Msuva: Baba baki na Simba
Mfungaji bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara na mshambuliaji ya Yanga, Simon Msuva.
MFUNGAJI bora wa msimu uliopita
wa Ligi Kuu Bara, Simon Msuva, amemwambia baba yake mzazi, Happygod
Msuva, amuache na Yanga yake na yeye abaki na Simba yake.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni siku chache
tangu baba yake atangaze kumzuia mwanaye kuongeza mkataba mwingine Yanga
mara huo alionao utakapomalizika ili aende Simba au akacheze soka la
kulipwa.
Kiungo huyo, hivi karibuni alitangazwa
kuwa mchezaji bora wa msimu uliopita, huku akifanikiwa kutwaa tuzo ya
ufungaji bora kwa kupachika mabao 17 akifuatiwa na mshambuliaji wa Yanga
Mrundi, Amissi Tambwe.
Akizungumza na Championi Jumatano,
Msuva alisema kuwa kikubwa baba yake anatakiwa kutambua soka kwake
anachukulia kama ajira inayoendesha maisha yake ya kila siku.
Msuva alisema, baba yake anachukulia
soka kama burudani kwake kutokana na kuwepo na mapenzi na Simba. Lakini
amesisitiza yeye hachezi soka kwa ajili ya kumfurahisha baba yake, hivyo
ni vyema akafahamu hilo.
“Ujue mara nyingi nimekuwa nikimzuia
baba yangu kuongea na waandishi kwa kuhofia kuongea tofauti kwa hofu ya
kunigombanisha na viongozi, pia mashabiki wa Yanga.
“Watu wengi wanajua kama baba yangu ni
Simba, hivyo anavyoongea tofauti kuhusiana na mimi na timu yangu ya
Yanga, mimi ndiye ninayeathirika kwa kukosa uaminifu kwa mashabiki.
“Hivyo, nikwambie tu mimi sina mpango
kwa hivi sasa wa kuondoka Yanga na ninaomba nimwambie kuwa, yeye abaki
na Simba yake na mimi aniache na Yanga yangu.
“Kwa sababu mimi bado ni mchezaji halali
wa Yanga mwenye mkataba wa mwaka mmoja ambao unatarajiwa kumalizia
Juni, mwakani ni vyema akalifahamu hilo,” alisema Msuva.

Post a Comment