BAO NNE ZA YANGA ZILITENGENEZWA NDANI YA YANGA NA YANGA WENYEWE

Na Saleh Ally
YANGA
wamepoteza mechi yao dhidi ya Azam FC kwa mabao 4-0. Hakuna shabiki wa
Yanga aliye na furaha hata kidogo na wengi wameanza kulaumu mambo mengi
sana, hakuna anayejaribu kutafakari.
Yanga
wanaamini wao wana kikosi cha kushinda kila mechi, kupoteza kwao ni
sare. Hili ni jambo la hovyo kabisa kuliamini kwa yeyote yule.
Niliamini
Azam FC inaweza kuifunga Yanga, nilijua inaweza kuwa sare na Yanga pia
inaweza kushinda. Sikutarajia Yanga inaweza kupoteza mechi hiyo kwa
idadi hiyo kubwa ya mabao, lakini hakuna ajabu ndiyo soka.
Wakati
mechi hiyo ikiendelea, nilikuwa nikijiuliza maswali mengi na hata baada
ya mechi nilijaribu kuzirudia video kadhaa zilizorekodiwa zikiwemo zile
za mabao manne, nikagundua vitu nilivyoona ni vigeni kabisa kwa
wachezaji wa Yanga na kuanza kuamini bao hizo nne zilitengenezwa ndani
ya Yanga huku ikiwezekana hata wao Yanga hawakuwa wakijua.
Muonekano
wa uchezaji au movement appearance. Si ya kawaida, wachezaji
walionekana ni wavivu, hawana kasi na walicheza kama ambao hawakuwa
tayari.
Ukiangalia
takwimu za mapumziko na takwimu za baada ya dakika 90, Yanga ndiyo
ilikuwa chini na inakuwa mechi ya kwanza ndani ya msimu wa 2016-17 iwe
ya Ligi Kuu Bara, kirafiki au Mapinduzi, Yanga kumaliza ikiwa chini
kitakwimu na timu yoyote iliyocheza nayo, kwani hata ilipofungwa na
Stand United na Mbeya City, bado ilikuwa bora kwa maana ya umiliki wa
mpira, mashuti mengi langoni hata iliyokosa na mashambulizi mengi.
Kutomfurahia kocha:
Wakati
nilipoona tofauti hiyo, niliona wazi kuna shida suala la wachezaji
kutomfurahia kocha na mazoezi yake magumu kunaweza kukawa kumechangia
kwa kiasi kikubwa.
Yanga
inaweza ikawa imefungwa uwanjani lakini sababu zikawa zinaanzia mbali
nje ya uwanja. Kwa kuwa hivi karibuni wachezaji waliwahi kulalamika kuwa
wanafanyishwa mazoezi magumu lakini wakaitumia nafasi hiyo kulalamika
kwamba mshahara umecheleweshwa.
Nilianza kufikiria kabla ya mechi ya Azam FC, wachezaji walifanyishwa mazoezi makali jambo ambalo liliwaudhi kwa mara nyingine.
Lakini
pia, kama walifanya mazoezi makali siku moja kabla au siku ya mechi ni
kosa kubwa. Miili yao isingeweza kunyumbulika na mfano mzuri angalia bao
la kwanza, kipa Deogratius Munishi anapangua shuti la Joseph Mahundi,
linarudi ndani na John Bocco anafunga mbele ya mabeki watatu ambao
wanaonekana wamezubaa.
Angalia
bao la pili, Vicent Andrew ambaye ni bora kwa vichwa lakini anashindwa
kuruka vizuri na kumpa Mghana, Yahaya Mohamed nafasi ya kufunga kwa
urahisi sana.
Bao
la tatu, Mahundi anamuacha Dante kwa kumdanganya na mwili. Hata kabla
hajapiga, muangalie Dante anavyokimbia kama mtu aliyebeba dunia
mgongoni.
Bao
la nne, wakati inapigwa krosi, jiulize Kelvin Yondani na Dante walikuwa
wapi, lakini Geofrey Mwashiuya naye anaukosa mpira ikionyesha miili yao
imekuwa migumu sababu ya fatiki kama hayo mazoezi yalikuwepo.
Angalia
vizuri tena hiyo mechi, utagundua unyumbulikaji wa wachezaji wa Yanga,
kasi yao pia haikuwa sawa ukilinganisha na michezo iliyopita.
Wengi
walikuwa wakianguka, hawakuwa na uwezo wa kupiga pasi nyingi na hata
ile sifa ya kupokonya mpira haikuwepo tena maana Azam FC wakati mwingine
walipiga hadi pasi 18 na kufika langoni halafu wakashambulia.
Kipindi
cha kwanza kinaisha Yanga haijapiga hata shuti moja langoni! Hakuna
pasi hata moja bora ya Haruna Niyonzima au Thabani Kamusoko!
Kugomea mshahara:
Suala
la wachezaji kugoma kwa kuwa walicheleweshewa mishahara, kiasi fulani
linaonekana bado limewaathiri wachezaji wa Yanga. Maana mashabiki
walikasirishwa nalo na kuwasakama wakiwakosoa, wao waliona mashabiki
hawapo nao.
Wamejituma katika mechi kadhaa, lakini inawezekana bado ni kitu kinachowaumiza maana kilikuwa na ukweli.
Mfumo
wa Yanga upo hivi; mshahara wa Januari, wachezaji wanalipwa Januari
Mosi, hivyo wao wanakuwa na deni la mwezi mzima. Hivyo kweli waliona
walikuwa na kosa na wameshindwa kulisahau.
Makocha wawili:
Suala
la Kocha Hans van der Pluijm kuondolewa kwenye benchi, kachukua George
Lwandamina na bado ndani yake kuna Juma Mwambusi aliyekuwa msaidizi wa
Pluijm, hili ni kosa kama nilivyoeleza awali.
Utawala
wa Lwandamina si asilimia mia, bado wachezaji wakichukizwa wana sehemu
ya zamani kufikiria ilikuwa sahihi kwa kuwa ipo karibu na wanaona
wanaweza kuungwa mkono.
Hili
linaweza kuonekana ni la kawaida sana, lakini litaendelea kuipa Yanga
wakati mgumu kila kunapotokea kosa dogo ambalo lingeweza kuonekana ni
dogo kama utawala wa kocha wa sasa ungekuwa unajitegemea kwa asilimia
mia.
Post a Comment