Kitanzi, Kisu au Bastola - 7

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
“Simama hapohapo!” Salima alisema akimkatiza usemi Madam Flaviana na kushuka haraka akikimbilia moja kwa moja hadi ndani ya nyumba, macho yake yakakutana na mlango wa chumba chake ukiwa wazi huku kila kitu ndani ya chumba chake kikionekana isipokuwa Dedan.
Songa nayo…
Salima hakuwa na muda wa kumshukuru Mungu baada ya kuona kila kitu chake kilikuwa salama, badala yake alizidi kupata wasiwasi na hofu baada ya kubaini kuwa Dedan hakuwepo ndani ya chumba hicho.
Madam Flaviana alimfuata kwa nyuma na kuingia katika nyumba hiyo ambapo watu na majirani walishaanza kutokeza vichwa vyao wakimshangaa Salima na huyo mgeni aliyeambatana naye kwa jinsi walivyopendeza huku watoto wa uswahilini wakilichezea gari la Madam Flaviana kila moja akidai ni la kwake.
Salima alishindwa kujizuia, alikaa chini na kuangua kilio akilitaja jina la Dedan. Madam Flaviana hakuwa akijua kilichokuwa kinaendelea, lakini kwa hali aliyoiona akajua kwamba huyo Dedan aliyekuwa akiishi na Salima hakuwepo chumbani humo jambo ambalo lilikuwa kweli.
Akajitahidi kumkokota Salima huku akimbembeleza hadi ndani ya chumba chake na kumwacha akilia kama mtoto kisha akatoka nje na kuulizia watu kama walimuona mwanaume yeyote akitoka ndani ya chumba hicho.
Watu wote walikuwa kimya wasijue kama Salima alikuwa akiishi na mwanaume mle ndani na wengine wakishangazwa na taarifa za kupotea kwa mtu aliyekuwa akiishi ndani ya chumba hicho na Salima bila ya wao kujua.
Madam Flaviana akiwa katika hali ya kukata tamaa, mtoto mmoja wa kiume alimfuata na kusema alimuona mwanaume mmoja akitokea chumba kilekile alichokuwemo Salima na kuelekea barabara ya Machinjioni.
Kwa siri kubwa Madam Flaviana akamvuta mtoto yule pembeni na kumuuliza kama kuna mtu mwengine alimwambia kuhusu jambo hilo, mtoto yule alijibu kuwa hakuna mtu yeyote aliyemwambia isipokuwa yeye tu.
“Safi sana, sasa usiseme kwa mtu umesikia eeeh!” alisema Madam Flaviana na kuchomoa noti ya shilingi elfu kumi na kumpa, lengo lake likiwa ni kumtenga Salima na jambo lolote litakalomtoa kwenye akili ya kazi waliyotaka aifanye.
Madam Flaviana alijua fika kuwa uhusiano wa mapenzi na kazi zao jinsi zisivyochangamana. Tangu mwanzo alipopata taarifa kuwa Salima alikuwa akiishi na Dedan alikuwa akifikiria jinsi ya kuwatenganisha na siku hiyo ilikuwa kama bahati kwake, ikiwa kama Dedan alitoka humo ndani mwenyewe au lah! Salima hakupaswa kuujua ukweli.
Kwa kificho akatoa simu yake na kumpigia Side akitoa maelekezo amfuatilie mwanaume fulani barabara ya Machinjioni na ikiwezekana ammalize mara moja. Side alifanya kama alivyoamrishwa, akakitonya kikosi kazi chake na mara moja wakaingia mtaani kumsaka Dedan wakati kwa upande wa pili, Madam Flaviana alimdanganya Salima kuwa kampuni imewataarifu polisi na tayari walikuwa wakimtafuta.
Akamshawishi waondoke maeneo hayo kwa usalama wake kwani alimfanya Salima aamini kuwa watu waliotumwa na Caro ndiyo waliomteka Dedan. Salima alikubali kwa kuwa aliamini Dedan hakuweza kusimama wala kutembea mwenyewe na hata kama angeweza kufanya hivyo isingekuwa rahisi kuufungua mlango kwani alikumbuka vyema alivyoufunga, tena kwa ufunguo.
Ni wazi aliyoyasema Madam Flaviana yalikuwa na ukweli ndani yake, akakubali kuondoka maeneo hayo huku akichukua baadhi ya vitu muhimu.
***
Ndani ya jengo kubwa la ‘serenity’ salima alikuwa ndani ya ‘lifti’ akiongozwa na Madam Flaviana mpaka kwenye chumba kilichokuwa ghorofa ya sita alichooneshwa kuwa makazi yake mapya. Mazingira mazuri ya chumba hicho hayakumfanya amsahau Dedan hata kidogo.
Katika mawazo yake alishawishika kuwa kutoweka kwa Dedan ulikuwa ni mchezo aliochezewa na Carolina kama alivyodanganywa na Madam Flaviana. Uoga na hasira vyote vilimjaa kwa pamoja akashawishika kuwa ‘Serenity’ ni mahali salama kwake kwa muda huo japo hakukubali kama amempoteza Dedan moja kwa moja kiasi cha kutoonana naye maisha yake yote.
“Siku moja nitakuona mpenzi wangu, utakuwa wangu tena,” alijiliwaza Salima huku machozi yakimlengalenga. Akapitiwa na usingizi huku akiombea yote yaliyotokea yawe ndoto ya mchana isiyo na ukweli wowote wakati atakapoamka.
***
Usiku uliingia, Dedan alizidi kutokomea mitaani huku njaa ikizidi kumuuma. Hakuna mtu aliyekuwa akimjali hata pindi alipojibana kwenye kona ya Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mwanakwetu akiugulia njaa kali asijue dawa yake.
Kama angelijua kuwa chakula ndiyo tiba ya ugonjwa wake si ajabu angeishajiunga na mapunguwani wenzake waliojazana karibu na jalala kubwa la jiji wakigombania mabaki ya vyakula jirani kabisa na mahali alipokaa, lakini Mungu wake kwa siku hiyo hakuwa kabisa na mja wake huyo. Kiu na njaa kali vilimfanya adhoofu na kupoteza fahamu kabisa, akalala kifo kikimnyemelea, ubongo wake ukiimba nyimbo za huzuni huku taswira na jina la msichana mzuri aitwaye Carolina ikififia kichwani mwake.
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Kiu na njaa kali vilimfanya Dedan adhoofu na kupoteza fahamu kabisa. Akalala kifo kikimnyemelea, ubongo wake ukiimba nyimbo za huzuni huku taswira na jina la msichana mzuri aitwaye Carolina ikififia kichwani mwake.
Songa Nayo...
Usiku huo giza lilikuwa nene kupita kiasi. Watu wengi tayari walisharudi kutoka kwenye mihangaiko ya kila siku na kujifungia majumbani mwao. Hakuna hata mmoja aliyejua kama kuna mtu aliyekuwa akitaabika na njaa huko nje pasipo kuwa na msaada wowote.
Kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele, ndipo kibaridi cha usiku kilizidi kuvuma na kumfanya Dedan azinduke kutoka katika usingizi wa kifo uliompitia. Kidogo fahamu zake zilirejea, akasimama na kutazama kila kona kama vile hakumbuki kama alienda mahali hapo mwenyewe.
Ghafla, tone zito la maji ya baridi lilimwangukia mkononi, akalitazama na kulipangusa mara moja. Mara matone mengi zaidi yalizidi kumwangukia kila sehemu ya mwili wake huku upepo mkali ukiyumbisha miti na mapaa mahali hapo. Kufumba na kufumbua ilizuka mvua kubwa ya upepo.
Dedan akiwa hafahamu lolote, akasimama mahali hapo amejikunyata kwa baridi huku akilowa na mvua pasipo kujua jinsi ya kujikinga nayo. Mvua ilinyesha na kuilowanisha midomo yake mikavu, kidogo maji yaliyopenya yalimpa ladha nzuri katika ulimi wake. Akaachama mdomo huku akiyameza maji ya mvua yaliyokuwa yakitiririka kwa wingi usoni mwake.
Aliendelea kunywa mpaka tumbo lake likagoma kupokea maji tena. Hapo ndipo alipogundua tiba ya kiu chake japo tumbo lilianza kumuuma huku baridi kali likimpiga kila kona, alianza kutetemeka.
Kwa mwendo wa kasi gari moja lilipita maeneo hayo na kufunga breki mbele ya Dedan. Mara moja watu watatu waliovalia makoti makubwa ya mvua walishuka na kumsogelea Dedan. Mkubwa kuliko wote ambaye alionekana kama kiongozi wao, alitoka na kusimama karibu kabisa na gari lile huku wale wawili wakimfuata Dedan.
“Wewe kwa nini upo hapa peke yako?” alisema mmoja wao kwa ukali akimwambia Dedan huku akitazama kila upande kuhakikisha kwamba hakukuwa na mtu karibu.
“Una uhakika ni huyu?” yule mwingine alimuuliza mwenzake huku akionekana kuchoka sana kwa kazi fulani waliyoifanya siku hiyo.
“Funga domo lako bwana we huoni ninajaribu?” alijibu kwa hasira mtu yule wa mwanzo na kumtikisatikisa Dedan aliyesimama akiwatazama kwa uwoga.
“Lazima atakuwa ndiye huyu, angalia!” yule mtu wa mwanzo alimwambia mwenzake baada ya kugundua kucha fupi na ndevu zilizokatwa vizuri usoni kwa Dedan japokuwa alikuwa mchafu kama chizi wengine.
Wote wawili walikubaliana kuwa huyo ndiye mtu waliyetumwa kumtafuta na Side, wakamuangalia yule mtu mwingine aliyesimama nyuma yao akatoa ishara fulani. Mara moja Dedan akapigwa mtama na kufungwa kamba mikono na miguu kisha wakamtupa ndani ya buti la gari na kupotea maeneo hayo.
***
“Haloo (kimya kidogo) ndiyo lakini lazima tuhakikishe kama huyu ndiye Dedan kweli kabla hatujafanya jambo lolote (kimya kidogo..) okey, basi kama Salima atakuwa na picha yake litakuwa jambo zuri (kimya kidogo..) kama atakuwa ni huyu tuliye naye basi hesabu kama kazi imekwisha tayari,” aliongea Side kwa njia ya simu na mtu mwingine.
“Wewe ni Dedan au siyo?” aliongea Side akimtazama Dedan aliyekuwa akifakamia chakula kwa pupa baada ya kuiga mfano kutoka kwa mtu fulani aliyemuona akila pembeni yake.
Kwa jinsi Side alivyosimuliwa na Madam Flaviana kuhusu Salima alivyosahau kumpa chakula Dedan kwa siku nzima, alimuonea huruma mtu huyo na kumpa chakula.
Side alikuwa na amekuwa akishuhudia mara nyingine kusababisha au kufanya mauaji ya watu wengi kwa manufaa ya ‘Serenity.’ Hakufikiria kama angetumwa tena kumuua mtu mwingine ambaye hana hatia kwa masilahi ya kampuni hiyo. Dhamira yake daima imekuwa ikimsuta kwa yote aliyoyafanya. Akaamua lolote na liwe, lakini kwa mikono yake hata mwaga damu ya mtu mwingine tena lakini lazima atafute njia ya kumficha mtu huyo ikiwa ni Dedan kweli.
***
Kama kuna mtu alifahamu kuwa ndani ya vyumba vya ‘Serenity’ kulikuwa na siri basi alikuwa amekosea. Kuanzia sakafuni mpaka kwenye paa, jengo zima lilikuwa limesheheni vinasa sauti na kamera za ‘CCTV.’ Kwa hiyo kila kitu kilichokuwa kikifanyika na kuongelewa humo ndani, kilikuwa kinasikiwa na kuonwa na Mr. John Chakos aliyekuwa maili mia moja kutoka katika jengo hilo.
Chakos alijua vema yupi kati ya wasichana walioingia humo mjengoni hana ari ya kazi na yupi kwa pesa alizopata kwa kazi hiyo alikuwa radhi kukaa hapo ‘Serenity’ kwa miaka yote ya maisha yake.
Tangu Salima alipoingia ndani ya jengo hilo Mr. John Chakos, alikuwa akimtazama kupitia kompyuta yake. Alimtazama usiku mzima jinsi alivyokuwa amelala, mpaka asubuhi ya siku hiyo mpya. Alishinda akimuangalia Salima alivyokuwa akioga na kuvaa nguo zake na hata akitembea ndani ya korido za jengo hilo.
Nafsi yake ilianza kujaa tamaa ya kufanya mapenzi na msichana huyo.
Itaendelea KESHO
Post a Comment