Simbachawene Anawana Mikono....Aagiza Uchaguzi wa Meya Jiji la Dar Ufanyike Kabla ya Tarehe 25 Mwezi Huu
Hatimaye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene
amemaliza mzozo wa uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar es Salaam baada ya
kuagiza ufanyike kabla ya Machi 25 na kutaja sifa za wapigakura.
Uamuzi
huo wa kutangaza tarehe na sifa za wapigakura unaonekana kuwa ahueni
kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo
vilifurahia hatua kama hiyo, lakini wadau wa CCM wakafungua kesi
iliyosababisha uchaguzi huo uahirishwe mara tatu.
Simbachawene,
ambaye aliwahi kuagiza uchaguzi huo ufanyike kabla ya Februari 29 lakini
ukakwama mara tatu, aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Arisha kuwa
uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia kifungu cha 13 (1) cha Kanuni za
Kudumu za Jiji.
Alisema watakaopiga kura katika uchaguzi huo ni
madiwani wote wa halmashauri za jiji la Dar es Salaam ambazo ni Ilala,
Temeke na Kinondoni, wabunge wa kuchaguliwa na wabunge wa viti maalumu
ambao mchakato wa kuwapata ulianzia kwenye mamlaka za halmashauri hizo.
Simbachawene
alisema wapigakura wengine watakuwa ni wabunge wa kuteuliwa na Rais,
ambao ni Dk Philip Mpango, Balozi Agustine Mahiga, Dk Ackson Tulia,
Profesa Joyce Ndalichako, Dk Abdallah Possi, Profesa Makame Mbarawa
ambao ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.
“Tunaomba vyama
kuheshimu misingi ya demokrasia kwa kukubali matokeo ili kutosimamisha
maendeleo ya jiji la Dar es Salaam,” alisema.
Taarifa ya tarehe
ya uchaguzi huo na sifa za wapigakura imepokewa vizuri na viongozi wa
Ukawa, ambao walitaka tamko hilo litolewe ndani ya siku saba na Serikali
ibainishe sifa za wajumbe watakaoingia kupiga kura.
Kwa uamuzi huo wa
Simbachawene, Ukawa, ambayo ina madiwani na wabunge kutoka vyama vya CUF
na Chadema, itaingia kwenye uchaguzi ikiwa na wapigakura 87, huku CCM
ikiwa na 76.
Akizungumza baada ya kupata taarifa hizo jana,
Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo alisema
Simbachawene amesikia agizo lao walilotaka kupewa mapema tarehe ya
uchaguzi huo.
“Kimsingi zile siku saba zilikuwa zinaisha leo
(jana). Kwa hiyo Waziri Simbachawene ametumia busara. Hivyo ndivyo
kiongozi anatakiwa kuwa,” alisema Kilewo.
Kilewo aliitaka CCM
kujianda kisaikolojia, akisema wasitarajie ushindi kwa kuwa licha ya
kuongezewa wajumbe, Ukawa bado wana hazina kubwa ya wajumbe.
“Tumeshapata
taarifa kuwa wamepanga kuwakamata baadhi ya wajumbe wetu ili idadi
ipungue. Nawaambia wasisithubutu kufanya mchezo huu bali wakubali yaishe
na kuachia jiji,” alisema Kilewo.
Kwa takriban miezi miwili,
uchaguzi katika jiji la Dar es Salaam umesimama kutokana na mvutano
baina ya CCM na Ukawa, hasa wa uhalali wa wajumbe halali wa kupiga kura.
Kutokana na mgogoro huo, wabunge watatu wa Chadema, Halima Mdee
wa Kawe, Mwita Waitara (Ukonga) na Said Kubenea (Ubungo) wameshtakiwa
kwa tuhuma za kusababisha vurugu baada ya kusitishwa uchaguzi huo hivi
karibuni kwa kutumia zuio hilo ambalo limebainika kuwa batili.
Akizungumzia
zuio hilo, Simbachawene alisema lilikuwa ni batili kwa kuwa lilitolewa
wakati tayari kesi ya msingi ilikuwa imetolewa uamuzi tangu Februari 23.
Post a Comment