ad

ad

ACT yaahidi vipaumbele vinne


Dar es Salaam. 
Chama cha ACT – Wazalendo kimezindua kampeni na ilani yake kikiahidi kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa yenye vipaumbele vinne endapo kitapewa ridhaa ya kushika dola.
Akizungumza jana kwenye uzinduzi uliofanyika katika Viwanja vya Zakhem Mbagala, jijini hapa, mgombea urais wa chama hicho, Anna Mghwira alisema Serikali hiyo itaundwa na viongozi wa vyama vya siasa na makundi mbalimbali ya jamii.
Baada ya kukabidhiwa ilani hiyo na Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe, mgombea huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho aliahidi kurejesha hadhi ya Mji wa Dodoma kuwa makao makuu ya Serikali, yatakayokuwa kitovu cha kuwaunganisha Watanzania kutoka mikoa yote nchini.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, hifadhi ya jamii, afya na elimu na kwamba itakuwa mwongozo katika utekelezaji wa majukumu yake.
Alisema ACT – Wazalendo inayoongozwa kaulimbiu ya utu, uzalendo na uadilifu, katika uchaguzi ujao itawajibika kwa wananchi na Taifa kwa kuwekeza katika maeneo manne ya vipaumbele hivyo.
Mghwira alisema ili kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini, Serikali ya ACT – Wazalendo inalenga kutengeneza Taifa linalofanya kazi kwa kuchukua hatua madhubuti katika sekta za kilimo, viwanda, utalii, madini, mafuta na gesi asilia.
Alisema ili kujenga uchumi shirikishi, ni muhimu kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha kilimo  kinaanza kuchangia vya kutosha ukuaji wa uchumi, ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
“Shughuli za kilimo lazima ziendeshwe na wananchi wenyewe kwa kuwawezesha kumiliki ardhi, kuongeza tija na kupata mitaji kwa kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii,” alisema.
Alisema lazima kuwe na mfumo wa hifadhi ya jamii na utawekewa utaratibu wa kuweka fao la bei ya mazao, bima ya mazao na mifugo na mikopo ya gharama nafuu kwa vikundi vya wakulima ili kununua pembejeo za kilimo na ufugaji kwa lengo la kuhami mwananchi.
“Ardhi na mashamba yote yaliyokuwa ya mashirika ya umma na kubinafsishwa yarejeshwe kwa wananchi wasio na ardhi… wajibu wa kuhakikisha mazao ya kilimo ya wananchi yote yamenunuliwa kwa bei nzuri utakuwa wa Serikali kupitia shirika la umma litakaloundwa mahsusi kwa kazi hiyo,” alisema.
Chini ya kipaumbele hicho, alisema ataweka msukumo kwenye viwanda vikiwamo vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuchochea mauzo ya nje.
Kuhusu utalii alisema, shabaha ni Tanzania kuwa na uwezo wa kuingiza na kuhudumia watalii milioni tano kwa mwaka na kuingiza fedha za kigeni zisizopungua Dola za Marekani nane bilioni kwa mwaka.
“Makusudio ya Serikali katika sekta ya utalii itakuwa si kukusanya kodi tu, bali ni kuzalisha ajira na kuongeza mapato ya fedha za kigeni. Sekta ya utalii ina nafasi kubwa ya kuzalisha ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla.
Alisema ACT – Wazalendo kitaagiza serikali kuweka mfumo rahisi wa kodi katika sekta kwa kuondoa msururu wa kodi. Huku akiahidi: “Kuunda upya Shirika la ndege la Taifa ili liwe chachu ya kuongeza mapato ya fedha za kigeni nchini.”
Mgombea huyo aliahidi kuweka maliasili zote za madini, mafuta na gesi asilia kuwa mali ya wananchi kikatiba na uchimbaji wake kuwa na kibali cha wananchi.
“Mapato yatokanayo na maliasili ya nchi yawekwe kwenye mfumo maalumu na kutumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, upanuzi wa huduma za afya na elimu,” alisema.
Afya 
Kuhusu afya, mgombea huyo alisema: “Mpango wa ACT – Wazalendo kuhusu afya katika kukabiliana na changamoto za huduma mbovu za afya, vifo vya watoto wachanga na kina mama wajawazito na uchakavu wa miundombinu, ni kuwekeza katika huduma za kinga.
“Serikali itatenga bajeti maalumu kwa ajili ya kupanua mafunzo ya kada zote za afya katika vyuo vikuu vya umma na kuweka ushirikiano maalumu na vyuo binafsi vya afya ili viweze kutoa wataalamu wengi zaidi katika fani za afya,” alisema.
Elimu 
Mghwira alisema chama hicho kinaamini kuwa elimu ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo na kwamba lengo ni kuwekeza kikamilifu katika sekta hiyo ili kuhakikisha watu wengi wanapata fursa ya kusoma katika mazingira bora.
“Ili kupanua fursa na kuboresha viwango vya elimu katika ngazi mbalimbali, Serikali ya ACT – Wazalendo itaanza utekelezaji wa sera mpya ya elimu inayounganisha mfumo wa elimu ya msingi na sekondari ili kufanya elimu ya msingi kuwa miaka 10, kama ilivyo kwa Zanzibar,” alisema.
“Kuwahimiza wazazi na walezi katika kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao kuandikishwa shule na kuweka utaratibu imara zaidi wa kisheria utakaotoa adhabu kwa wazazi na walezi ambao hawawapeleki watoto wao kuandikishwa shule,” alisema.
Hifadhi ya jamii 
Akizungumzia kipaumbele Mghwira alisema, “Tunakusudia kupanua hifadhi ya jamii na kuwafikia wakulima, wafugaji na wananchi wengine waliojiajiri kwa kutunga sheria.”
Alisema analenga kutumia hifadhi ya jamii kuwezesha wananchi kujiwekea akiba kupitia vyama vyao vya ushirika kama Sacoss na kupata mikopo ya gharama nafuu ili kuanzisha biashara ndogondogo, kupata bima ya afya na kuhimili mahitaji kama ya kusomesha watoto.
Alisema serikali yake itaboresha sheria ya hifadhi ya jamii kwa kuunganisha mifuko iliyopo sasa na kubakia na mitatu tu; wa bima ya afya, sekta ya umma na wa hifadhi ya jamii ambao utahusisha sekta binafsi na isiyo rasmi.
“Ili kufikia malengo hayo, Serikali yetu itaongeza shughuli za uzalishaji mali ili kuwezesha wananchi kuwa na kipato, kuondoa misamaha ya kodi isiyo ya lazima na kutunga sheria itakayohakikisha kuwa misamaha ya kodi haizidi asilimia moja ya Pato la Taifa.
“Kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, kuweka mfumo mpya wa kodi za kimataifa ili kuzuia kampuni za kimataifa kumomonyoa wigo wa kodi na kupanua wigo wa kodi kwa kuhakikisha kila raia mwenye kipato analipa kodi kwa kujaza kila mwaka.
“Pia, tutarahisisha mfumo wa kodi ili kuondoa mizengwe na kuwezesha watu kulipa kodi bila shuruti kwa kushusha kiwango cha chini cha kodi ya wafanyakazi (Paye) mpaka asilimia tisa.
Pia, aliahidi kupambana na ufisadi, kuimarisha uongozi bora, kupiga vita rushwa na kusafisha uozo ili kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali.
By Suzan Mwillo, Mwananchi
Powered by Blogger.