TUKUBALI, KOMBE LA SHIRIKISHO KWA YANGA, TANZANIA BADO NI MZIGO MZITO ILA YAPO YA KUJIFUNZA
Na Saleh Ally
TAYARI
mabingwa wa soka Tanzania, Yanga wameshacheza mechi tatu za Kundi A
katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na wamefanikiwa kupata
pointi moja inayowafanya wakae mkiani.
Kundi
hilo lina Timu za TP Mazembe ya DR Congo, MO Bejaia kutoka Algeria na
Medeama kutoka Ghana ambayo iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi
mbili baada ya kupata sare mbili.
Yanga
ambayo ni timu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki kufikia katika
hatua hiyo msimu huu, iko mkiani ikiwa na pointi moja.
Awali
baada ya ratiba ya makundi kutangazwa, asilimia kubwa ya uchambuzi au
makisio yalikuwa hivi; TP Mazembe ilikuwa na uhakika wa kufuzu, hakuna
aliyekataa na wengi waliamini Yanga ingeweza kupambana na MO Bejaia na
Medeama na kufuzu kwenda nusu fainali.
Mechi
tatu ilizocheza Yanga tayari ni kipimo tosha kwa kuwa sasa mambo ya
kubashiri hayapo tena. Kila mmoja ameziona TP Mazembe, MO Bejaia na
Medeama, ni timu za namna gani na inakuwa rahisi sana sasa kupima kwa
kuwa hakuna haja ya kupima urefu wa kina cha mto kwa kutupia kijiti.
Katika
mechi tatu ambazo Yanga imecheza, imefungwa mbili na kutoka sare moja.
Katika mechi hizo imefungwa mabao matatu na kufunga moja tu. Kitakwimu
utaona imefeli sehemu kubwa kabisa.
Katika
mabao mawili iliyofungwa, imefungiwa nyumbani. Ugenini imefungwa moja
na haijafunga hata bao moja ugenini. Nyumbani imeambulia sare na
kufungwa.
Lakini
ukizungumzia uchezaji, utaona Yanga ilikuwa katika kiwango bora kabisa
kwa maana ya kumiliki mpira, kutengeneza nafasi na ikapoteza mambo
mawili muhimu sana ambayo katika ‘level’ waliyonayo yanakuwa muhimu
kuliko inavyokuwa kwenye ligi ya nyumbani.
Yanga
imekuwa dhaifu kwenye ulinzi. Tena inaonekana ina makosa mengi sana
inapokuwa inashambuliwa kwa mipira ya adhabu au ile ‘iliyopoa’ kwa kuwa
mabao mawili iliyofungwa yametokana na mipira hiyo.
Faulo
dhidi ya TP Mazembe ilizaa bao, ingawa bado lina utata hadi sasa,
lakini utaona bao la Medeama lililoanzia na kona, linakwenda kuimaliza
Yanga kwa ulaini kabisa!
Pili
ni umakini ambao unaendana na vitu viwili, moja upande wa walinzi na
pili upande wa washambuliaji. Ukianza na walinzi ni kushindwa kuwa na
umakini wa mwendelezo.
Wakati
wa mipira ya faulo, Yanga walishindwa kuwa makini katika mechi dhidi ya
TP Mazembe. Hata kama kulikuwa na utata wa ‘offside’ bado hata wao
hawakuwa wamekaba ‘ng’adu kwa ng’adu’ na kuwanyima pumzi TP Mazembe
washindwe kabisa kufunga. Hilo ndilo lililotokea katika mechi ya juzi
dhidi ya Medeama.
Yanga,
wameshindwa kuwa makini kwa kuwa inaonyesha wakati mfungaji anafunga,
alikuwa kazungukwa na mabeki watano wa Yanga lakini bado aliweza kufunga
kwa kuwa kati ya mabeki hao wote, hakuna aliyekuwa anamkaba.
Hata
Vincent Bossou aliyekuwa karibu na Bernard Danso Ofori aliyefunga,
hakuwa mwepesi kuufikia mpira kabla ya mshambuliaji huyo. Katika boksi,
formula inasema; “Beki ndiye wa kwanza kuupiga au kuugusa mpira.”
Upande
wa pili wa umakini ni ushambulizi, Yanga walipoteza nafasi zaidi ya
mbili dhidi ya Bejaia wakiwa ugenini. Wakafanya hivyo dhidi ya TP
Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Wamerudia juzi,
nikukumbushe tu nafasi hizi tatu ni za Amissi Tambwe, Obey Chirwa na
Donald Ngoma.
Nafasi
ya Yanga sasa unaweza kusema ni asilimia 10 ikitegemea miujiza ya soka.
Lakini ukitanguliza ukweli, jibu litakuwa Yanga haina nafasi kwa kuwa
inaonekana haijaiva kwa ajili ya michuano hiyo.
Haijaiva
kwa kuwa makosa yanayofanyika yanaonekana kuwa ni ya ‘level’ ya Ligi
Kuu Bara au yanaweza kuwa ni yale ya kiwango cha Kombe la Kagame ambalo
linafanyika Afrika Mashariki na Kati.
Yanga
imeingia anga nyingine ambazo inatakiwa kujifunza na kuthibitisha ule
usemi wa kosa moja, bao moja. Unapokutana na watu walio makini au
wanaojua mpira, hakika hawawezi kufanya utani.
Unaweza
kusema Yanga ina wachezaji wa nje ya Tanzania. Kweli ni wazuri, lakini
unarudi palepale, wanatokea Zimbabwe na Burundi ambao kweli hawana
tofauti kubwa na Tanzania kwa kuwa wanatokea katika ukanda uleule.
Tunajua Ukanda wa Kaskazini na Magharibi mwa Afrika ndiko soka lipo juu.
Lakini
hata Bossou anayetokea Togo, bado nchi yake imeporomoka, naye si beki
wa kiwango cha juu cha kutisha. Uzuri wake ni wa kupanda na kushuka,
mechi hii juu, ile chini. Lakini makosa yake mengi ambayo amekuwa
akiyafanya yanakuwa ni adhabu kubwa, kama hilo la kushindwa kuuwahi
mpira ndani ya 18 akiwa amekaa na fowadi bila ya kumkaba, naye
akamalizia kwa ulaini na kupata bao ‘laini ile mbaya’.
Yanga
imepiga hatua kubwa, hili wote tunapaswa kulitambua na kulikubali.
Tunajua timu za Tanzania kufikia hapo ni zaidi ya miaka nane iliyopita
na Yanga ilijitahidi kufika lakini ikateleza kwa misimu miwili
mfululizo.
Sasa
kama kuna aliyefikiri ikifika basi lazima ivuke tena hadi nne bora,
alikosea. Lazima kulitakiwa umakini na upungufu wa makosa, jambo ambalo
zaidi huletwa na jambo moja kuu, ubora ambao pia hujengwa na ushiriki
sahihi.
Huenda
Yanga ingeweza kufanya vizuri zaidi kama itaingia hatua nyingine.
Lakini safari hii, inaonekana ‘Mzigo mzito wa Mnyamwezi waliopewa,
umekuwa mzito, umewazidi’. Kikubwa ni kuanza upya na uzoefu wa msimu
huu, unaweza ukawa chachu ya kufanya vizuri katika michuano ijayo ya
Ligi ya Mabingwa Afrika.
Takwimu
zinaifunga Yanga, kwamba hatua hii ilikuwa ni ya juu kwake na inaweza
‘kujaribu tena’. Lakini viongozi, makocha na wachezaji wanaweza pia
kuchagua, kujifunza au kukubali kufeli ili wasifeli tena itakapofikia
wakati mwingine.
Katika
soka, hakuna linaloshindikana. Lakini pia ukweli unakuwa una nguvu
kuliko hisia za kudhani au kuona tu inawezekana na kulazimisha kuukimbia
ukweli unaoonyesha kilicho wazi.
Post a Comment