ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 3



 


ILIPOISHIA...
“Nimeshajua cha kufanya!” akajisemea Chris akipiga funda moja dogo, akachanganya na mate, akameza.
SASA ENDELEA...
SASA alipata wazo jipya. Wazo ambalo kwa hakika lingeweza kumsaidia kumpata yule msichana. Alianza kumfuatilia kijana mmoja ambaye alionekana kama wangeweza kuelewana kidogo. Aliachana na wote, akabaki akimwangalia huyo tu. Mara yule kijana akajitoa pale na kutembea akielekea chumba maalum cha kuvutia sigara. Chris na glasi yake, akamfuata yule kijana.
“Oyaa mambo vipi?” Chris akamsalimia.
“Aaaaah! Mkubwa, bora nimekuona nitapona. Inakuwaje mwana?”
“Salama.”
“Umeingia lini Singapore?”
“Jioni ya leo...samahani huu ni mguu wako lakini kama hutajali kachukue kwanza kinywaji. Unakunywa nini?”
“Ngumu bro.”
“Ngumu?”
“Ndiyo.”
“Unamaanisha nini?”
“Kitu cha konya ndo mzuka.”
“Sawa, kachukue kubwa na pakiti nzima ya fegi,” akasema Chris akimkabidhi noti mbili za elfu kumikumi.
Yule jamaa akaondoka na dakika mbili tu baadaye alirudi akiwa na chupa kubwa ya pombe kali aina ya konya na pakiti ya sigara. Akamrudishia chenji Chris ambaye alimshika mkono na kumtoa katika kile chumba cha kuvutia sigara.
“Vipi?”
“Njoo huku.”
Waliishia kwenye sofa kubwa ndani ya ukumbi ule, pembeni na meza ya Pool Table ambapo bila kupoteza muda, Chris alianza kumwuliza kuhusu yule msichana.
“Nimewaona muda mrefu mkicheza na yule dada. Vipi unamfahamu vizuri?” akauliza Chris.
“Tunasoma naye.”
“Kati yenu pale kuna mtu wake?”
“Mtu wa wapi? Yule msichana ni mwanafunzi mwenzetu tu, hakuna mwenye kisu kikali pale kaka. Yule demu ni mkali chuo kizima.”
“Mnasoma chuo gani?”
“Uhasibu.”
“Oke! Sikia nikuambie mdogo wangu, yule mtoto mimi nimempenda..siyo kwamba nakuambia kwakuwa sijui kutongoza laah! Nataka tu unisaidie kunikutanisha naye, maana naona kama ananata fulani hivi...mambo mengine nitajua mwenyewe.”
“Usiogope mwanajeshi wangu, hilo limepita.”
“Kweli?”
“Wewe sema unataka aje sasa hivi?”
“Ndiyo...”
“Nakuja naye.”
“Sawa.”
“Njoo kwanza....” Chris akamwita yule kijana ambapo mara moja alirudi.
“Hujaniambia jina lako bado.”
“Naitwa Julius.”
“Poa.”
Julius akaondoka. Kama mchezo hivi, dakika moja baadaye, alifika alipokuwa amekaa Chris akiwa amemshika mkono yule msichana. Akamkalisha kwenye sofa kubwa, akamuweka katikati. Pembeni wakamzunguka na Chris.
“Huyu ni kaka yangu...anaitwa Chris. Nimesoma na mdogo wake JK Nyerere Sekondari, Moshi. Tunaheshimiana sana lakini nimechukizwa na tabia yako ya dharau kwake,” Julius akamwambia yule msichana huku akimkazia macho.
Chris akashtuka.
“Mbona huyu dogo anataka kuharibu sasa?” akawaza.
“Nimemfanyaje?” yule msichana akauliza.
“Hujui? Najua unanata na una dharau lakini kwani wewe humfahamu Chris? Utakuja kupoteza bahati bure wewe mtoto wa kike...si kila mwanaume ni mhuni,” akasema Julius kwa hasira.
Pamoja na kwamba kile alichokuwa akikifanya ilikuwa ni maigizo tu ili kumuunganisha na Chris lakini pia pombe aliyokunywa ilikuwa inafanya kazi yake sawasawa.
“Samahani bro Jully.”
“Siyo mimi, wa kumuomba msamaha ni huyu hapa...mimi nawaacha, naamini utafanya hivyo.”
Yule msichana akatingisha kichwa kukubaliana naye. Julius akasimama na kurudi zake ‘Smoking Room’.
Yule msichana alitulia kwa muda, Chris bila kupoteza muda, akamsogelea kidogo. Naye akaanza kumwangalia kwa macho yanayozungumza. Chris alikuwa akifikisha ujumbe wake moja kwa moja.
Itaendelea wiki ijayo.

Powered by Blogger.