Ndalichako aokoa bil. 2.6/- chapchap
·
*** Aeleza
alivyoshtukia marehemu waliokuwa wamepewa mikopo ya mamilioni.
TAMKO la
kuanza ukaguzi wa wanafunzi hewa wanaopata mikopo ya elimu ya juu lililotolewa
na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,
mwezi uliopita, liliwezesha kurudishwa kwa Sh. bilioni 2.6 kimyakimya na vyuo
mbalimbali nchini, imefahamika.
waziri wa
elimu profesa joyce ndalichako.
Kiasi hicho cha fedha kiligundulika kulipwa wanafunzi
hewa katika vyuo 29 kati ya 31 vilivyokaguliwa, alisema.
Akizungumza na Nipashe baada ya mkutano huo, Prof.
Ndalichako alisema katika vyuo vilivyorudisha fedha hizo kabla ya ukaguzi, Chuo
Kikuu cha Dodoma (Udom), kiliongoza kwa kusalimisha fedha nyingi zaidi - zaidi
ya Sh. milioni 400.
Licha ya kurudisha fedha hizo, wakati wa ukaguzi
ilibainika chuo hicho kina wanafunzi hewa 364 ambao kwa mwaka wa fedha
uliopita, walilipwa Sh. milioni 460.96.
Katika orodha ya vyuo 31 vilivyokaguliwa, ni Chuo cha
Mtakatifu Agustino (Saut-Mbeya) na Chuo Kikuu cha Biashara (CBE-Dodoma) tu
ambavyo havikuwa na wanafunzi hewa.
Chuo ambacho kimebainika kutafuna kiasi kikubwa cha fedha
baada ya ukaguzi, alisema Prof. Ndalichako, ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) chenye wanafunzi 13,972 wanaopata mikopo, lakini kati yao, 350 ni hewa
na walilipwa Sh. milioni 703.43.
Akifafanua juu ya fedha zilizorudishwa baada ya kutoka
kwa tangazo la uhakiki wa wanafunzi, Waziri Ndalichako alisema sheria inataka
fedha zikikaa siku 30 bila kuchukuliwa, zirudishwe Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
Juu (HESLB).
“Lakini hilo lilikuwa halifanyiki, ila tulivyosema
tunakagua, fedha hizo zilirudishwa ndani ya muda mfupi,” alisema.
MAREHEMU, WALIOFUKUZWA
Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako alisema fedha za
mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa elimu ya juu zimeshatolewa.
Alisema awali aliagiza utoaji fedha hizo usimame baada ya
kubaini takribani wanafunzi 600 kati ya waliokuwa wanaombewa fedha hizo
walikuwa ama marehemu, waliofukuzwa vyuo na walioacha.
“Mwanzo nilitaka vyuo viniletee orodha ya wanafunzi wao
waliopo chuoni na ambao hawapo kwa sababu mbalimbali, zile taarifa nikazipeleka
Bodi ya Mikopo,” alisema.
“Baadaye (vyuo) vikaleta orodha ya wanaotakiwa wapewe
fedha za mafunzo kwa vitendo, kwa haraka haraka tu mimi nikaona kama (wanafunzi)
600 ambao baadhi yao ni marehemu, wengine wamefukuzwa chuo na wengine wameacha.
“Ndipo nikasema zoezi lile lisimame kwanza na uhakiki
ufanywe na vyuo na wakuu wa vyuo wasaini kabisa.
” Waziri huyo alieleza kuwa ‘madudu’ hayo yamebainika
kwenye ukaguzi uliofanywa na kitengo cha ukaguzi wa ndani cha HESLB kwa
kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Baada ya hatua ya kwanza ya ukaguzi, sasa sehemu ya pili
itaendelea ili kumaliza vyuo vyote 81 vilivyopo nchini,” alisema.
Alisema wanaohusika na mtandao huo watakabidhiwa kwa
vyombo vya dola kwa hatua zaidi, na kwamba baadhi ya maofisa mikopo wa vyuo
mbalimbali na wahasibu wamepewa barua za kujieleza ni kwanini wasichukuliwe
hatua.
Alisema hatua zaidi zitaendelea kwa kuwa ‘ulaji’ huo una
mtandao mpana, kuanzia wanaotengeneza majina ya wanafunzi waliomaliza vyuo,
kujumuisha waliofariki, kuacha ama kufukuzwa na kuyapeleka bodi ya mikopo.
Prof. Ndalichako pia alisema wamebaini benki zina urasimu mkubwa katika kutoa
fursa kwa wakaguzi wa kazi hiyo.
CHANZO; NIPASHE

Post a Comment