ad

ad

JOSE MOURINHO HAKUNAGA

 
Mashabiki wa timu ya Chelsea wakiwa wamebeba bango la kumsifia, Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho.
LONDON, England
MWACHE Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho atembee kifua wazi na kutamba katika mitaa mbalimbali ya Jiji la London, kwani ni miongoni mwa makocha wachache wageni waliopata mafanikio England.
Sifa kubwa ya kocha huyu raia wa Ureno ni maneno mengi yenye kejeli, dharau, majigambo na mambo mengine mengi ambayo hugeuka na kuwa burudani kwa mashabiki wakati mwingine.
 
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho akiwa amebeba Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya England.
Mara ya kwanza aliifundisha Chelsea kuanzia mwaka 2004 hadi 2007 akitokea Porto ya Ureno, kisha akaondoka zake kujiunga na Inter Milan, lakini akarejea tena klabuni hapo mwaka 2013 akitokea Real Madrid na hadi leo anapiga mzigo.

Ndani ya kipindi hicho, Mourinho amefanikiwa kuipa mataji manane Chelsea ikiwemo ubingwa mara tatu wa Ligi Kuu England, raha iliyoje kwake na familia yake.
Msimu huu wa ligi hiyo unaofikia tamati kesho Jumapili, Mourinho ameshatwaa ubingwa wake na anachofikiri sasa ni ushiriki wake katika msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na ligi kuu.
Mourinho akiwa akiongea na mashabiki.
AZILAUMU MAN UNITED, ARSENAL KUMPA UBINGWA
Mourinho, haishiwi vituko moja ya kauli alizotoa wikiendi iliyopita wakati timu yake ilipofungwa mabao 3-0 na West Brom, alikuwa na sentensi tata kuhusu kipigo hicho lakini alienda mbali zaidi kwa kuziponda klabu kubwa za Arsenal, Manchester United, Liverpool na Manchester City.
"Sisi ni mabingwa. Usitegemee twende kwenye basi letu huku tukilia eti kwa sababu tumefungwa mabao 3-0. Nina furaha kwa sababu tumefungwa? Hapana, wala sina furaha. Lengo letu lilikuwa ni kutwaa ubingwa na kurejea nyumbani si zaidi ya hapo.
Akaongeza: "Watu wa kulaumiwa hapa ni hizi timu kubwa ambazo zimeturuhusu kutwaa ubingwa huu kirahisi kabisa.”
Akiongea na wanahabari (hawapo pichani).
HATA ANGEKUWA MAN CITY ANGETWAA UBINGWA TU
Beki wa zamani wa Chelsea na Ufaransa, Marcel Desailly anaamini kwa mbinu alizonao, Mourinho angeweza kutwaa ubingwa wa England hata kama angekuwa anaifundisha Man City inayonolewa na Manuel Pellegrini.
“Siamini kama makosa yanayofanywa na Pellegrini, yangefanywa pia na Mourinho, namjua huyu kocha (Mourinho) angefanya jambo na kikosi kilekile kingetwaa ubingwa.
“Unajua kwa nini? Sababu zake ni rahisi sana. Kwanza, unahakikisha safu ya ulinzi ipo imara. Pili, badala ya kutumia vipaji binafsi uwanjani wafanye wachezaji wako wacheze kama timu, lazima mshinde na ndicho anachofanya Mourinho.
“Hivi una watu kama Aguero (Sergio), Fernandinho, Fernando na Yaya Toure halafu unakosa ubingwa? Hao wote wana vipaji ambavyo alipaswa kuwepo mtu wa kuviunganisha,” anasema Desailly.

KAULI ZAKE TATA
Mourinho anasifika kwa kauli zake tata na kali kwa makocha wenzake, kuna wakati amewahi kumwambia Kocha Arsene Wenger wa Arsenal kwamba: "Nafikiri kuna mtu mmoja ana jicho kali sana. Anapenda kutazama wengine tu, anakaa nyumbani kwake na familia yake akiwa na darubini kali sana kuwatazama wengine wanafanya nini. Kila mara (Wenger) anaongea kuhusu Chelsea.”
Kuna wakati alipewa shutuma ya kupangiwa kikosi na mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich lakini haraka akajibu: “Ikitokea Abramovich akanisaidia hata kusimamia mazoezi yetu basi timu itashika mkia, na hata mimi nikiingia katika biashara zake tutapata hasara kubwa!”
Alipokuwa Real Madrid hakutaka wachezaji nyota kama Cristiano Ronaldo kuwa juu yake, aliwahi kusema: “Ni bora timu icheze na wachezaji kumi tu kuliko kumsubiri mtu aliyechelewa basi.”
Lakini ana adabu kwa kocha wa zamani wa Man United, Sir Alex Ferguson: “Namheshimu sana Ferguson, namuita bosi kwa sababu yeye ni bosi wetu (makocha). Ni mtu makini na anastahili kuwa bosi, huwezi jua nikifisha miaka 60 naweza kupata heshima kama yake.”
 
MADRID YAMNYATIA
Muda mfupi tu baada ya kutwaa ubingwa wa England msimu huu, Mourinho amehusishwa na mipango ya kujiunga na Real Madrid ya Hispania ambayo haijatwaa ubingwa msimu huu na tayari amezungumza nao.
Baada ya kukosa ubingwa, mabosi wa timu hiyo wanataka kumtimua Carlo Ancelotti ili kupata kocha mwingine atakayewapa ubingwa. Majina ya makocha wanaowaniwa ni Julen Lopetegui wa Porto, Jurgen Klopp (Borussia Dortmund), Rafa Benitez (Napoli) na Mourinho aliyewahi kuifundisha timu hiyo kati ya mwaka 2010-13.
“Mourinho ameshazungumza nao lakini amekataa ofa ya kujiunga nao,” kilisema chanzo cha habari, lakini Mourinho alipoulizwa akajibu: “Siyo kweli kwamba nataka kujiunga nao, isipokuwa nilimpigia simu raia wao ili kumpongeza kwa timu yao ya mpira wa kikapu kutwaa ubingwa si vinginevyo.”

AMETWAA UBINGWA NCHI NNE
Tofauti na watu wengine waliojaliwa maneno mengi halafu utendaji dhaifu, Mourinho anaweza kuwa kocha mwenye historia ya pekee baada ya kutwaa mataji ya ligi kuu za nchi nne duniani ambazo ni Ureno, England, Italia na Hispania.
Kocha huyu amewahi kutwaa ubingwa Ligi Kuu Ureno ‘Primeira Liga’ msimu wa 2002/03 na 2003/04 akiwa na Porto, Ligi Kuu Italia ‘Serie A’ akiwa na Inter Milan msimu wa 2008/09 na 2009/10, Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ akiwa na Real Madrid msimu wa 2011/12 na sasa England.
Akiwa na Chelsea alitwaa ubingwa kwa mara ya kwanza msimu wa 2004/05, halafu 2005/06 na hivi sasa 2014/15. Kwa jumla Mourinho ametwaa mataji 22, huku ya Ligi ya Mabingwa yakiwa mawili.
Mara ya kwanza alitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2003/04 akiwa na Porto na 209/10 akiwa na Inter Milan. Mataji mengine ni yale ya ndani katika nchi alizofundisha pia Kombe la Uefa ndogo.
Jina: Jose Mourinho Felix
Kuzaliwa: Januari 26, 1963
Mahali: Setubal, Lisbon, Ureno
Nafasi: Kocha
Klabu: Chelsea

No comments

Powered by Blogger.