ad

ad

First Eleven Simba… Wapisheni wanaume

KIKOSI cha Simba katika maandalizi yake ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kimekuwa kikijifua vikali huku kikitumia kambi mbili tofauti wilayani Lushoto, Tanga na Zanzibar ambako kipo mpaka sasa.

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha mkuu, Muingereza, Dylan Kerr, kinaonekana kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa juu ambao hata akikosekana mmoja ni vigumu kuliona pengo lake, ni rahisi kusema kuwa msimu huu wana kikosi imara zaidi.
Akizungumzia ishu hiyo, Kerr aliliambia Championi kuwa kwa sasa hana ‘partnership’ ambayo moja ni kali kuizidi nyingine, bali kila mchezaji akimpanga na yeyote basi wanacheza kwa kuelewana.

Simba ambayo msimu uliopita ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu, inaonekana kuwa imara huku tayari kukiwa na baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa na uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza lakini licha ya hivyo, hata wale watakaoanzia benchi wanao uwezo wa hali ya juu.
Katika lango, Vincent Angban anapewa nafasi ya kwanza huku Ivo Mapunda na Peter Manyika wakiwa benchi.

Beki ya kulia anasimama Hassan Kessy, huku wakiwa na uhaba kwenye nafasi hiyo, lakini beki ya kushoto yupo Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akisaidiwa na Samih Nuhu, huku 
Hassan Isihaka na Juuko Murushid wakimaliza beki ya kati na kama mmoja akikosekana bila shaka Mohammed Fakhi, anaweza kuziba pengo hilo bila wasiwasi.
Kwenye nafasi ya kiungo hapa ndiyo kuna shughuli kubwa kwani Jonas Mkude, Peter Mwalyanzi, Mwinyi Kazimoto na Awadh Juma ndiyo wanaoweza kuanza, huku wakiwa wanapewa presha na Said Ndemla, Simon Sserunkuma, Abdi Banda waliopo benchi na Justice Majabvi kama atafuzu majaribio yake.

Washambuliaji wao, Hamis Kiiza na Mussa Hassan Mgosi wanatarajiwa kuanza kikosi cha kwanza huku Elius Maguli, Ibrahim Ajibu, wakisubiria katika benchi.
Kocha anena…
Championi Jumatano lilizungumza na Kerr kuhusiana na kikosi hiki na kueleza kwamba ni kizuri sana huku akitaja sababu za Ivo kuanzia benchi.
Moja ya sababu hizo ni kipa huyo hajafanya mazoezi na wenzake kwa takriban wiki tano, lakini anayo nafasi ya kuwa ‘first eleven’ kama atarudi na kuonyesha makali yake kama zamani, lakini kwa sasa atasubiri.
Powered by Blogger.