ad

ad

Kitanzi, Kisu au Bastola - 9



ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Angalia!” aliongea Madam Flaviana huku akimpatia bahasha ndogo Side aliyeipokea kwa wasiwasi na kuifungua.
“Ndiye, siye?” aliuliza Madam Flaviana akimtazama Side aliyekuwa akizikodolea picha alizozitoa ndani ya bahasha ile.
Tiririka Nayo...
“Vipi?” Madam Flaviana aliuliza tena baada ya kumuona Side akitetemeka kwa hofu kama mtu aliyeona jini.
Picha zilikuwa sawa kabisa na mtu waliyemkamata usiku wa jana yake, isipokuwa tofauti ilikuwa ni unene na nywele ambazo kwenye picha alikuwa nazo tofauti na alivyomuona.
Akili ya Side ikafanya hesabu za harakaharaka na kujipongeza kwa kile alichokiita kujihami, kwa kuwa alikuwa tayari ameishafikiria jinsi ya kumtorosha Dedan mapema kabla ya kufika hapo kwani alijua lazima Dedan atakuwa ni mtu yuleyule waliyemkamata jana yake.
Kikwazo kikabaki kuwa Madam Flaviana.
Side alijiuliza ikiwa mwanamke huyo atataka akamuone huyo mtu waliyemkamata jana yake wangempeleka nani tofauti na Dedan? Hata kama wangempeleka mtu mwingine ambaye Side tayari alikuwa ameshamuandaa badala ya Dedan je, Madam Flaviana atamwacha mtu huyo akiwa hai? Side alijiuliza maswali hayo kwanza kabla hajajibu swali  aliloulizwa na Madam Flaviana. Hakutaka kuona damu ya mtu mwingine ikimwagika kwa ajili yake.
Muda wa kufikiri ulikuwa umekwisha kwa Side, alihofia pengine angempandisha hasira Madam Flaviana kwa kuchelewa kujibu maswali yake haraka iwezekanavyo, kwa ujasiri akafungua kinywa chake.
“Siye,” alijibu Side huku akishindilia picha zile ndani ya mifuko ya suruali yake.
“Siye!..twende ukanioneshe huyo mtu uliyenaye,” aliongea Madam Flaviana kwa hamaki huku akipiga hatua kuelekea mahali lilipo godauni.
Side alikuwa makini akiitegemea hatua hiyo ya Madam Flaviana, kwa pamoja wakaelekea ndani ya godauni hilo ambalo mara nyingi hulitumia kwa mambo yao ya kikatili.
“Ooh shit! Namtaka Dedan haraka sana siyo chizi huyu!” aliwaka Madam Flaviana baada ya kumuona mtu asiyefanana hata chembe na Dedan akiwa amefungwa kitambaa kizito usoni na mikononi.
Kwa hasira Madam Flaviana akaikoki bastola yake akitaka kumuulia mbali mtu huyo.
Ghafla Side akamuwahi Madam Flaviana na kuukwepesha mkono wake, risasi mbili zikatua pembeni bila kumpata huyo chizi.
“Madam, mtu mwenyewe ni chizi asiyejitambua unapoteza nguvu zako bure,” aliongea Side akimpooza Madam Flaviana aliyefura kwa hasira.
Kwa ushawishi huo Side alifanikiwa kumuondoa Madam eneo hilo bila ya damu ya mtu yeyote kumwagika. Akamfungulia chizi huyo na kumuacha huru aondoke zake, cha kushangaza ndiyo kwanza alikuwa aking’ang’ania kubaki maeneo hayo bila uoga wowote.
***
Salima aliamka katikati ya usiku akiwa mchovu sana kutokana na wingi wa pombe alizokunywa mchana wa siku hiyo. Akiwa amechanganywa na giza la usiku, alihisi huenda alipitiliza siku nzima akiwa kitandani. Akilini mwake alihitaji kujua nini kilikuwa kikiendelea muda wote alipokuwa amelala. Akaamka na kuufungua mlango wa chumba chake akaelekea kwenye korido kuu inayovitenga vyumba vingi katika upande wa kulia na kushoto.
Ukimya wa hali ya juu ndani ya jengo hilo haukumtisha na kumfanya asitembee huku na huko akichunguza kila sehemu ya jengo hilo ambalo tangu ahamishie makazi yake humo hakuwahi kulichunguza.
Akiwa katika kutembea huko, ghafla alihisi kuna mtu alikuwa akimfuata nyuma yake. Mwili wake ukasisimka kwa mtindo wa ajabu. Akageuka nyuma na kutazama, lakini hakukuwa na mtu yeyote.
Bila hofu Salima akaendelea kutembeatembea, bila kujua kuwa hisia zake zilikuwa kweli, kwani Mr. John Chakos ndiye mtu pekee aliyekuwa akimtazama kupitia kamera zilizotegwa humo ndani akimfuatilia kila alipokuwa akielekea usiku huo.
Alimaliza kuzunguka kila mahali katika ghorofa hiyo, akapanda ngazi inayoelekea ghorofa ya juu yake na kushangazwa na muundo uleule wa vyumba kama ulivyokuwa katika ghorofa aliyoitazama mwanzoni. Vyumba vingi katika ghorofa hiyo vilikuwa havina madirisha wala milango iliyoruhusu kutazama mazingira ya nje. Kwa namna moja ama nyingine Salima alistaajabishwa na ramani ya jengo hilo lililokaa kama aina fulani ya gereza.
Akiwa katika mawazo hayo mara alisikia muungurumo wa lifti ikishuka kutoka ghorofa ya juu na kusimama. Mara akasikia sauti ya mlango wa umeme ukifunguka na kufuatiwa na hatua za watu. Hakutaka kukamatwa akichunguzachunguza mambo ya watu usiku kama alivyokuwa akifanya. Hatua zilizidi kusogea kuelekea mahali alipokuwa.
Laiti kama angechelewa kujificha kwa dakika moja tu, basi watu hao waliokuwa wakipita maeneo hayo wangemkuta hapo.
Kwa muda huo kona ya korido tu ndiyo iliyokuwa ikimfanya asionekane. Bila kupoteza muda Salima alijaribu kufungua mlango wa chumba kilichokuwa karibu yake mara moja ukafunguka kisha akajitosa ndani yake asijue kama chumba hicho kilichotanda kwa kiza totoro kilikuwa ni cha nani!
Nini kiliendelea? Usikose wiki ijayo katika gazeti hili.

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Kwa muda huo kona ya korido tu ndiyo iliyokuwa ikimfanya asionekane. Bila kupoteza muda, Salima alijaribu kufungua mlango wa chumba kilichokuwa karibu yake, mara moja ukafunguka kisha akajitosa ndani yake asijue chumba hicho kilichotanda kwa kiza totoro kilikuwa cha nani!
SASA ENDELEA…
Hatua zile zilifika na kukomea hapohapo kwenye chumba alichoingia Salima. Mara akasikia mlango ukifunguliwa na kufungwa huku sauti za minong’ono na miguno ya kimahaba zikisikika kutoka kwa watu hao ambao kwa sauti zao, Salima aliwatambua kuwa wote walikuwa wanawake.
Salima alikuwa ameshajua jinsi gani alivyojiweka matatani kwa kuingia ndani ya chumba hicho, kwani kama angelikubali aibu ya kukamatwa akizungukazunguka kwenye vyumba vya ghorofa isiyomhusu, ingelikuwa afadhali kuliko kujitokeza muda huo, tena akiwa ameshaingia kwenye chumba cha watu. Akaendelea kujificha nyuma ya sofa kimya bila kutikisika wala kutoa sauti akisubiri nini kitakachofuatia.
***
Wakati huo Mr. John Chakos alikuwa akikosa uhondo wa kuona kile kilichokuwa kikiendelea ndani ya kile chumba. Kamera zake zilishindwa kupata picha angavu kutokana na kiza kilichotanda ndani ya chumba hicho.
Mara ya mwisho alimuona Salima akijificha na kukimbilia humo ndani ambapo baada ya dakika chache, aliwaona Madam Bernadeta na Julieth nao wakiingia huku wakiwa wamekumbatiana na kupigana mabusu mfululizo.
Mara nyingi amekuwa akiwaona wakiwa katika hali hiyo na pengine hata wakifanya mapenzi ya jinsi moja. Jambo hilo halikumsumbua Chakos hata kidogo kwa kuwa Madam Bernadeta na Delilah walikuwa wakifanya kazi zao vizuri.
Mr. Chakos alitaka kushuhudia jinsi ambavyo Salima atajiokoa na kutoka humo chumbani bila kuonekana. Akawa makini kuangalia video ya chumba kile bila kupepesa macho kwa kuhofia kupitwa na shoo ile.
“Wawili kwa mmoja, Salima! Mtoto mzuri utatokaje?” Mr. Chakos alijikuta akizungumza mwenyewe huku macho yake yakiangalia kwa makini giza nene la chumba kile kwa kutumia televisheni kubwa zilizounganishwa kitaalamu na kamera za jengo zima la Serenity, lakini aliambulia kusikia sauti za akina Madam na Delilah tu wakiwa katika mambo yao.
***
Usiku huo, Madam Flaviana akiwa kwenye gari lake tayari kwa kuondoka, machale yakamcheza. Akairudisha siku nyuma na kutafakari, taratibu akaona shaka juu ya tabia ya Side.
Alikumbuka jinsi Side alivyokuwa na wasiwasi alipomkabidhi azitazame picha za Dedan, pia alishindwa kujua kwa nini Side alikuwa na huruma kiasi kile hata akamkwepesha mkono wake alipotaka kumfyatulia risasi yule mwendawazimu aliyefungwa ndani ya godauni!
Madam Flaviana alihisi kuna kitu kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Akaanza rasmi kumtilia shaka Side. Akainua simu yake ya mkononi na kubofya namba kadhaa kisha akaiweka sikioni na baada ya muda kidogo:
“Haloo Henry,” aliongea Madam Flaviana kwa madaha huku akivuta sigara kubwa maarufu kama ‘cigarette.’
“Haloo Madam,” ilisikika sauti nzito kutoka upande wa pili wa simu.
“Ninahitaji kukupa kazi nzito, upo tayari?”
“Sema ni nani nikammalize!”
“It’s a rat out mission, no one in particular people (ni mpango wa kumfichua msaliti, siyo mtu fulani moja kwa moja).”
“Guess it’s like old times, is it! (Nadhani ni kama enzi zile au siyo!)”
“Yeah! It’s like old times (Ndiyo, sawia kabisa)”
“Hesabu kazi yako imekwisha. Ni nani mtu huyo?”
“Unamkumbuka Side?”
“Yeah, unahitaji nini kuhusu yeye?”
“Kikubwa nahitaji kujua kila kitu anachokifanya, narudia tena kila kitu!”
“Mh! Nahisi itakugharimu kidogo. Nadhani unajua kuwa mimi ni muuaji siyo paparazi?”
“Usihofu kuhusu malipo, nusu kabla na nusu ukimaliza kazi, sawa?”
“Ok sawa.”
Baada ya kumaliza kuongea na mtu huyo, Madam Flaviana akawasha gari lake na kutokomea gizani, akifikiria jinsi gani Side ataliepuka hilo zimwi aliloliamsha juu yake.
“Better be without any secret Side, otherwise you will be dead (Bora usiwe na siri Side, la sivyo utakufa).”
***
Baada ya purukushani za muda kwenye kitanda, hatimaye muda ulifika na watu hao wakawa kimya kabisa huku sauti pekee Salima aliyokuwa akiisikia ni mlio wa moyo wake tu ambao ulikuwa ukidunda kwa nguvu.
“Madam, nitakuja kesho mi naondoka bwana,” aliongea Julieth na kusimama akiwa na nguo zake mkononi.
“Subiri kwanza kwani unawahi nini?” alisema Madam Bernadeta akimvutia Julieth ndani ya kitanda chake.
“Unamjua yule msichana mpya?” alisema Madam Bernadeta kwa kunong’ona huku akiendelea kumtomasatomasa Julieth.
“Namjua yule anayeitwa Salima?”
Salima alishtuka baada ya kusikia jina lake likitajwa, akatega masikio yake ajue ni nini kilichokuwa kikitaka kuongelewa kuhusu yeye.
Je, nani alilitaja jina la Salima? Usikose wiki ijayo.

ILIPOISHIA
Nilimuangalia mume wangu huku nikitokwa na machozi. Nilijaribu kusema jambo lakini ulimi ulikuwa mzito. SASA SONGA NAYO...
MUME wangu aliamua kujilaza kwenye kochi kisha kunitaka niwe karibu naye ili aniambie jambo. Nilipomsogelea alisema nisijali kwani maneno ya yule mwanamke, yaani Mei yasinitie wazimu.
“Kwa nini amenidhalilisha?”
“Yule Mei japokuwa ni mkwe wangu sitataka akanyage hapa tena.”
“Unasema kweli?” nilimuuliza mume wangu.
“Nakuapia. Hakanyagi hapa. Ninachowaza ni mtoto wangu tu maana bado ni mdogo na najua hana uwezo wa kumtunza.”
“Nikuambie jambo?”
“Sema.”
“Yule amefanya hivyo kwa kuwa anataka mtoto wako amfanye mtaji, yaani apate matumizi ya kila siku kupitia mwanao…”
“Thubutu, hapati kitu hapa!”
Mara tulisikia breki ya gari ambalo lilisimama nje ya nyumba yetu. Nilichungulia na kumuona Mei akitoka huku uso ukiwa umevimba.
Aliingia ndani bila kubisha hodi.
“Nimegeuza gari. Njiani nimemuuliza Pili kama umetoa fedha za matumizi ya mtoto akasema hujatoa, nikamuamuru dereva ageuze gari.”
Tuliangaliana mimi na mume wangu kwa kuwa hayo tulikuwa tukiyazungumza dakika kama mbili zilizopita. Mume wangu aliinuka na kukaa kwenye kochi huku akiwa amekunja uso, aliniangalia nami nikakunja uso.
“Lakini Mei kwani wewe ni mke wangu? Hayo mambo angefanya Pili siyo wewe.”
“Mimi nahusika mia kwa mia, kwani Pili anakwenda kukaa kwa nani?”
“Pili kwenda kukaa kwako ni wewe umejitakia, kwani mimi nimeshindwa kumlea?”
“Kwa maana hiyo unataka kuniambai hutoi?”
“Kwako Mei sitoi hata senti tano. Hapa umemchukua Pili kwa nguvu hata muda wa kumpa hizo fedha ingekuwa saa ngapi”
“Kwani kutoa fedha kunahitaji winji, kalete hizo fedha tuondoke zetu.”
“Nakuambia nenda kwenye gari na ukabaki na mtoto kisha mtume Pili aje hapa nimuelekeze cha kufanya.”
“Yaani unaniamuru kwamba niende nikamchukue mtoto ina maana unanigeuza mimi ni yaya siyo?”
“Hapana.”
“Sasa kwa nini unasema niende kwenye gari nikampakate mtoto, unanivunjia heshima Bwana Chinchi kuwa umemzalisha mwanangu?”
“Huyo ni mke wangu, wewe ulitaka nizae na nani?”
“Na huyo mkeo wa kwanza.”
Baada ya kusema hivyo alinitibua nikasimama na kutaka kumuendea pale alipokuwa amesimama lakini Chinchi mume wangu akanizuia.
“Hebu niache, nikamfundishe adabu huyu pimbi.”
“Nani pimbi.”
“Wewe pimbi, sasa hivi umeponea tundu la sindano na umerudia tena kosa lilelile, sasa nakuua kabisa.”
Wakati nasema hivyo Pili aliingia ndani huku akiwa na mtoto wake.
“Mama, sasa hivi ulikuwa umezimia na unarudia tena kutaka kugombana na mama mkubwa, unafanya vibaya mama.”
“Sifanyi vibaya, mimi napigania haki zako, huoni kwamba huyu bwana anataka kukutesa?”
“Hapana mama, mambo yangu na huyu bwana tuachie wenyewe tutayamaliza.”
“Acha kunifundisha cha kufanya, kosa mimi unadhani huyu bwana angekuoa, si angeendelea kukaa na huyu mwanamke tasa hapa ambaye anajaza choo tu!”
Maneno hayo yalinifanya nitoke jikoni huku nikiwa nimeshika panga, hasira zilikuwa zimenikaa barabara kichwani. Haraka kama umeme mume wangu alinishika huku akipiga yowe:
“Salome utaua, utaua mke wangu…”

Je, nini kilitokea baada ya hapo? Fuatilia siku ya kesho.

No comments

Powered by Blogger.