Kiba Apata Mpenzi Mwingine, Asema: Nikimrudia Jokate nisutwe
Staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’
Stori: Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM: Siku chache baada
ya kusaini mkataba wa kimataifa na Kampuni ya Sony, Staa wa Bongo
Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ amedaiwa kufunguka kuwa, kamwe hawezi
kurudiana na aliyekuwa mpenzi wake na akifanya hivyo asutwe mchana
kweupe.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini ambacho kipo karibu na
msanii huyo kimeeleza kuwa, staa huyo amegundua alipotea njia kwenye
penzi la Jokate hivyo hana sababu ya kurudi nyuma kwani huu ndiyo wakati
wake wa kufanya mambo makubwa.
“Jamaa tangu asaini mkataba mpya na
Sony, hataki kuutia doa. Amesema anataka kutusua kimataifa zaidi hivyo
anaona akirudi kwa Jokate ni kama atakuwa amerudi alikotoka kisanii.
“Unajua amejifunza mambo mengi kipindi
yupo na Jokate, hataki tena kurudi kule kwani kusaini kwake mkataba
mkubwa anataka kuendane na maisha yake binafsi,” kilisema chanzo chetu.
Jokate Kidoti ‘Jojo’
CHANZO CHAZIDI KUTIRIRIKA
Kama hiyo haitoshi, chanzo hicho
kilizidi kutiririka kuwa, mbali na kula mkataba mnono, Kiba tayari
amempata mpenzi mpya ambaye wanaendana kwa kila kitu hivyo anaona ni
wakati mzuri wa kufaidi maisha ya uhusiano sambamba na maisha yake
kimuziki.
“Ni mtoto f’lani mwenye maadili. Kama
unavyojua Kiba ni mtoto wa Kiislamu, safari hii ameona achukue binti
mwenye imani kama yake ili aweze kufika mbali maana japo hana mpango wa
ndoa kwa sasa lakini anataka mtu ambaye ataishi naye kwa muda mrefu,”
kilisema chanzo hicho.
KUFANYA MAMBO MAKUBWA
Chanzo hicho kilizidi kuweka bayana
kuwa, Kiba ameapa kufanya mambo makubwa kwani amepata uongozi mzuri
ambao unajua kuongoza wasanii na kuwaunganisha na televisheni za
kimataifa.
“Kiba kwa sasa ngoma yake inachezwa
kimataifa, juzikati kupitia televisheni ya Sound City Africa ambayo
makao makuu yapo Nigeria, walitoa saa 12 kwa ajili ya Kiba, wakaiita Ali
KibaDay, hapo zilichezwa nyimbo zake tu, ni nafasi kubwa sana ya
kujitangaza, imempa connection nyingi za kimataifa,” kilisema chanzo
hicho.
DIAMOND ATASUBIRI SANA
Chanzo hicho kilizidi kummwagia sifa
Kiba kuwa kutokana na uwezo, uongozi na mkatapa huo mpya, sasa hivi
Diamond atasubiri sana kwani levo zake zitakuwa za mbali.
“Aaah! Diamond atasubiri sana. Kiba
anabebwa na vingi kwa sasa, uongozi mzuri na anajua kuimba kuliko huyo
Diamond. Ataisoma namba kama unavyosikia wimbo wa Aje ndani ya muda
mfupi tu, tayari umekamata,” kilisema chanzo hicho.
MENEJA AFUNGUKA
Baada ya kushibishwa ubuyu huo,
mwanahabari wetu alimvutia waya mmoja wa mameneja wa msanii huyo ambaye
hapendi jina lake lichorwe gazetini kwa kile alichodai si mambo ya
muziki aliyoulizwa, lakini akaweka bayana kuwa kweli Kiba hayupo tayari
kurudiana na Jokate kwani ana mtu wake mpya.
“Hawezi kumrudia, sijui hata amemchukia
nini yule mrembo (Jokate). Jamaa kwa sasa ana kifaa kipya lakini hapendi
kukiweka wazi. Si unajua naye alivyo mtu wa sirisiri,” alisema meneja
huyo.
KIBA ANASEMAJE?
Risasi Jumamosi
lilimtafuta Kiba ili kuweza kumsikia anazungumziaje juu ya mrembo huyo
na kama kweli hana mpango wa kurudi nyuma hadi kufikia hatua ya kutamka
kuwa asutwe kuliko kurudina na mrembo huyo, Kiba alijibu kwa kifupi:
“Haya ni mambo yangu binafsi. Sipendi
sana kuyazungumzia. Kifupi wewe elewa kwa sasa siwezi kurudi nyuma, nipo
kwenye hatua nyingine za kimaendeleo na namshukuru Mungu nakubalika.”
YA AWALI
Miaka miwili iliyopita, Kiba na Jokate
wamekuwa habari kwenye vyombo vya habari wakidaiwa kuwa wapenzi licha ya
kwamba, mara nyingie alikuwa akikanusha huku mwenzake akiwema wazi.
Hata hivyo, maisha yao ya kimapenzi yamekuwa yakitawaliwa na mlolongo wa kumwagana na kurudiana.
Kuna wakati ilidaiwa Jokate alinasa mimba ya Kiba lakini baadaye ikasemekana kuchoropoka.
Maneno mengi yalisemwa kuwa, hakuna
tumaini la mbele katika uhusiano wao kwa vile, Jokate ni Mkristo, Kiba
Muislam huku familia ya mrembo huyo ikitajwa kutokuwa tayari binti yao
kuingia kwenye ndoa na mwanaume wa imani tofauti.
Kumwagana kwa safari hii na Kiba kupata kifaa kingine kunahitimisha ‘kapo’ yao iliyodumu kwa miaka mitatu sasa.
CHANZO; GPL

Post a Comment