Rais Magufuli Apiga Marufuku Uingizwaji wa Sukari toka Nje ya nchi
RAIS John Magufuli amesema amedhamiria kwa dhati kufufua viwanda vya ndani na kama mfano amepiga marufuku kwa kiongozi yeyote wa serikali, kutoa kibali cha kuagiza sukari kutoka nje ya nchi zaidi yake.
Aidha,
amesisitiza kwamba ataendelea kutumbua majipu ya viongozi mafisadi na
wala rushwa, kwa kuwa yeye na viongozi wenzake sio wakatili, ila ni
kutokana na nchi kuoza.
Amesema
yupo radhi kuchukiwa na Watanzania wachache, ambao wamekuwa wakihusika
na vitendo vya ufisadi, vinavyoathiri maisha ya Watanzania wengi ili
kuiwezesha nchi kusonga mbele kuelekea kwenye uchumi wa kati kwa kasi.
Rais
Magufuli alisema hayo Ikulu Dar es Salaam jana, alipokutana na makundi
mbalimbali ya wadau walioshiriki kwenye kampeni zake kuelekea kwenye
Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana na kuibuka na ushindi
uliomuwezesha kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Akizungumzia
ufufuaji wa viwanda ikiwa ni moja ya eneo alilolitilia msisitizo mkubwa
wakati wa kampeni, Rais Magufuli alisema nia yake ya kufufua viwanda
ipo pale pale na kusema tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa.
Akitoa
mfano, Rais alisema wakati yapo maeneo ambayo wakulima
wanajishughulisha na kilimo cha miwa na zao hilo kuwa tegemeo lao katika
kuinua uchumi wao, wapo wafanyabiashara wanaojali maslahi yao binafsi
ambao wamekuwa wakiagiza sukari kutoka nje hatua inayosababisha kufa kwa
viwanda vya sukari vya ndani.
“Mtu anaagiza sukari kutoka nje, tena wakati mwingine ni sukari ambayo muda wake wa kuisha matumizi umekaribia kumalizika.
"Huyu
mfanyabiashara anaingiza sukari hiyo na kuifungasha upya ili
isijulikane kuwa inakaribia kuharibika na kuwauzia wananchi masikini.
“Kitendo
hiki kinasababisha sukari inayozalishwa na viwanda vya ndani kukosa
soko, wakulima wanakosa soko la miwa yao, na serikali nayo inakosa
mapato ya ushuru.
"Kwa
vile bahati nzuri Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Makamu wa Rais
(Samia Suluhu Hassan) mpo hapa, nasema kuanzia sasa asiwepo mtu wa kutoa
kibali cha mtu kuagiza sukari kutoka nje hadi ruhusa hiyo itoke
kwangu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema
mkakati kama huo hautaishia kwenye sukari pekee, bali ni mkakati ambao
utahusu maeneo yote ya uzalishaji ili wananchi wa kipato cha chini
waneemeke na nchi yao.
“Nimekuwa
nasema nchi yetu si masikini. Hii nchi ni tajiri sana, lakini wapo watu
wamekuwa wanajinufaisha wao. Wapo tayari wapokee virushwa ili waneemeke
wao huku Watanzania wengi wakiumia na kuteseka.
“Ndio maana nasisitiza kwamba nitaendelea kutumbua majipu ya viongozi mafisadi na wala rushwa.
"Tunapotumbua
majipu si kwamba sisi ni wakatili hapana, ila ni kutokana na nchi yetu
kuoza. Kila unapotupia jicho pameoza, hadi wakati mwingine unashindwa
kuamua uanze na jipu lipi na lipi ulitumbue kesho, yapo majipu mengine
hayasikii dawa.
“Hawa
watu wanaolalamika sana sasa ni wachache ambao walikuwa wananufaika na
ufisadi na rushwa. Ni bora ukachukiwa na watu 1,000 ili upendwe na watu
milioni 50.Kama nitaboresha maisha ya Watanzania milioni 50, hata kwa
Mungu tutapokelewa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema
serikali yake itaendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha kuwa
Tanzania inakuwa nchi ya neema na ya uchumi wa kati na kuwa umoja,
mshikamano na uzalendo usioambatana na tofauti za kidini, ukabila na
itikadi za kisiasa ni nyenzo kubwa katika kufikia mafanikio hayo.
==>Tazama Video hii kumsikiliza Rais akitoa amri ya kupiga marufu uagizaji Sukari

Post a Comment