Lowassa, Lema Wamtembelea Sumaye Gerezani
Mawaziri
wakuu wa zamani ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, jana
wamemtembelea Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema katika Gereza Kuu la
Kisongo mjini Arusha.
Lowassa
akiongozana na Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye pia ni
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika
katika gereza hilo.
Calist
alisema Lowassa alifika gerezani hapo saa tano asubuhi huku Sumaye
aliyeongozana na Naibu Meya wa Arusha, Viola Lazaro akifika baadaye saa
saba mchana.
Calist
alisema Lowassa akizungumza na Lema, alimwambia kuwa mahakama ndiyo
chombo pekee kinachoaminiwa na wananchi, hivyo kinapaswa kutenda haki
kwa watu wote.
Alisema
Lowassa aliridhishwa na afya ya Lema na kumtaka awe mvumilivu, hasa
katika kipindi hiki anachokabiliwa na kesi na aliwataka wananchi wa
Arusha Mjini kumwombea kiongozi huyo.
“Watanzania
wana matumaini makubwa sana na mahakama, wanaamini chombo hiki pekee
ndicho kitakachowapa haki yao, hivyo kwa mwaka 2017 mahakama itoe haki
na kuendesha kesi bila upendeleo kwa sababu ndiyo sauti ya wanyonge,
nakutakia amani na mwaka mpya mwema,” Calist alimnukuu Lowassa.
Kwa
upande wake, Sumaye alisema kuwa alimtaka mbunge huyo kuwa jasiri
katika kipindi hiki kwa sababu suala linalomkabili litafika mwisho.
“Mimi
nilikuja tu kumsalimia, kumjulia hali ya afya yake kwa sababu Lema
tangu amekaa huku gerezani nilikuwa sijapata nafasi ya kuja kumtembelea,
kwa vile wakati huu niko katika maeneo haya ya Kaskazini, nikasema nije
kumsalimia, afya yake nzuri na nimemuona hana wasiwasi, naona kabisa
amekaa vizuri, ameelewa hiyo hali na amepokea, hana uso wa kusononeka na
hilo limenipa moyo.
“Nimemwachia
ujumbe ‘just be strong’ (awe jasiri), haya yote yatapita muda wake
ukifika, suala lake liko mahakamani sio la kisiasa, hata kama
lililomleta huku linahusiana na siasa, suala la dhamana tunatarajia
litafika mwisho wake, lakini nimemwambia hata kama dhamana ikikosekana,
bado kesi ya msingi itafika mwisho wake, asiwe na wasiwasi wala hamaki,
awe jasiri asikate tamaa,” alisema.
Desemba
11, mwaka jana, Katibu wa Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa
Ponda, alimtembelea Lema katika gereza hilo na alimtia moyo aendelee na
mapambano na kumtaka asikate tamaa ya kupigania haki za Watanzania.
Lema
alikamatwa Novemba 2, mwaka jana akiwa nje ya Viwanja vya Bunge mjini
Dodoma na kufikishwa mahakamani Novemba 11, mwaka jana akikabiliwa na
kesi za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli na hadi wakati huo
bado anashikikiwa mahabusu katika gereza hilo.
Januari
4, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Arusha inatarajia kutoa uamuzi wa
rufaa namba 135 ya mawakili wa Serikali waliyokata kupinga uamuzi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliompa Lema dhamana, hata hivyo uamuzi
huo haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya nia ya kukata rufaa waliyoitoa
mawakili hao wa Serikali.
Post a Comment