ad

ad

Cheka ashinda kimaajabu, Mzungu awatusi Wabongo

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka, amefanikiwa kuibuka mshindi wa Ubingwa wa Mabara (WBF Intercontinetal) kwa kumpiga Geard Ajetovic kwa pointi, baada ya majaji wote kumpa pointi nyingi.
 

Licha ya Cheka kushinda, lakini Mserbia Ajetovic anayeishi nchini Uingereza, alipinga vikali ushindi huo kutokana na madai ya kucheza vizuri zaidi ya mpinzani wake katika pambano hilo lililokuwa la raundi 12 lililofanyika kwenye Viwanja vya Leaders Club, Dar.
 

Awali Cheka ambaye kwa sasa ndiye bingwa mpya wa mabara baada ya kuupoteza nchini Urusi mwaka 2014, alionekana kucheza kwa tahadhari kubwa na woga kutokana na kasi ya mpinzani wake, kitendo kilichosababisha aangushwe chini baada ya kupata ngumi kali katika raundi ya kwanza kabla ya kukaa sawa na kuendelea na pambano.
 

Championi ambalo lilikuwepo viwanjani hapo likishuhudia pambano hilo, lilimuona Cheka akirusha ngumi nyingi za kudokoa ambazo hazikuwa na nguvu ya kumchosha Mzungu huyo, hali iliyosababisha mashabiki wake waingiwe na hofu kubwa ya kwamba ataweza kushindwa kutokana na kasi ya Ajetovic ambaye alikuwa akipiga ngumi nzito kila mara.
 

Katika raundi ya tisa, Cheka alichanika usoni na kuanza kuvuja damu, lakini aliweza kuendelea na pambano hilo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa daktari.
 

Baada ya kutangazwa mshindi, kuliibuka tafrani kubwa kwa upande wa Ajetovic ambao ulipinga matokeo hayo kwa madai ya Cheka kupigwa ngumi nyingi za pointi huku Mserbia huyo akitoa lugha chafu za matusi kwa Wabongo.
 

“Huu ni ujinga, watapangaje ushindi wakati nilimzidi katika raundi zote, sikutendewa haki… (tusi), wamenichafulia rekodi yangu kwa ujinga wao, ni wapuuzi kwa kweli kazi yote niliyoifanya kumbe ni bure, inatia uchungu (tusi),” alisikika bondia huyo akifoka huku akigoma kuongea na waandishi wa habari.
 

Kwa upande wa Cheka, alisema: “Namshukuru Mungu na Watanzania kwa sapoti waliyonipa kwani imechangia kwa asilimia kubwa kuweza kutwaa ubingwa huu, maana ulikuwa ni wetu ndani ya chini yetu.”
 

Hata hivyo, Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, Emmanuel Mlundwa, ametolewa ufafanuzi ushindi huo kwa kusema: “Majaji walikuwa sahihi kwa sababu kila jaji anakaa peke yake, jaji wa kwanza alitoa alama 115-114, wa pili akatoa 115-114 na wa tatu alitoa 116-114.”

No comments

Powered by Blogger.