliyofuata, akakodi ndege kuelekea nchini Marekani. Hakukuwa na tatizo la viza kwani Wamarekani walimuona kama mwenzao kwa sababu alikuwa na kazi kubwa aliyokuwa akiifanya chini ya CIA.
Taarifa ikapelekwa nchini Marekani kwamba William alikuwa njiani kuelekea huko. Walichokifanya CIA ni kuwasiliana na mkewe na kumwambia kwamba hakutakiwa kumwambia mtu yeyote juu ya ujio wa William.
Ndani ya ndege William alikuwa na mawazo tele, hakuamini kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake. Wakati mwingine alibaki na kuyafikiria maneno ya mama yake kama kweli alimfukuza Linda nyumbani.
Mbali na mwanamke huyo pia akamkumbuka Cassey, alijiuliza juu ya mimba aliyokuwa nayo kama alijifungua salama au la. Safari iliendelea na baada ya saa ishirini na saba, ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK jijini New York.
Akateremka, kulikuwa na maofisa wengi wa CIA waliokuwa wakimsubiri, hakukuwa na mwandishi wa habari, mbali na maofisa hao pia alikuwepo Linda aliyekuwa na mtoto William Jr, alipomuona mpenzi wake, akaanza kumsogelea na kumkumbatia kwa furaha.
“Hatimaye umeruudi mpenzi!” alisema Linda huku akilia.
“Nimerudi kuanza maisha mapya na wewe. Futa Machozi Mpenzi! Kila kitu kilichopita, naomba ukisahau,” alisema William.
Waliendelea kukumbatiana, hakuridhika, akambeba William Jr, kila alipomwangalia macho yake yalijaa machozi kwani alihisi mapenzi mazito yakiongezeka kwa familia yake hiyo.
Hawakukaa sana wakachukuliwa na kuingia ndani ya gari ambapo safari ya kuelekea nyumbani ikaanza. Wakaelekea huko, ndani ya gari walikuwa wakizungumza mambo mengi. William hakutaka kukumbuka kilichotokea, akaanza maisha yake na Linda, kwa kipindi hicho alihitaji sana kuwa karibu na familia yake.
Baada ya siku mbili kupita akampigia simu Cassey na kumuuliza kuhusu ujauzito. Kwanza msichana huyo akafurahi kusikia kwamba William amerudiwa na kumbukumbu zake na kitu alichomuongezea ni kwamba hakuwa na mimba, alimwambia vile kwa sababu alitaka kujua ni kitu gani kingetokea.
“Wewe mpumbavu sana, ulinitisha mno,” alisema William huku akitoa kicheko, naye Cassey akaanza kucheka.
“Nilijua kwamba ungechanganyikiwa. Hujachelewa, umewahi sana. Ninafunga ndoa wiki mbili zijazo. Ungependa uwepo?” aliuliza Cassey.
“Haina shida. Niandalie kadi yangu na Linda, baada ya kwako, yangu itafuata,” alisema William, wakazungumza mambo mengine na kukata simu.
Maisha yakabadilika, akaendelea kuingiza fedha, mtandao wake wa MeChat uliendelea kumuingizia fedha, akawa bilionea na ndani ya miaka miwili akawa juu zaidi ya Mtandao wa Facebook, aliendelea kupendwa huku kila siku akifanya kazi za CIA za siri na kufanikiwa kuwapa Wamarekani siri za majeshi ya Urusi, silaha zao, Wachina, Wakorea na nchi yoyote ambayo ilikuwa adui mkubwa wa Marekani.
Na la kuongezea zaidi, yeye ndiye mtu aliyehusika kuzidukua kompyuta za Tume ya Uchaguzi Marekani kwa kuyabadilisha matokeo ya Marekani kwa kumpa Donald Trump badala ya Hillary Clinton.
MWISHO
Post a Comment