ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 5



SHINDI ulianza kunukia. Kukubaliwa tu na msichana yule kwenda naye hotelini kwa mazunguzo ilikuwa sehemu ya ushindi. Potelea mbali kuhusu masharti aliyosema angempa, yasingemshinda!
“Kwanza masharti yapi?” akajiuliza Chris.
“Hana cha kunishinda huyu,” akazidi kuwaza.
Tabasamu changa lilichanua usoni mwa Chris wakati akizidi kufaidi uzuri wa macho ya msichana yule wa kuvutia; Laura! Kama kungekuwa na mashindano ya kumsaka mwanamke mwenye mvuto hasa wa kike, Laura lazima angeshinda.
Nini hana?
Angalia miguu yake. Hebu mtazamo anavyozungumza kwa mpangilio mzuri. Ona nyusi zake, angalia kiuno. Mwone hata mikono yake laini, mizuri inayoshawishi.
Laura ni mwanamke wa haja. Hana upungufu wowote kwa kumwangalia. Chris alivuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu. Akanyanyua glasi yake yenye pombe kali na kuipeleka kinywani.
Ilikuwa kali lakini hakujali. Aliifuta yote, aliposhusha glasi chini, ilikuwa tupu! Laura akawa anaangalia sinema ya bure. Akaachia tabasamu changa la kupendeza.
“Sawa kaka Chris?” Laura akauliza.
“Bila shaka Lau.”
“Mbona hujauliza kuhusu masharti?”
“Sina shaka kabisa na masharti yako, najua nitayamudu tu.”
“Unajua ni nini?”
“Kwanza utanirudisha chuo...” akasema Laura kwa sauti ya kudeka.
“Hilo limepitishwa bila kupingwa....lingine?”
“Hatutafanya chochote.”
“Wewe! Chochote lazima tufanye, maana tunakwenda kuzungumza.”
“Mi’ sitaki!”
“Hutaki?”
“Ndiyo sitaki.”
“Sasa mbona umekubali kwenda hotelini?”
“Nimekubali kwa ajili ya mazungumzo tu.”
“Sasa kwani hayo mazungumzo siyo chochote?” akauliza Chris.
Sura ya Laura iliyokuwa imekunjamana sasa ikarudi kawaida kabisa. Tabasamu likaonekana. Uzuri wake ukazidi kuchanua.
“Tuondoke zetu basi!” akasema Chris.
“Poa, twende.”
Waliongozana hadi nje, wakashikana mikono kama vile walikuwa wakifahamiana kabla. Laura alijishangaa sana kumzoea Chris kwa muda mfupi kiasi hicho.
Macho ya watu wote yalikuwa kwao. Tatizo ni umaarufu wa Chris. Moja kwa moja hadi kwenye taksi. Wakaingia.
“Wapi brother?”
“Aqua Vitae Resort.”
“Buku tano tu.”
“Endesha gari kaka.”
Dereva ni kama alikuwa amechanganyikiwa. Haraka akawasha gari na kuliondoa kwa kasi kuelekea Aqua Resort.
***
Chumba kilikuwa kikubwa, kizuri chenye hewa safi iliyochanganyika na manukato hafifu yasiyokera pua. Chris alikuwa amekaa kitandani na Laura kwenye sofa kubwa! Taa chumbani mle ilikuwa ya rangi hivyo kumfanya Laura azidi kuonekana katika mwonekano wa kuvutia zaidi.
Kitanda kilikuwa kikubwa, chenye mito mikubwa minne iliyopangwa vizuri kitandani. Mashuka meupe nayo yalizidi kukifanya chumba kionekane nadhifu zaidi.
Ni saa nane za usiku!
“Karibu sana Laura,” akasema Chris.
“Ahsante sana.”
“Kikubwa nilichotaka kukuambia ni kwamba wewe ni mrembo sana na unaweza kufanya vizuri kwenye sanaa kama ukiwezeshwa na kupewa mwongozo mzuri. Nakuambia ukweli, kuna uwezekano mkubwa sana wa kumfunika hata Wema au Johari.
“Niamini mimi, uwezo wako ni mkubwa sana Laura. Kubali nikusaidie tafadhali. Isitoshe nina sinema yangu mpya ambayo naiandaa, kuna sehemu ndani yake inahitaji sana msichana kama wewe. Nakuhakikikishia wewe ni staa na maisha yako yanaweza kubadilika ukitumia kipaji chako ipasavyo,” akasema Chris kwa sauti ya taratibu sana.
Shoti ya umeme wa mapenzi ilimwingia moyoni. Ilikuwa nafasi kubwa na muhimu sana kwake. Hakutakiwa kufanya ajizi katika nafasi ile ya pekee. Msichana mrembo kama Laura kuingia chumbani kwake halafu aondoke hivihivi?
“Kaka Chris, kweli mimi naweza kuwa msanii? Naweza kuwazidi hata mastaa?”
“Kabisa...niamini mimi. Ni marekebisho madogomadogo tu.”
Chris aliwaza kwa muda, alitakiwa kuwa na mbinu za kisasa ili aweze kumpata Laura. Lakini alijihakikishia moyoni kwamba alimpenda kwa dhati ya moyo wake. Kumpata kwa usiku ule tu halikuwa jambo muhimu kwake, alimtaka kwa maisha yake yote!
“Lakini nikimkosa usiku huu, sitaeleweka. Anaweza kuniona sijakamilika,” akazidi kuwaza Chris.
Itaendelea kesho

Powered by Blogger.