ad

ad

Uzinduzi kampeni za Ukawa...Matukio 7 nyuma ya pazia!


WAKATI Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakizindua kampeni zao za uchaguzi mkuu kwenye Viwanja vya Jangwani, Dar, Jumamosi iliyopita, matukio saba yamenaswa nyuma ya pazia, Ijumaa Wikienda linatiririka nayo.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa Ukawa, Emmanuel John Makaidi (NLD), James Francis Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Aikaeli Mbowe (Chadema) na Seif Sharif Hamad (Cuf) na wote walimpigia debe mgombea urais wao, Edward Ngoyai Lowassa.


HIRIZI, UNGO
Katika mambo hayo saba, moja ni kabla ya kuanza kwa mkutano huo, wananchi waliojitokeza walijikuta wakiyahusisha matukio kadhaa yaliyotokea uwanjani hapo na imani za kishirikina hasa baada ya mvua kunyesha.
Kioja kilichowashtua wengi ni kunaswa kwa mwanaume mtu mzima aliyekuwa na hirizi na ungo akiwa katikati ya uwanja na kuondolewa na wanausalama wa vyama husika akipewa onyo.
Baadhi ya watu walimtaja mtu huyo kwamba alitaka kutumia nafasi ya uwanja huo kujaa kuwawangia kwa faida zake mwenyewe. Lakini wenyeji wa uwanja huo walisema wanga kwenye viwanja hivyo ni kawaida na wala si wakati huu wa kampeni tu.
NJIWA WATANO
Tukio la njiwa watano kuruka kwenye anga la viwanja hivyo nalo liliwashangaza wengi, wengine wakidai ni ishara ya vyama husika kupima upepo wao wa kisiasa bila kufafanua.


WALIOZIMIA WAELEZA YA AJABU
Katika uzinduzi huo, watu kadhaa walianguka na kupoteza fahamu. Wote wakiwa wanawake.
Ijumaa Wikienda lilizungumza na wawili kati yao ambapo kila mmoja kwa wakati tofauti alisema alianza kuona giza nene mbele yake na kuhisi usingizi. Hata hivyo, watu wa Msalaba-Mwekundu walisema hali hiyo ilisababishwa na joto la msongamano.
MA- LOWASSA FEKI
Vijana waliobadilisha rangi nywele zao kuwa nyeupe ili wawe na mwonekano wa ki-Lowassa nao walikuwa miongoni mwa matukio yaliyoshangaza.
Baadhi ya watu walitaka kujua vijana hao walitumia dawa gani mpaka kubadilisha mwonekano wao na baadaye kubainika walipaka rangi nyeupe ya mafuta kichwani na kwenye mustachi!
WAMASAI
Kwa kawaida, jamii ya watu kutoka kabila la Wamasai si rahisi sana kuonekana kwenye shughuli za kisiasa lakini juzi, walijitokeza kwa wingi. Miongoni mwa wanawake waliopoteza fahamu alikuwa mmoja wa jamii hiyo.
Ijumaa Wikienda lilizungumza na wanaume wawili kutoka kabila hilo ambao walisema kufika kwao ni kwa lengo la kumsikiliza Lowassa kwa vile ni mtu wa kwao.
PICHA KWAMBA KUNA NYOMI ILIKESHA
Miongoni mwa mambo yaliyosambaa Jumamosi asubuhi ni picha yenye giza iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha umati ukiwa kwenye viwanja hivyo usiku wa Ijumaa kwenda Jumamosi. Ilidaiwa umati huo ni watu waliofika mapema kuwahi nafasi.
Hata hivyo, kiongozi mmoja wa Chadema (hakupenda kutajwa) aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa, hakuna watu waliolala kwenye viwanja hivyo kwa ajili ya kuwahi nafasi bali ni walinzi waliokuwa wakilinda vitu mbalimbali vilivyotumika kwenye mkutano huo.
WATU KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA YA MKATO
Biashara kubwa kwenye viwanja hivyo ilikuwa kuuzwa kwa fulana za Ukawa na vipeperushi vyenye picha ya Lowassa. Ijumaa Wikienda lilibaini kuwa, biashara hiyo ilifanywa na mtu yeyote aliyeweza kutengeneza vitu hivyo.
MITAA ILIVYOKUWA
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, mitaa mbalimbali ya Dar ilirindima kwa shamrashamra za wanachama wa Ukawa wakiongozwa na bodaboda. Wanachama walikuwa na sare za vyama vyao huku wengi wakinogesha kwa kauli mbiu inayofahamika na wengi ya ‘pipoooz… pawaa!
Hali hiyo ilijionesha hasa kwenye mitaa ya karibu na Jangwani, Mtaa ya Swala, Faru na Jangwani wenyewe ambapo umati wa wanachama wa Ukawa walionekana wakipita katika makundi wakishangilia kabla ya kuelekea uwanjani.
Kivutio katika uzinduzi huo alikuwa mgombea kupitia tiketi ya Chadema, Edward Lowassa na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambao walizinadi sera zao.
Stori: Chande Abdallah, Deogratius Mongela, Richard Bukos, Shani Ramadhani na Mayasa Mariwata.

CHANZO: IJUMAA WIKIENDA
Powered by Blogger.