Mtikila achukua fomu ya urais kwa shingo upande
Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP),
Christopher Mtikila akigoma kusaini fomu za kugombea urais akitaka
ufafanuzi wa mgombea binafsi, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa amekwama
kwenye lifti za jengo lililopo katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC)
kutokana na kukatika umeme.
Mchungaji Mtikila ambaye
aliambatana na mgombea mwenza Juma Metu Juma, alitaka ufafanuzi wa
kutokuruhusiwa kuwania urais akiwa mgombea binafsi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wakati Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika
(AfCHPR) imeruhusu.
“Siondoki hapa na wala sitaweza
kuchukua hizi fomu hadi mniambie ni wapi nitapata jibu la tume la
kukiuka maagizo ya mahakama ya Afrika.
“Waandishi embu
subirini kwanza mkurugenzi wa uchaguzi aje hapa ilia atoe ufafanuzi na
nyie msikilize mkaandike ukweli kwa sababu hii siyo haki ni sawa na
kudharau mahakama,” alisema.
Baada ya kuzozana na
maofisa waliokuwa wakimkabidhi fomu hizo, walilazimika kumuita
mkurugenzi wa uchaguzi Kailima Ramadhani, ambaye alimwambia kwamba
sheria hairuhusu.
“Sisi tunafuata sheria mwenyekiti
kama hicho kipengele kingekuwapo tungekuruhusu uchukue fomu hizo, lakini
hapa tunabanwa na sheria tunaruhusu kutoa fomu kwa watu wanaotoka
kwenye vyama vyao,” alisema Ramadhani
Alisema ni vizuri
Mtikila angefuatilia kwa makini suala hilo ili sheria ipitishwe kwani
NEC wanachokifanya ni kufuata sheria zilizopo tu na si vinginevyo.
Baada
ya kumaliza maongezi Mtikila aliamua kuweka sahihi na kuchukua fomu
hizo kwa shingo upande huku akisema atakiwakilisha vyema chama chake
hicho.
Juni 13,2013 Mtikila alishinda kesi aliyofungua
AfCHPR, mjini Arusha akidai Tanzania inakiuka demokrasia inapozuia
wagombea binafsi.
Mchungaji Mtikila, ambaye ana
historia ndefu ya kukwaruzana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM),
alifungua shauri mahakama ya Afrika mwaka 2011 baada ya jitihada zake za
kupindua mabadiliko ya kikatiba yaliyofuta ugombea binafsi kugonga
mwamba kwenye mahakama za kitaifa.
Dovutwa
Mwenyekiti wa UPDP Fahmi Dovutwa alikwamba kwenye lifti kwa dakika kumi baada ya jana kuchukua fomu za kuwania urais.
Dovutwa
ambaye alikuwa wa kwanza kufika kuchukua fomu saa tatu asubuhi, akiwa
ameambatana na mgombea mwenza, alisema kwamba kukwama kwake kwenye lifti
ni hujuma iliyofanywa na baadhi ya wagombea wenzake wa urais.
Wakati
huohuo; Mgombea urais kwa tiketi ya TLP Maxmilian Lyimo, ambaye hakuwa
na mgombea mwenza alikuwa wa pili kufika katika ofisi hizo kwa ajili ya
kuchukua fomu.
Mgombea huyo alifika saa 5:33 asubuhi
baada ya kuchukua fomu alisema kuwa upepo wa Uchaguzi Mkuu unaovuma
mwaka huu, haukuwahi kuvuma wakati mwingine wowote, hivyo inaashiria
kuwa nchi itapata kiongozi asiyetarajiwa na wengi.
“TLP
ni chama kisichochafua amani tangu kuasisiwa kwake, hivyo wananchi
waangalie amani ya nchi kwani ni bora kuliko kitu kingine,”alisema na
kuongeza:
“TLP bado kuna nafasi za uongozi kuanzia kata
hadi za ubunge, wanaoshindwa huko waliko tunawakaribisha kwa ajili ya
kuja kugombea nafasi hizo.”

Post a Comment