BAVICHA WATOA TAMKO JUU YA DAFTARI LA WAPIGA KURA
Katibu
wa BAVICHA, Julius Mwita, akitoa tamko kuhusu muda mfupi uliopangwa wa
kuandikisha wapiga kura nchini kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Kulia ni
Mratibu Uhamasishaji wa BAVICHA, Edward Simbeye.
BARAZA la Vijana wa Chadema (BAVICHA) wametoa tamko juu ya daftari la wapiga kura kwa mfumo wa ‘BVR’.Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Katibu Mkuu wa BAVICHA, Julius Mwita, amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshindwa kutekeleza matakwa ya wananchi kutokana na muda wao walioupanga wa kujiandikisha wa siku saba kuwa mdogo na kutotosha.
Amesema tume hiyo haina malengo ya dhati kwa wananchi wake kutokana na usumbufu wanaoupata wakati wa kujiandikisha, hali inayosababisha wengi wao kulala katika vituo vya kujiandikisha.
“Tumeshuhudia watu wakikesha ama kulala nje katika zoezi hili la uandikishwaji, jambo linalopelekea wananchi wengi kukosa haki ya msingi ya kujiandikisha, au kuipata katika wakati mgumu sana. Tumeshuhudia hivyo Njombe, Songea, Mtwara Iringa na maeneo mengine Watanzania wakiamka alfajiri na hata kukesha kwenye vituo vya kujiandikisha,” alisema Mwita.
Aliongeza kuwa tume lazima ikubali kuwa muda wa kuandikisha wa siku saba ni mfupi na hautoshi, hivyo kuiomba tume hiyo kukubali kuongeza muda na kuongeza idadi ya vifaa kwa ajili ya kulifanya zoezi hilo kuwa la ufanisi.
“Viongozi wetu wakuu wa chama, Mwenyekiti na Katibu Mkuu, wamefanya ziara katika maeneo kadhaa, na wamejionea ulaghai wa hali ya juu unaofanywa na NEC ambapo wanatangaza kuwa watakuwa mkoa fulani, lakini cha kushangaza wanakuwepo katika kata tatu mpaka tano, jambo linalowachanganya wananchi na kuwafanya wakeshe vituoni,” alisema.
Aidha alieleza jinsi tume hiyo ilivyotenga siku 12 za kuandikisha watu mkoani Dar es Salaam, jambo alilolisema kuwa ni kichekesho, akisisitiza BAVICHA haitakubali kuburuzwa kwa wananchi wa mkoa huo na kuwa watachukua hatua kuilazimisha NEC kuongeza muda.
Mwita pia aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kugombea nafasi za uongozi.
“Mwaka jana wakati wa uchaguzi wa ndani ya chama, Mwenyekiti, Freeman Mbowe, aliutangaza mwaka 2015 kama mwaka wa vijana na wanawake, hivyo na sisi BAVICHA tunawaasa vijana kujiandikisha kwa wingi ili kupata haki ya kuamua hatma ya nchi hii,” alisema Mwita.
NA DENIS MTIMA/GPL
Post a Comment