UPDATES: CHANZO CHA MOTO UWANJA WA NDEGE DAR CHAJULIKANA

Taarifa zilizotufikia hivi punde zimeeleza kuwa, chanzo cha moto mkubwa
uliozuka usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salam na kusababisha shughuli zote
za usafirishaji Uwanjani hapo kusimama kwa muda, kimejulikana kuwa ni
hitilafu ya umeme.
Akizungumza na mtandao wa Global Publshers mapema asubuhi ya leo,
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, ACP Martin Otieno amesema kuwa,
uchunguzi umebaini kwamba, kulikuwa na tatizo la umeme ambalo hata hivyo
lilishughulikiwa mara moja.
“Kulikuwa na tatizo la umeme kwenye eneo la kuhifadhia mizigo lakini
moto ulidhibitiwa vizuri na sasa shughuli zinaendelea kama kawaida
japokuwa bado tunatumia Terminal One (uwanja wa zamani) kwa kuwabeba
abiria kwenye mabasi na kuwapeleka panapohusika.
“Kwa sasa ndege zote zinatua na kuruka bila tatizo lolote na kufuatana
na ratiba hivyo hakuna hofu yoyote kwani muda si mrefu eneo hilo la
mizigo litakuwa limeshawekwa sana, ” alisema Kamanda Otieno.
Aidha Mamlaka ya Uwanja huo imetoa mabasi kwa ajili ya kubeba abiria
kuwapeleka Terminal One ambako shughuli za usafirishaji zinaendelea kama
kawaida.
Post a Comment