Mkutano wa 6 wa Bunge Kuanza Leo, Maswali 125 Kuulizwa Yakiwemo ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu
Mkutano wa Sita wa Bunge unatarajiwa
kuanza siku ya Jumanne tarehe 31 Januari 2017 na kumalizika tarehe 10
Februari 2017 Mjini Dodoma.
Mkutano huo utakuwa ni mahususi kwa ajili ya kupokea Taarifa za mwaka
za Kamati za Kudumu za Bunge ambapo Kamati 14 za kisekta na mtambuka
zitawasilisha taarifa zake Bungeni katika kipindi hiki. Shughuli
nyingine zitakazofanyika katika Mkutano huu ni kama ifuatavyo:-
1.0 KIAPO CHA UAMINIFU
Kufuatia uteuzi wa wabunge watatu
walioteuliwa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli hivi karibuni na
Uchaguzi Mdogo uliofanyika katika Jimbo la Dimani, Zanzibar Tarehe 22
Januari 2017, kutakuwa na Kiapo cha Uaminifu kwa Wabunge wapya wanne
ambao ni:-
(i) Mhe. Alhaji Abdallah Majula Bulembo
(ii) Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi
(iii) Mhe. Anne Kilango Malecela
(iv) Mhe. Ali Juma Ali – (Jimbo la Dimani)
2.0 MASWALI
Katika Mkutano huu jumla ya maswali ya
kawaida 125 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa Bungeni. Aidha, kwa mujibu
wa Kanuni ya 38 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge wastani wa maswali 16
ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yataulizwa na kujibiwa pia
siku za Alhamisi.
3.0 KAULI ZA MAWAZIRI
Aidha, katika Mkutano huu wa Bunge Kauli mbili za Mawaziri zitawasilishwa kama ifuatavyo:-
(i) Kauli ya Serikali Kuhusu Hali ya Chakula Nchini itakayotolewa Tarehe 31 Januari, 2017.
(ii) Kauli ya Serikali kuhusu Deni la Taifa na Hali ya Uchumi Nchini itakayotolewa Tarehe 31 Januari, 2017.
4.0 MISWADA YA SHERIA
Katika Mkutano wa Tano wa Bunge
uliomalizika mwezi Novemba, 2016 Miswada mitatu (3) ya Sheria ilisomwa
kwa mara ya Kwanza Bungeni na kupelekwa kwenye Kamati husika ili
ifanyiwe kazi.
Hivyo katika Mkutano huu wa Sita Miswada
hiyo inatarajiwa kuwasilishwa Bungeni kwa mara ya Pili, kujadiliwa na
kupitishwa na Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 91. Miswada hiyo ni:-
- Muswada wa Sheria ya Sheria ya Madaktari wa Meno na Wataalam wa Afya Shirikishi wa mwaka, 2016 (The Medical, Dential and Allied Health Professionals Bill 2016).
- Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa mwaka 2016 (The Legal Aid Bill, 2016).
- Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na.4) wa mwaka 2016. {The Written Laws (Miscellaneous Amendments)}, Bill, 2016)
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA
30 Januari, 2017.
Post a Comment