ad

ad

KWELI NAPE, HAKUNA NIDHAMU KABISA, ILA ITAKUA POA UKIANZA NA WATU WA HAPO WIZARANI

 NILIMSIKILIZA Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akizungumzia kuhusiana na suala la nidhamu katika michezo kwamba ni sehemu ya chanzo au tatizo kubwa.
Nape aliyasema hayo dakika chache baada ya kumaliza shughuli ya kuapishwa iliyosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, John Pombe Magufuli.

Nape alieleza sehemu ya anavyoona kuwa kweli katika michezo hakuna nidhamu. Jambo ambalo nimekuwa nikilitia mkazo tena kwa kiwango cha juu.

Mara kadhaa, nimesema kuhusiana na nidhamu na nikawagusa watu kwa majina au taasisi fulani na mfano wangu mzuri umekuwa ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na upande wa vyama vya riadha na mashirikisho mengine.

 Nilisikia faraja kuona Nape angalau ameweza kuzungumza jambo kubwa ambalo ni tatizo kubwa pia katika michezo. (Huenda mara kadhaa amekuwa akipitia makala zangu na hilo ni moja ya vilio vyangu vikubwa).

 Niliona baadhi ya watu mitandaoni, wakipinga au kushangazwa kwamba nidhamu si jambo kubwa kuporomoka kwa michezo huku wakiona kama Nape alikosea kabisa. Huenda ni ushabiki wao wa kisiasa au vinginevyo, au hawaijui michezo ya Tanzania inavyoendeshwa!

 Kwanza naungana nao, kweli michezo ina matatizo lundo, lakini nidhamu na ubinafsi linaweza likawa jambo linalohitaji dawa kali au yenye nguvu ya juu kulimaliza.
 Nidhamu ipo kwenye kila kitu, ukifeli basi ujue umeanguka bila ya kujali una uwezo mkubwa kifedha, akili nyingi au kipaji cha juu kabisa. Hayo yote lazima yaongozwe na nidhamu.

 Katika michezo hakuna nidhamu ya matumizi ya fedha. Watu wanatumia fedha kama za baba zao au wazazi wao, hawataki kuhojiwa au kuelezwa ukweli, wanakuwa wakali na vitisho juu.

 Kama hiyo haitoshi, watu hawajali maendeleo ya michezo ndiyo maana katika nafasi nyeti zinahusisha maendeleo ya michezo wanaweka washikaji zao bila ya kujali uwezo walionao. Wanafanya hivyo kulinda maslahi yao binafsi na vimada wao na si kwa ajili ya mchezo husika au michezo kwa ujumla.

 Kuna mashirikisho yamejaa uozo, wako wanaofanya kazi kwenye vyama au mashirikisho kwa kuwa rais au mwenyekiti anamchukua dada yake au mama yake mdogo. Ajira za michezo hazifuati tena ushindani na badala yake ni urafiki na kubeba kwa ajili ya kuwafurahisha watu fulani au ahsante kwa kuonyesha ukaribu na ushikaji wa kufa na kupona.

Lazima tukubali hata migogoro mfululizo ni kutokuwepo kwa nidhamu na lazima watu wabadilike. Isitokee watu wakataka kuikanyaga kauli ya Nape kuhusu nidhamu na kuchukulia kama kitu kidogo ili kutaka kufanya mambo yaonekane kwamba ni poa sana.

Katika michezo nidhamu hata kwa wachezaji pia ni tatizo na hili nimelizungumza sana. Wao ndiyo wanaotegemewa lakini hawaonyeshi nidhamu hata kidogo, hili si jambo sahihi na wachezaji wanapaswa kujitambua na kubadilika.

Lakini wakati Nape amezungumzia nidhamu, mimi nianze kumkumbusha kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya ambayo inatakiwa kuanzia katika wizara yake.

 Ndani ya wizara hiyo ambayo safari hii imeongezewa kitengo cha sanaa pekee. Kumekuwa na watu magwiji ambao wanaendesha mambo kwa mazoea na ule mfumo wa aliye serikani hashikiki wala hakuna wa kumgusa.

 Mfumo mbovu wa aliye serikali kuonekana ni bosi wa jamii badala ya mtumishi wa jamii. Wako watu hapo wizarani hawana nidhamu ya kazi na wamefanya mambo mengi katika michezo kukwama kwa kuwa tu wao wanaona kila kitu rahisi na kamwe hawajawahi kuwa na mipango madhubuti katika uendelezaji.

Nitakupa mfano, rasimu ya michezo ambayo ndiyo ya michezo ilitengenezwa katika miaka ya 1960, lakini hadi leo ndiyo inayotumika. Hakuna anayejali kufanya mabadiliko ili iendane na muda na badala yake, watu wanaendelea kufurahia kuwa wageni rasmi wakati wa ukabidhishaji wa bendera kitu ambacho ni hovyo na hakipaswi kuendelea kufumbiwa macho!

Karibu tena Waziri Nape, ila naendelea kukumbusha wasio na nidhamu ni wengi sana, usiwalazie damu.
Powered by Blogger.