Siri 5 Mauaji Msikitini, Usiku wa kuamkia Mei 19, mwaka huu ni wa kukumbukwa Nyamagana
Gaidi.
Na Waandishi Wetu, UWAZI
MANZA: Usiku wa
kuamkia Mei 19, mwaka huu ni wa kukumbukwa kwa wakazi wa Ibanda Relini
Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana kufuatia watu nane wanaodhaniwa ni
magaidi kuvamia Msikiti wa Rahmani na kuua waumini watatu kwa kuwakata
mapanga, sasa nyuma ya mauaji hayo kuna siri 5, Uwazi limechimba.
Watu hao walijitambulisha kuwa, wao ni
wa kutoka Kundi la Islamic States ‘IS’ huku wakionesha bendera nyeusi
yenye maandishi ya Kiarabu.
CHANZO CHA MAUAJI
Ilidaiwa kuwa, kundi hilo liliingia
msikitini hapo na kuwauliza waumini hao ni kwa nini wanaswali wakati
kuna wenzao wamekamatwa na polisi wa jijini Mwanza kwa madai ya ugaidi.
Hivyo waumini hao hawakupaswa kuswali bali kwenda kupambana na polisi
ili kuwatoa wenzao.
Tayari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
SACP Ahmed Msangi alishakiri kushikiliwa kwa watu hao wanaodhaniwa kuwa
magaidi, lakini akatoa angalizo kwa wote wanaotaka kutumia nguvu
kuwatoa watuhumiwa hao.
NI MKAKATI WA MUDA MREFU
Madai ya kundi moja kutangaza mkakati wa
kuwatoa wenzao walio gerezani yalianza muda mrefu ambapo mwaka jana,
mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kaisi Bin Abdullah (mtazame
ukurasa wa mbele amevaa ninja) alisambaza video akianika mkakati huo
kama njia ya kulipa kisasi kwa wenzao wanaoshikiliwa nchini kote kwa
madai ya uhalifu.
Katika video hiyo, Kaisi alisikika
akisema: Tumeshaungana ili kupambana. Mkoa wa Mtwara zaidi ya wenzetu 17
walikamatwa kwa makosa ya dhuluma, makosa ya kupanga makosa ya ugaidi.
21 wamekamatwa Zanzibar wako katika Gereza la Segerea (Dar). Wenzetu
wengine 18 wamekamatwa Mwanza wako katika Gereza la Kisongo, Arusha.
Ndugu zangu, wenzetu wengine 17 wameuawa Mtwara kwa amri ya …(anamtaja
waziri).
“Subira yetu imefika mwisho na
tulichokuwa tunasubiri Mungu ameshatupa. Tunatoa ahadi kilichopo hivi
sasa tunatoboa jahazi wote tuzame. Tunatoa rai, wenzetu waliopo Gereza
la Kisongo waachiwe huru. Hapa hatumtishi mtu yeyote yule.”
Baada ya kunaswa kwa video hiyo,
waandishi wa Global Publishers walitia timu kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi,
IGP Ernest Mangu na kuzungumza naye kuhusu mtu huyo na kumkabidhi video
ambapo alisema:
“Nawashukuru sana kwa kuleta video hii.
Huu ndiyo ushirikiano unaotakiwa, nawaomba wananchi video za aina hii
wazikatae kwa sababu ni kosa kuwa nazo na watu kadhaa wameshakamatwa kwa
kuwa nazo.
“Sisi kama jeshi la polisi tunajua kuwa
kuna watu wanadhani kufanya uhalifu kama huo kutawasaidia kutimiza
matakwa yao, lakini ukweli ni kwamba polisi wapo imara na nina uhakika
watuhumiwa watakamatwa kwa kushirikiana na raia wema.”
Kwa mujibu wa chanzo chetu, siri ya
kwanza ya mauaji hayo ilitokana na ukatili wa watu hao ambapo walionesha
kuwa, endapo wasingemwaga damu, dhamira yao ya kutaka kuwakomboa wenzao
polisi isingekuwa na nguvu.
“Wakati wanalazimisha waumini kulala,
mmoja alisema; ‘lazima tumwage damu ili watu wajue hatuna utani.
Tusipomwaga damu watatudharau hawa,’” alisema mmoja wa walionusurika
akiwakariri watu hao huku akiomba hifadhi ya jina lake.
Mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye anasema
aliwashuhudia watu wao wakiwa wanaondoka, alimsikia mmoja akisema;
‘serikali si inataka kuambiwa kwa vitendo, hivi ndivyo vitendo sasa.
Hakuna kumwabudu Mungu mpaka haki ipatikane.’ (akimaanisha wenzao
waachiwe).
Mmoja wa waumini wa msikiti huo ambaye
pia hakupenda kuandikwa jina gazetini, alisema mauaji hayo yalifanywa na
watu hao baada ya kuwatumia salamu mapema waumini wasisali lakini
walipogundua watu wanasali wakaona wamepuuzwa.
“Tunasikia walituma ujumbe wa onyo tangu
awali kwamba waumini wasisali washughulikie kuwatoa wenzao. Sasa
walipobaini watu wameingia kuswali wakajikusanya na kuja kufanya mauaji
wakiamini ndiyo dawa pekee ya maneno yao kufuatwa.
Naye kiongozi mmoja wa Bakwata Mkoa wa
Mwanza ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa, kwa
kawaida makundi ya watu wanaotumia mwavuli wa imani ya Kiislam kufanya
mauaji, ni ya wale wanaopenda kuabudiwa kwa kile wanachokisema.
KUCHELEWA KUTII AMRI
Hata hivyo, siri nyingine ya tano ya
watu hao kuuawa inadaiwa kuwa ni kuchelewa kutii amri. Inadaiwa kuwa,
wakati magaidi hao wakiingia na kuamrisha watu kulala, wapo waliochelewa
kutii wakitaka kujua kwanza wanaotoa amri hiyo ni akina nani na wana
lengo gani!
“Karibia wote waliokatwa mapanga sana
walichelewa kutii amri ya kulala. Walitaka kuwaona wale watu ni akina
nani. Kwani lilikuwa tukio la kufumba na kufumbua. Na wao walipoona kuna
ambao ni wagumu kulala, wakaanza kutembeza majambia mpaka kuua,”
alisema muumini mmoja.
WALIBADILI SAUTI
Muumini mwingine wa msikiti huo alisema
kuwa, sauti walizotumia watu hao si za asili kwani alimsikia mmoja wao
ambaye huenda ni kiongozi, aliwasisitizia wenzake kuhakikisha wanabadili
sauti ili wasibainike.
“Zile sauti hazikuwa zao. Naamini wale
watu wanatujua na sisi tunawajua, nilimsikia mmoja akisisitiza kuhusu
sauti. Alikuwa akisema; ‘sauti sauti, angalieni sauti zenu.”
SIRI YA KUFICHA SURA
“Ndiyo maana walificha sura kwa kuvaa
ninja. Mbona majambazi kibao tu wanaingia benki kuiba bila kuficha sura?
Wale sura zao si ngeni kwetu ndiyo maana walificha,” alisema muumini
huyo.
WATOTO WAWILI WAZUA UTATA
Muumini mwingine aliyenusurika katika tukio hilo yeye anasimulia kwa kirefu tangu alipoingia kwenye mlango wa msikiti huo.
“Ilikua saa 2: 35 usiku nilipongia
msikitini na kuwakuta watoto wawili wageni. Mmoja aliketi mbele mwingine
nyuma. Kwa kawaida Waislam kuwa hatuulizani na kuwa na wageni wa
kawaida, kumbe sivyo. Naamini walikuwa kwenye mpango.
“Baada ya muda nikasikia watu wakiingia
na kutuamuru tusigeuke na tulale pale tulipo. Walimuulizia imamu wa
msikiti, alipokosekana wakampata msaidizi, wakampiga shoka kichwani na
kumcharanga sana huku wengine wakiendelea na mauaji, sisi tulifanikiwa
kukimbia,” alisema muumini huyo.
MWINGINE HUYU
“Mimi nilifika msikitini saa 2:40
nikiwa nimechelewa, nikaenda kujipanga mbele. Wakati tunamalizia Rakaa
ya mwisho, tukasikia watu wanaingia wakatuambia hapohapo mlipo laleni
chini, wakasema wanamtaka imam. Mimi nilijua ni polisi kumbe siyo,
wakamchukua Ostadh Feruz wakampiga bapa kwanza, alipopiga kelele
wakamkata panga, lakini kumbe vipaza sauti vya msikitini vilikuwa wazi,
wakavizima.
“Walizima taa na kuanza kumchinja
Ostadhi tukiwa tunaona huku wakisema nyiye badala ya kupigana
mnasalisali, mnasali nini kwanza mmetusaliti.
“Kiongozi wa kundi hilo alikuwa
mwanamke, akaanza kuamrisha kwa kusema; ‘chinja na huyu.’ Alipofika mtu
wa tatu, yule mwanamke akasema; ‘watoto wasichinjwe.’ Baada ya kusema
hivyo mimi nikachoropoka na kuanza kupiga kelele, na wao wakaondoka.”
KISA CHA WALIOKAMATWA
Kutokana na eneo la Ibanda Relini kuwa
nje kidogo ya Jiji la Mwanza, inadaiwa limekuwa likitumiwa kufanya
mafunzo ya kigaidi kwa baadhi ya watu wa eneo hilo ambao walikuwa kwenye
Kikundi cha Al Shabaab hivyo, baada ya jeshi la polisi kupata taarifa
walifanya msako na kuwakamata watu kadhaa ambao ndiyo chanzo cha magaidi
hao kuvamia msikitini na kuwaambia wenzao wasisali.
MKE WA MAREHEMU
Amina Salumu ni mke wa marehemu, Ostadh
Feruz Ismail Elias, alisema siku ya tukio, mume wake aliondoka nyumbani
saa 2:15 kwenda msikitini kuswali lakini baada ya muda mfupi alisikia
kelele za watu huku kukiwa na milipuko msikitini hapo.
“Lakini polisi walipofika eneo la tukio
tayari mume wangu alikuwa ameshafariki dunia. Naiomba Serikali ijitahidi
kuwakamata waliohusika na tukio hili ili sheria ichukue mkondo wake,”
alisema Amina.
JESHI LA POLISI
Kutokana na tukio hilo kuvuta hisia za
wengi ndani na nje ya Jiji la Mwanza, jeshi la polisi mkoani hapa
kupitia kwa Kamanda Msangi, limesema waliouawa katika tukio hilo ni
Feruzi Isamail Eliasi (27) kabila Muha, Imamu wa msikiti huo na mkazi wa
Ibanda Relini, Mbwana Rajab (40) kabila Mbondei na Khamis Mponda (28)
dereva wa kiwanda cha samaki na mkazi wa Mkolani.
Aliyejeruhiwa vibaya ni Ismail Abeid
(13) mwanafunzi wa Shule ya Kiislam ya Jabari iliyoko Nyansaka,
anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Butimba.
Feruzi Isamail Eliasi (27) na Khamis Mponda (28) walizikwa Mwanza na Mbwana Rajab (40), alizikwa Tanga.
CHANZO: GPL
Post a Comment