ad

ad

HUKATAZWI KUMFUATILIA MPENZI WAKO LAKINI KWA NINI UMFUATILIE?

Mapenzi ya zama hizi yamejaa changamoto nyingi sana. Usaliti umekuwa mwingi kiasi kwamba, kila anayeingia kwenye uhusiano anajipa asilimia chache za kutosalitiwa.

Ndiyo maana leo hii hakuna anayeweza kusimama na kusema hasalitiwi na mpenzi wake, kila mmoja kwa wakati flani hujihisi kuibiwa lakini anajaribu kupotezea mawazo hayo ili asijikoseshe amani.

Ni kweli, ukitaka mapenzi yakukoseshe amani, itakuwa hivyo! Utashindwa kufanya mambo yako ya msingi kwa sababu tu mpenzi uliyenaye hakupi kile ulichokitarajia. Tusifike huko!

Tujengeane mazingira ya kuaminiana lakini pale tunapohisi tunaibiwa, siyo dhambi kufuatilia ili kujua ukweli. Ndiyo! Lazima kufuatilia kwa sababu kuendelea kuwa mpole wakati unaona kabisa kuna mtu unashea naye penzi ni uendawazimu.

Ndiyo maana leo nikaona nizungumzie hii tabia ya baadhi ya wapenzi kufuatiliana na kuchunguzana sana kiasi cha kukoseshana amani. Ninachojaribu kukiweka wazi hapa ni kwamba, huzuiwi kumfuatilia mpenzi wako lakini je, kuna sababu ya msingi ya kufanya hivyo?

Wapo watu huko mtaani, anamuaga mkewe anaenda kazini lakini haendi. Anabaki mitaa ya nyumbani kufuatilia kama mkewe huwa anaingiza wanaume ndani kwake akiwa hayupo.

Achilia mbali hao, wapo wanawake hasa maeneo ya mjini wanatoa pesa zao kuwalipa watu ili wawafuatilie waume zao kubaini kama wana michepuko. Sasa unajiuliza, kwa nini mtu atumie melfu kibao ya fedha ili kumchunguza mumewe ambaye hana hata dalili ya kusaliti?

Kama umetonywa mara nyingi sana kuwa mtu wako ana vimwana kibao huko nje, sioni tatizo wewe kujiridhisha kwa kumfuatilia kwa staili hiyo lakini kama hakuna mazingira ya kukufanya umhisi vibaya, kisha ukatumia muda na pesa zako kumfuatilia, hiyo ni kazi bure!

Ndiyo maana nikasema unapojipanga kumfuatilia mpenzi wako uwe una na sababu ya kufanya hivyo na pia ujiandae na majibu ya uchunguzi wako.

Nasema hivyo kwa sababu unaweza kuhisi mpenzi wako ana mtu mwingine, ukamuuliza, akakukatalia. Swali ni je, siku ukigundua kuwa ulichokuwa ukihisi au ulichoambiwa na wambeya kina ukweli utachukua uamuzi gani? Je, utamuacha?

Swali hilo ulipe jibu kabla ya kuanza kazi ya kumfuatilia. Kwamba ukigundua kuwa ni kweli anakusaliti utampa nafasi ya kubadilika au utamuacha? Na kama utamuacha, unadhani utakuwa ni uamuzi sahihi?

Kama hutamuacha, je utakuwa tayari kuendelea kuwa kwenye uhusiano na mtu ambaye huna uhakika kama ataacha tabia ya kukusaliti au ataendelea nayo? Hayo ni mambo ya kujiuliza.

Ndiyo maana sasa baadhi ya watu huwa hawana ‘time’ ya kuwafuatilia wapenzi wao. Siyo kwamba hawawapendi, la hasha! Wanawapenda lakini wanajua wakiwafuatilia watagundua mambo yanayoweza kuwafanya wakaachana na wao hawako tayari hilo litokee.

Kimsingi mambo ya kufuatiliana yamepitwa na wakati na ukimuona mtu anamfuatilia sana mpenzi wake ujue huyo anatafuta sababu waachane. Kwa nini? Kwa sababu leo hii hata wewe unayesoma makala haya ukiamua kumfuatilia mpenzi wako, utagundua vitu ambavyo vinaweza kukufanya ukaamua kumuacha.

Nishauri kwamba katika ulimwengu wa sasa siyo vizuri wapenzi kufuatiliana    kwani mpenzi wako akibaini unamchunguza wakati yeye katulia anaweza kukuacha.
Powered by Blogger.