ad

ad

HOTUBA YA MHE. NCHEMBA: TAIFA LETU KUWA LA KIPATO CHA KATI

Taifa letu kuwa la kipato cha kati. Hii ni habari njema kwa kila mtanzania aliyemsikiliza Mhe. Mwigulu Nchemba ambaye ana kauli mbiu ya #Mabadiliko ni Vitendo Wakati ni Sasa. Kilichonivutia sana kwa mtangaza nia huyu ni uwezo wake wa kueleza ni kwa namna gani anaweza kutupeleka huko kwenye kipato cha kati kwa kutumia viwanda vya ndani. Lakini bado najiuliza inawezekana kweli? Tunajua maneno mara zote ni rahisi kuliko vitendo lakini angalau tumesikia njia ambazo kama atapewa ridhaa basi anaweza kuzitumia kutufikisha huko kwenye uchumi imara.
 29551-mwigulu1


Hotuba ya Mhe. Nchemba imesheheni mambo kadha wa kadha ya kuvutia na kutuacha tukitoa udenda nje kwa hamu ya kupata yale aliyoyazungumza kwa ujasiri mkubwa. Ametamka mambo makubwa matatu ambayo atayasimamia iwapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi yetu. Mambo hayo muhimu ni: 1.Kuhakikisha kila mtanzania anayestahili kulipa kodi basi analipa kodi 2. Kuweka nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ikiwemo kuziba mianya yote ya matumizi mabaya 3. Kukomesha ufanyaji kazi wa mazoea.
Nimefarijika sana kuona kati ya vipaumbele vyake ni kuinua viwanda vya ndani. Hicho kimekuwa kilio changu cha muda mrefu. Jana nilisema kuwa hakuna nchi yoyote duniani ambayo inaweza kuendelea bila kuendeleza teknolojia yake ya ndani. Watanzania tunaendelea kuwa wategemezi wa bidhaa za watu Kwasababu tu tumeshindwa ama tumekuwa wavivu wa kuwekeza na kuendeleza teknolojia yetu.
Kinachotokea ni kwamba badala ya kutengeneza bidhaa zetu wenyewe na kuziuza ndani ya nchi na kutafuta masoko mengine nje ya nchi tumeishia kuwa wauzaji wa malighafi kwenye nchi za magharibi tena kwa bei wanayopanga wao. Kama hutaki ondoka na pamba yako tuone utaifanyia nini? Laiti tungekuwa na viwanda vyetu si tungetumia malighafi zetu wenyewe? Serikali inashindwaje mbona Bakhressa ameweza matunda yaliyokuwa yanaoza yamepata kazi. Sasa fikiria tungekuwa na kina Bakhressa kama mia tungekuwa na haja ya kunyanyasika kwenye soko la dunia si tungezitumia hizo malighafi hapa hapa nchini? Hivi kuna mtu ambaye hajawahi kutumia bidhaa za Azam? Inawezekana kabisa na ndiyo maana nimefurahi kusikia Mhe. Nchemba akilipa kipaumbele suala hili. Mkulima ahangaike na mazao kununua pembejeo na dawa, halafu eti mwisho wa siku mtu mwingine anapanga bei, huu si utumwa jamani?
Mhe. Nchemba amekuja na mkakati mzuri wa kuhakikisha kwamba hatuwi wategemezi tena kwenye soko la dunia na badala yake tunaweza kujifunga mkanda tumboni na kushirikiana na sekta binafsi kuanzisha viwanda mbalimbali ambavyo tutaweza kutumia malighafi zetu wenyewe badala ya kukimbilia kwenda kuziuza katika soko la dunia. Akaenda mbele zaidi na kuonyesha jinsi anavyoweza kufanikiwa jambo hilo kwa kuwafanya watanzania wenyewe ndiyo wawe wateja wa kwanza wa bidhaa zitakazotengenezwa na viwanda vyetu kwa kutumia malighafi yetu. kwa mfano akasema sare zote za shule nchi nzima, nguo za jeshi n.k zizalishwe katika viwanda vyetu ambavyo vinatumia pamba yetu.
Mimi naamini kama tutaimarisha viwanda vyetu vya ndani ikiwemo kuvifufua vile vilivyokufa faida tutakazopata ni pamoja na kuongeza vipato vya watanzania wakiwemo wakulimu, kutengeneza ajira kwa vijana ambao wanazurura tu mitaani bila kuwa na ajira lakini vilevile itatusaidia kuimarisha fedha yetu kwasababu tutakuwa na bidhaa (hapa namaanisha bidhaa na si malighafi) ambazo tutaweza kuziuza nchi za jirani na kwingineko duniani zikiwa na lebo ya ‘Made in Tanzania’. Kama kweli Mhe. Nchemba amezungumza kwa dhati kutoka moyoni na si mambo ya kisiasa kama tulivyozoea basi kwa mikakati aliyoisema bila shaka tunaweza kuinua viwanda vyetu vya ndani na hatimaye kusaidia uchumi wetu kupiga hatua kadhaa mbele. Lakini kama ni maneno tu ya kisiasa kama yale ya ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’ basi uchumi wa kati tutaendelea tu kuusikia katika nchi za wenzetu na kwenye vyombo vya habari. Lakini tujiulize kama wachina wameweza kwanini sisi tunashindwa? Hivi nani anaweza akasimama na kusema hana kitu chochote ambacho kimetengenezwa China?
Pamoja na kuvutiwa na yaliyozungumzwa hasa hili la kuendeleza viwanda vyetu. Swali ni je itawezekana kufika huko Kwa kutumia chama hichi hichi ambacho kimeshindwa kwa zaidi ya miaka hamsini kutuondoa katika lindi la umasikini? Kwani hata miaka kumi iliyopita si tuliahidiwa maisha bora kwa kila mtanzania? Yapo wapi? Si tumeishia kuona kundi kubwa la vijana wakiitwa kwenye usahili uwanja wa taifa kuwania nafasi chache zilizotangazwa? Huku lindi kubwa la vijana likiendelea kurandaranda mitaani mikononi wakiwa wameshikilia vyeti vyao vya chuo kikuu? Ni nini ambacho Mhe. Nchemba atatumia kubadili mfumo uliopo uliojaa rushwa na ufisadi kufikia hayo yote aliyoyazungumza kwa ujasiri? Ama hili ni changa lingine la macho? Maneno ni rahisi lakini vitendo vinawezekana?
Mhe. Nchemba amezungumza mengi kwenye afya amegusia suala la wizi wa dawa kwenye hospitali za serikali, elimu ya juu atahakikisha kila mtoto wa kitanzania mwenye vigezo anapata fursa hiyo. Amezungumzia suala la rushwa, umeme, michezo na suala la kulipa kodi. Pamoja na hayo yote lakini moyo wangu umeguswa sana na ari yake ya kutaka kuinua viwanda vyetu na kukuza teknolojia yetu ya ndani. Yaani natamani siku nikitembelea Kenya nikute tuna duka kubwa (Supermarket) ambalo limesheheni bidhaa za watanzania kama ilivyo hapa kwetu. Tuna maduka makubwa kama ya Nakumati, lini na sisi tutakuwa na maduka makubwa katika nchi za wenzetu? Tunachotaka watanzania sasa ni vitendo, tumeshachoshwa na maneno. Tumechoka kuahidiwa maisha bora, tumechoka kuahidiwa ajira kwa vijana, tumechoka kuahidiwa huduma bora za maji na umeme, tumechoka kuambiwa watoto wetu watapata elimu bora. Tumechoka,tumechoka tumechoka, tunataka vitendo sasa.

No comments

Powered by Blogger.