Rais Magufuli Apokea Hati Za Utambulisho Kutoka Kwa Mabalozi Wa Nchi Mbalimbali Ikulu Jijini Dar
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
23 Agosti, 2016 amepokea hati za utambulisho kutoka Mabalozi wanne
wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi
hao ni Mhe. Roberto Mengoni - Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Kim
Yong Su - Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea hapa
nchini, Mhe. Mohamed Hassan Abdi - Balozi wa Jamhuri ya Somalia hapa
nchini na Mhe. Paul Sherlock - Balozi wa Ireland hapa nchini.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti baada ya kupokea hati za utambulizo za Mabalozi hao
Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha
nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali yake itawapa
ushirikiano wa kutosha ili kuendeleza na kuuimarisha zaidi uhusiano
ulipo kati ya nchi hizo na Tanzania.
Dkt.
Magufuli amewaambia Mabalozi hao kuwa katika kipindi cha kuanzia Mwaka
2016/2017 hadi 2020/2012 Tanzania imedhamiria kutekeleza mpango wa
ujenzi wa viwanda, hivyo amezialika nchi zao na sekta binafsi katika
nchi hizo kuungana na Tanzania katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda
na biashara.
"Naomba
kukuhakikishia kuwa Wafanyabiashara watakaokuja kuwekeza ama kufanya
biashara, mitaji yao itakuwa salama na Serikali yangu itatoa ushirikiano
wa kutosha kuhakikisha uwekezaji huo unafanikiwa na unanufaisha pande
zote mbili" Amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa
Ireland Mhe. Paul Sherlock.
Aidha,
Rais Magufuli amewashukuru Marais wa nchi zote nne ambazo Mabalozi wake
wamewasilisha hati za utambulisho kwake hii leo na amewahakikishia kuwa
uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo utadumishwa
na kuimarishwa zaidi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
23 Agosti, 2016
Post a Comment