ad

ad

Man Utd, Tottenham wapigwa Europa Ligi


Tottenham Hotspurs wakicheza ugenini katika dimba Signal Iduna Park huko nchi Ujeruman wamekubali kichapo cha mabao 3-0 .


LIVERPOOL, England
MANCHESTER United wameanguka katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Europa baada ya kuchapwa na Liverpool mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Anfield, usiku wa kuamkia leo.

Man United ambao walikuwa na rekodi nzuri ya kushinda dhidi ya Liverpool katika mechi za hivi karibuni, bado wana nafasi ya kufuzu kwa hatua inayofuata endapo watapata ushindi wa zaidi ya mabao 3-0 kwenye mchezo wa pili wiki ijayo.

Hata hivyo, Liverpool walionekana kuwa bora zaidi kipindi cha kwanza baada ya kumaliza wakiwa mbele kwa bao lililowekwa kimiani na Daniel Sturridge, ambaye alifunga kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 20 baada ya kiungo Memphis Depay, kumvuta Nathaniel Clyne, kwenye eneo la hatari.

Hata hivyo, utata ulizuka huku United wakiamini kuwa madhambi hayo yalifanyika nje ya eneo la hatari.

Liverpool walionyesha mchezo mzuri kipindi cha kwanza baada ya kufanikiwa kupiga mashuti sita langoni mwa United, ambapo manne yalilenga lango na moja kutoka nje.

Hata hivyo, United ambao kipindi cha pili walimtoa Marcus Rashford na kumuingiza Michael Carrick walionyesha uhai huku wakipambana kwa nguvu zote kupata bao la kusawazisha lakini ukuta wa Liverpool ulikuwa mgumu.

Dakika ya 73, Liverpool waliamka tena na kujipatia bao la pili lililowekwa kimiani na Firmino baada ya mabeki wa United kufanya uzembe.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana kwenye michuano ya Europa tangu kuanzishwa kwake na ni mchezo wa kihistoria kwa timu hizo.

Matokeo mengine:
Tottenham Hotspur wakiwa ugenini nchini Ujerumani walijikuta wakilala kwa mabao 3-0 dhidi ya Borrusia Dortmund.

Dortmund ambao waliwazidi Spurs muda mwingi wa mchezo walifunga kupitia kwa Pierre-Emerick Aubameyang na Marco Reus aliyefunga mawili.

Mechi nyingine za michuano hiyo zilizopigwa jana ni: FC Basel 0-0 Sevilla, Fenerbahce 1-0 Sporting Braga, Shakhtar Donetsk 3-1 Anderlecht.

No comments

Powered by Blogger.