Yaliyojili Kwenye Kesi ya Lema na Mkewe Kuhusu Kumtukana RC Gambo
Kesi ya kumtukana Mkuu wa Mkoa
wa Arusha Mrisho Gambo, inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini,
Godbless lema na mke wake Neema Lema (33), imeshindwa kusikilizwa
maelezo ya awali.
Hatua hiyo ni baada ya Mbunge huyo kukwama kuletwa Mahakamani toka Mahabusu kwa sababu zisizojulikana.
Kukosekana kwa Mbunge huyo kuonekana
Mahakamani, kulimlazimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Arusha Agustino Rwezile kutoa amri ya kutolewa hati ya kumtoa Mahabusu
mshitakiwa huyo na kumleta mahakamani hapo ili kesi hiyo isikilizwe
maelezo ya awali.
Hata hivyo tangu amri hiyo itolewe saa
nne asubuhi hadi saa saba mchana mshitakiwa hakuweza kuletwa mahakamani
hapo, licha ya mke wake kuwepo mahakamani hapo.
Rwezile alimtaka wakili wa serikali kueleza sababu za kushindwa kumleta Lema Mahakamani wakati Mahakama imetoa amri.
Wakili wa serikali Fotunatus Mhalila
alisema mshitakiwa ameshindwa kuletwa Mahakamani kutokana na sababu
zisizozuilika , ila kwa sababu upelelezi umekamilika aliomba Mahakama
ipange tarehe ya usikilizaji wa hoja za awali.
Majibu hayo yalipingwa vikali na
Wakili wa utetezi, John Mallya ambaye alitaka kufahamu sababu za
kutomleta Lema anazodai hazikuweza kuzuilika ni zipi na kwa nini
zisitajwe mahakamani.
“Mheshimia hakimu hizo sababu zisizoweza kuzuilika ni zipi,
Wakili wa seriali atueleze, tujue kama siyo amedharau mahakama licha ya
kutakiwa kumleta mshitakiwa,” alisema.
Baada ya hoja hizo kutolewa Hakimu
Rwezile aliendelea kusisitiza hati ya kumtoa Mahabusu itolewe ili aletwe
Mahakamani leo katika kesi hiyo, ambayo itasikilizwa hoja za awali.
Awali katika kesi hiyo Godbless Lema
na mke wake Neema, alisomewa mahitaka kuwa kati ya Agosti 20 Mwaka huu
ndani ya Arusha,walimtumia ujumbe wa simu ya kiganjani Mkuu huyo wenye
lugha ya matusi , huku wakijua ni kosa kisheria.
Ilidaiwa kuwa ujumbe huo ulitumwa kutoka 076415**47 namba 075655**18 kwenda namba 0766-75**75 ukidai, “Karibu, tutakuthibiti kama Uarabuni wanavyothibiti mashoga.” Washitakiwa walikana shitaka hilo na walipatiwa dhamana.

Post a Comment