Kila la kheri Dk. John Magufuli, kwaheri JK
Rais wa awamu ya tano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, leo anaapishwa rasmi kushika wadhifa huo.
Hatua hiyo inafuatia ushindi wake kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Tunapenda kumpongeza Dk. Magufuli kwa ushindi huo na pia anaingia
kwenye vitabu vya historia kama miongoni mwa waliowahi kushika wadhifa
huo wa juu nchini Tanzania.
Tanzania ni miongoni mwa nchi na hasa kwenye Bara la Afrika ambazo
zimejenga utamaduni wa viongozi wake wa juu kuachiana madaraka kwa
amani.
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, ndiye aliyeasisi
utaratibu huo alipong’atuka mwaka 1985 na kumwachia kijiti Ali Hassan
Mwinyi.
Rais Mwinyi alipomaliza muda wake mwaka 1995, nafasi yake ilichukuliwa na Benjamin Mkapa, ambaye aling’atuka mwaka 2005.
Rais Kikwete alichaguliwa kushika wadhifa wake katika mwaka huo na
leo anaachia madaraka kwa Dk. Magufuli kwa amani bila kumwaga damu.
Nchi nyingi hasa katika Bara la Afrika, zina matatizo ya viongozi
kung’ang’ania madaraka na hata kuwapo mapinduzi ya kijeshi, hali ambayo
husababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na baadhi yao kuwa na
uchu wa madaraka.
Kitendo cha Tanzania kujenga utamaduni wa kupokezana vijiti kwa viongozi wenzake, ni jambo la kupongezwa.
Pia tunampongeza Rais Kikwete kwa kuongoza taifa hili kwa miaka 10 na kung’atuka kwa njia ya kidemokrasia.
Rais Kikwete amefanya mengi tu mazuri, lakini pia utawala wake
ulikabiliwa na changamoto nyingi ambazo sasa zinapaswa kufanyiwa kazi na
utawala mpya wa Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli anapokea nchi huku wananchi wake wakiwa na kiu ya
mabadiliko, jambo ambalo lilidhihirika wakati wa mikutano ya kampeni.
Pia bahati nzuri wagombea wa vyama mbalimbali walipigania uongozi
kwa kuahidi jambo hilo, ambalo linapaswa kufanyiwa kazi katika uongozi
mpya chini ya Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli ana deni la kulipa Watanzania kwa imani waliyoonyesha kwake na kumpa dhamana ya kuongoza taifa hili.
Baada ya zaidi ya miaka 50 ya Uhuru, Watanzania wanataka kuona vita
dhidi ya maadui watatu; umaskini, ujinga na maradhi vikimalizika.
Bila shaka baada ya kuzungukia sehemu mbalimbali za Tanzania, Dk.
Magufuli atakuwa anaelewa vizuri changamoto anayokabiliwa nayo ya
kupambana na maadui hao.
Pia kero nyingine ambayo inawaumiza Watanzania, ni ya rushwa na ufisadi.
Vita dhidi ya rushwa na ufisadi, isiishie majukwaani tu, bali
vyombo vinavyotakiwa kukabiliana na matatizo hayo, lazima vipewe meno.
Tunamshauri Dk. Magufuli atekeleze ahadi yake ya kuunda mahakama maalum ya kushughulikia kesi za rushwa na ufisadi.
Hata hivyo, ni mategemeo yetu kuwa moja ya majukumu ya mwanzo ya
Dk. Magufuli itakuwa kuhakikisha mvutano wa sasa kuhusiana na Uchaguzi
Mkuu wa Zanzibar inamalizika.
Siyo jambo zuri kuona upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ikiwa na mvutano wa kisiasa wakati upande wa pili ukiwa
umetulia.
Tunaelewa kuwa Dk. Magufuli anapokea mzigo mzito kutoka kwa
mtangulizi wake, hata hivyo, tunaamini atatimiza imani na matarajio ya
wananchi wake.
Aidh, tunamtakia kila la kheri Rais Kikwete mapumziko mema na
maisha mazuri ya kustaafu baada ya utumishi uliotukuka wa miaka 10.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment