Lowassa aiteka rasmi Mwanza

Maduka yafungwa, wananchi wakesha wakimsubiri, baadhi wazimia, umati wafunga barabara ya uwanja wa ndege kwa saa kadhaa, mabomu ya machozi yapigwa.
Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na
Ukawa, Edward Lowassa, akiwapungia mkono maelfu ya wananchi baada ya
kumaliza mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, uliofanyika kwenye Viwanja
vya Furahisha mkoani Mwanza jana. Picha: Halima Kambi
Mwanasiasa mkongwe nchini ambaye amejiengua CCM hivi karibuni na
kujiunga na harakati za Lowassa kuwania urais, Kingunge Ngombale Mwiru
ameufananisha umati huo na bahari.
"Hii ni bahari haijawahi kutokea... na sijawahi kuona.”
MJI WA SIMAMA
Kabla ya Lowassa kuwasili katika uwanja wa Furahisha alikofanya
mkutano wake wa kampeni mjini hapa jana, baadhi ya wananchi walilala na
kukesha katika uwanja huo ili kuwahi nafasi.
Aidha, maduka na sehemu nyingine za biashara zilifungwa kutokana na umati uliojitokeza kuhudhuria mkutano huo.
Awali, mamia ya vijana walijitokeza katika Uwanja wa Ndege Mwanza
kwa ajili ya kumlaki mgombea urais huyo wa Ukawa, huku wengine wakipiga
deki barabara alizopita kuelekea uwanja wa Furahisha.
Akizungumza na wananchi hao katika mkutano wa kampeni uwanjani hapo, Lowassa alisema ataibadilisha Tanzania kwa spidi 120.
"Na wale ambao hawawezi naomba watupishe ili sisi tuendelee na kazi," alisema.
Aidha, alisema Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zinaweza kugharamia elimu bure na kuwalipa vizuri walimu.
Lowassa pia alisema atahakikisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
linachukua mara nne ya sasa ya vijana ili kuongeza ufanisi katika maeneo
mbalimbali nchini na kwamba akiingia madarakani atahakikisha wenyeviti
wa serikali, vijiji na mitaa wanalipwa posho.
DUNI
Naye Mgombea Mwenza wa Urais wa Ukawa, Juma Haji Duni, alisema uongozi ni hekima na si mabavu.
"Kiongozi ni mwenye hekima, huruma na mwenye kujua kuwa ni kiongozi
kwa sababu amechaguliwa na wananchi...sisi tunakwenda Ikulu kufanya
wema na si mabaya," alisema.
Aidha, aliwataka wananchi hao kujiamini na kutoogopa kwani CCM lazima itaondoka madarakani.
"Hawa jamaa (CCM) wamechanganyikiwa na hata hawajui nini wanachokifanya," alisema.
Duni alidai kuna mpango unaofanywa na CCM kuiba kura ili mgombea
wake wa urais, Dk. John Magufuli, ashinde urais uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alidai ili kutimiza mikakati hiyo, serikali ya CCM imeongeza vituo
hewa 24,000 vya kupigia kura na wapiga kura hewa milioni tisa.
"Tumewauliza Nec (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) kuhusiana na vituo
hivyo hewa lakini wamekosa jibu, 'wameufyata'...ila sisi tunawaambia
kuwa patachimbika," alisema.
KIWIA
Mgombea ubunge Jimbo la Ilemela (Chadema), Highness Kiwia, alisema
watu wa Mwanza wanakilio cha muda mrefu tangu Rais Jakaya Kikwete
alipowaahidi kuwajengea eneo la biashara (Machinga Complex) lakini
hajatekeleza ahadi hiyo.
Aidha, alisema Hospitali ya Bugando imetelekezwa, haina dawa za kutosha wala vifaa tiba.
"Mheshimwa Rais (Lowassa), tunaomba utakapoingia madarakani uweze kutatua matatizo haya ya wananchi," alisema.
WENJE
Naye, mgombea ubunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje, aliwaomba
viongozi wa dini kuwaombea Nec na vyombo vya usalama ili waweze kupata
ujasiri wa kutenda haki katika uchaguzi mkuu.
MBATIA
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye ni Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa, alidai mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli akiwa Wizara
ya Ujenzi alianzisha miradi 301 yenye thamani ya Sh. trilioni 5.3 lakini
ameshindwa kuwalipa wakandarasi na kuisababishia Tanzania kudaiwa Sh.
bilioni 124.8.
Aidha, aliyashukuru madhehebu ya dini nchini kwa kuwaruhusu waumini wao kwenda kupiga kura siku ya Jumapili.
"Nawashukuru sana tena sana kwa kujua umuhimu wa kupiga kura na
kuwaruhusu waumini wenu kupiga kura siku hiyo... hii ina maanisha kuwa
siku ya ukombozi imefika," alisema.
KINGUNGE
Ngombale-Mwiru alianza kwa kuwasalimia watu: ‘Mabadilikoooo’...na kuitikiwa ‘Lowassa’.
Wakati akizungumza Kingunge alishangiliwa na wananchi waliojitokeza uwanjani hapo kwa kumuita:
"Babu...babu...babu, Kingunge alisema yeye anaongozwa na misingi na
maadili ingawa uongozi wa CCM umevunja misingi hiyo kwa kuwanyanyasa
wagombea urais 38 waliokuwa wakiwania kuteuliwa na chama hicho.
"Nilipoona hivyo ilibidi niondoke CCM ili niwaache waendelee
kuvunja maadili...wengine walijifanya kuwa ni wafuasi wakubwa wa Hayati
Julius Nyerere, walikuwa wanatamba," alisema.
AWATAKA CCM KUFUNGA MDOMO
Aliwataka viongozi wa CCM kufunga midomo yao na wasiendelee kumjadili baada ya kukihama chama hicho.
"Naomba nitamke wazi kuwa mimi nipo upande wa mabadiliko...nilianza
mabadiliko hayo kuanzia Tanu hadi CCM na sasa vyama vingi...kama kuna
watu wapo CCM wanahitaji mabadiliko waje huku tuungane nao," alisema.
AMSHANGAA MAGUFULI
Alisema anamshangaa Magufuli kwa kuahidi vitu vingi ambavyo havitatekelezeki.
"Namshangaa ndugu yangu Magufuli, ana ahadi ambazo hazifiki mwisho...hata sijui atazitekeleza vipi?" alihoji.
Alisema Lowassa anatosha kuwa Rais kwa sababu ameonyesha uvumilivu kwa miaka nane.
"Ametukanwa, amepakaziwa, amezuliwa mambo lakini yeye amekaa kimya
wala hawajibu...wamesahau kuwa wanazidi kumjenga kwa wananchi," alisema.
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, aliwaomba CCM kuachia nchi kwa amani.
"CCM hatuhitaji vurugu, tunaiomba iachie nchi kwa amani bila vurugu zozote," alisema.
Sumaye alisema ataungana na Wenje Oktoba 24 mkoani Mwanza kwa ajili ya kufunga kampeni.
MGEJA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja,
alisema huu ni muda wa Rais Jakaya Kikwete kuanza kuwaandaa wenzake
kisaikolojia ili waweze kukabidhi nchi kwa wapinzani kwani wameshindwa
kuongoza.
WATU WAZIMIA
Watu zaidi ya 60 wanadaiwa kuzimia na wengine kujeruhiwa katika
mkutano huo kutokana na msongamano mkubwa katika viwanja hivyo
vilivyofurika hadi barabarani.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo,Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza,
Charles Mkumbo, alisema hadi baada ya kumalizika kwa mkutano huo hakuwa
amepokea taarifa zozote zaidi ya matukio mawili ya kuumia kwa watu
walioanguka kutoka kwenye mti waliokuwa wamepanda na pia kupigwa kwa
mabomu ya machozi kwa nia ya kuwatawanya wafuasi kadhaa wa Ukawa.
Kamanda Mkumbo alisema kuna watu watano wameumia na mmoja akiwa
katika hali mbaya baada ya kuanguka kutoka katika tawi la mti waliokuwa
wameupanda ili kufuatilia kila kinachoendelea uwanjani hapo.
Alisema watu hao walikimbiziwa katika Hospitali ya Sekou Toure na wanaendelea na matibabu.
"Hawa vijana walikuwa wamekaa katika tawi moja la mti lililoachia
ghafla na kuwaangusha, wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Sekou
Toure," alisema.
MABOMU YA MACHOZI
Katika hatua nyingine, Kamanda Mkumbo alisema polisi walilazimika
kufyatua mabomu kadha ya machozi kuwatawanya baadhi ya wafuasi wa Ukawa
waliokuwa wakipita mbele ya ofisi za CCM Nyamagana huku wakiwa na kila
dalili ya kufanya fujo mahala hapo.
Alisema mbali na matukio hayo, hakukuwa na matukio mengine ya makubwa.
Lowassa amebakiza mikoa miwili ambayo ni Mbeya na Pwani kukamilisha
kampeni zake kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba, 25, mwaka huu.
Imeandikwa na Jacqueline Massano na Daniel Mkate, Mwanza
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment