ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 4



ILIPOISHIA...
Yule msichana alitulia kwa muda, Chris bila kupoteza muda, akamsogelea kidogo. Naye akaanza kumwangalia kwa macho yanayozungumza. Chris alikuwa akifikisha ujumbe wake moja kwa moja.
SASA ENDELEA...
ILA kilichotokea ukumbini mle alihisi ni kama alikuwa ndotoni. Ukweli haukuwa huo, hakuwa anaota. Kila kitu kilikuwa yakinifu kwa hakika kabisa.
Akaufaidi uzuri wa yule msichana kwa karibu kabisa. Moyoni alikuwa na furaha akijua kuwa angalau alikuwa akielekea kutimiza lengo lake. Kukaa naye pale pekee kulimpa matumaini mapya.
“Samahani kaka Chris,” akasema yule msichana kwa sauti iliyojaa utulivu na unyenyekevu.
“Achana na samahani...unaitwa nani mrembo?”
“Naitwa Laura.”
“Nice name...sikia...sitaki kukupotezea muda wako. Kikubwa ni kwamba nahitaji kuzungumza na wewe. Si hapa club na ujue kabisa ni mambo ya kazi,” akasema Chris kwa uhakika kabisa.
Laura akatulia kwa muda.
Muda huu sasa, Laura alipata nafasi nzuri ya kumwangalia Chris kwa ukaribu. Aliyafumbua macho yake makubwa yaliyozungushwa na wanja hafifu mweusi na kuyatuliza usoni mwa Chris.
Kuna kitu kipya aligundua; Chris alikuwa mwanaume mwenye wivu na aibu kidogo. Ukimya na uso wake uliojaa bashasha ulizidi kumpa matumaini kuwa amekutana na mwanaume makini.
“Umesema kazi?” akauliza haraka kama aliyegutuliwa mawazoni.
“Ndiyo.”
“Mimi nasoma.”
“Najua lakini unaweza kufanya kazi nje ya masomo yako.”
“Mh! Kazi gani?”
“Sanaa.”
“Unamaanisha filamu?”
“Ndiyo! Wewe ni msanii mkali sana, hujapata nafasi tu. Unaweza kuwapindua wasanii wote wanaotamba Bongo Movies sasa hivi. Niamini mimi. Unaweza sana ni kiasi cha kupewa nafasi na kuelekezwa kidogo sana, utakuwa mkali.”
“Unataka tuzungumze lini?”
“Leo, maana kesho nasafiri kwenda Mkalama.”
“Mkalama ni wapi?”
“Yaani hujui wilaya ambayo ipo katika mkoa unaoishi?”
“Mimi ni mwanafunzi tu hapa, natokea Mwanza. Kule ndiyo kwetu. Niambie kuhusu Ilemela, Sengerema, Kwimba, Ukerewe, Magu, Nyamagana na Misungwi nitakuambia lakini hapa najua hapahapa mjini tu labda sana Ikungi na Manyoni.”
Chris akacheka.
“Haya mama, nimekuelewa vizuri sana. Namaanisha usiku huu.”
“Tukazungumzie wapi sasa?”
“Hotelini.”
Laura akafura!
Macho ya Laura ni kama yalijitokeza yote yalipojificha. Yalizidi kuwa makubwa na kuchambua kope zake zilizotingishika kwa kasi kutokana na kufumba macho na kufumbua mara kwa mara.
Sura ya Laura ilionekana wazi kabisa kuchukizwa na maneno aliyoyasikia kutoka kwa Chris. Alimwangalia kwa dharau kidogo, akimchambua kuanzia chini hadi juu.
“Chris kumbe uko hivyo?” akauliza Laura kwa hamaki.
“Nikoje?”
“Sikia nikuambie, mimi siyo malaya kama unavyonichukulia. Nimekuja club kwa pesa yangu na nitaondoka mwenyewe baadaye kwa muda wangu lakini huwezi kunipata kirahisi hivyo kwa sababu sijui ya pesa zako au kwa vile unajulikana. Mimi siyo wa hivyo. Umekosea njia!”
“Unanifikiria vibaya Laura. Mimi si mwanaume wa namna hiyo. Tafadhali usinipe sifa ambayo si yangu. Naomba unielewe, lengo langu ni kazi tu, hakuna kitu kingine.
“Inawezekana hujajua thamani ya kipaji ulichonacho au hakuna aliyewahi kukuambia kuwa kuna kitu kama hicho ndani yako. Lakini pia inawezekana umeathiriwa na tabia ya wanaume wengi, wakitaka kumsaidia mwanamke lazima wawe wapenzi kwanza...that’s not me!”
“Sasa kwa nini unataka iwe hotelini?” Laura akamwuliza akimkazia macho.
“Vizuri sana. Kwanza ni kwa sababu ndipo nilipofikia lakini pia kuna utulivu mkubwa zaidi ya hapa.”
“Lakini mbona hata hapa tunaweza kwenda kuzungumzia nje?”
“Laura tafadhali heshimu mawazo yangu na unatakiwa kujua kuwa utakuwa salama kwa kila kitu. Tafadhali naomba ukubali.”
“Sawa tutakwenda kuzungumza hotelini lakini kwa masharti!” akasema Laura sasa kwa utulivu.
“Paaaaaa!” moyo wa Chris ukapiga kwa nguvu.
Itaendelea kesho.

Powered by Blogger.