ad

ad

Kitanzi, Kisu au Bastola - 6



ILIPOISHIA
AKAJITAHIDI kuchokonoa kitasa hicho na mara kikazunguka na kichuma cha loki kikajiachia na kurudi ndani kadiri alivyokuwa akiunyonga msumari huo. Akaufungua mlango na kutoka nje kwa kupita koridoni hadi nje ya nyumba. Njiani akikutana na sura tofauti za watu wengi wakimtazama na kumshangaa kwa jinsi alivyovaa vibaya na jinsi uso wake ulivyomvimba kwa usingizi na njaa. Dedan akakatiza mitaa kama chizi huku akikoswakoswa na magari barabarani.
Shuka nayo…
***
Tangu alipofika asubuhi, alikuwa akitolewa chumba kimoja na kupelekwa chumba kingine. Alishangaa sana alipoingia kwenye chumba kidogo chenye mvuke wenye joto kali kiitwacho ‘Sauna’, aliambiwa mvuke huo humsafisha mtu kuzidi hata maji ya kawaida ambayo tumezoea kuyaoga.
Kisha akapelekwa chumba cha ‘massage’, humo alikandwakandwa na warembo wenye mikono laini utadhani mikono yao haifanyi kazi nyingine yoyote zaidi ya hiyo, kwani kwa jinsi mikono yao ilivyokuwa laini hakuna aliyeonekana kuwa na uwezo wa kushika shoka na kukata kuni au hata kusugua majungu yenye ukoko na masizi.
 Akapelekwa chumba kingine ambacho kwa huduma alizozipata humo alikitambua kama saluni ya kike. Humo alisetiwa nywele na kufanyiwa ‘facial’, ‘manicure’ na ‘pedicure.’
Kwa mambo hayo Salima alijikuta akisahau kabisa kuhusu Dedan ambaye kwa wakati huo alikuwa akitembea toka mtaa mmoja hadi mwingine bila kuelewa mahali alipokuwa akielekea au hatari iliyokuwa ikimkabili.
Wasichana wengi wazuri na warembo walimzunguka kila mmoja akifanya kazi fulani katika mwili wake. Alitumia muda mwingi sana akistaajabu, jinsi gani urembo wa mwanamke ulivyokuwa na gharama! Alishukuru tu kwamba kila kitu kilikuwa kikilipwa na kampuni hiyo aliyoitambua kwa jina la ‘Serenity’ .
Kwa muda wote huo Madam Flaviana alikuwa amekaa pembeni ya Salima akimtazama kana kwamba alizidi kuwa mpya kwa kadiri alivyokuwa akipambwa. Ilisemekana kuwa mwanamke huyo alikuwa na uwezo wa kumpima mtu kwa kumtazama tu na kujua haraka vipimo vyote vya nguo yake, kuanzia ukubwa wa kiuno, urefu, mpaka upana wa mabega.
Inawezekana kabisa Madam Flaviana alikuwa akimtazama Salima kwa lengo hilo, lakini kuna kitu cha ajabu ambacho Salima alihisi baada ya kumtazama jinsi Madam Flaviana  alivyokuwa akimuangalia, lakini alipuuzia na kukaa kimya.
“Salima, unajua kama wewe ni mrembo sana?” alisema Madam Flaviana huku akimwangalia Salima kuanzia chini mpaka juu.
“Mbona mi wa kawaida sana,” Salima alijibu kwa aibu kidogo.
Ukweli ni kwamba Salima hakujali sana urembo kama wasichana wengine kiasi cha kujijua na kujua watu wengine wanamuonaje. Alikuwa msafi na mzuri wa asili asiyependa kuupoteza muda wake mwingi mbele ya kioo, hivyo hakuwa akijifahamu kama ni mzuri kiasi hicho cha kusifiwa na Madam Flaviana, kilicho kuwa akilini mwake wakati huo ni harakati za kutoka kimaisha tu.
“Oke, twende nikakuchagulie nguo,” alisema Madam Flaviana bila kutaka kuendeleza ubishi kwa mtu ambaye haifahamu thamani ya uzuri wake. Alichowaza akilini ni kumtumia kwa manufaa ya kampuni yao haramu. Salima kwao alikuwa ni kama ndege mjinga asiyejua thamani ya mlio wa sauti yake, hilo lilikuwa jambo la kujivunia kwa Madam Flaviana, akapenda abakie hivyohivyo.
Akiwa katika chumba kilicho sheheni nguo mbalimbali, alichaguliwa nguo moja baada ya nyingine na kutakiwa kuzijaribu. Nyingi zilikuwa fupi, zenye kubana. Kila mara alivyotoka kwenye chumba cha kubadilishia nguo na kuvaa nguo nyingine, Madam Flaviana alionekana kumuangalia sana bila kusema chochote zaidi ya kumkabidhi nguo mpya badala ya ile ya mwanzo na kumtaka aendelee kuzijaribu.
Hatimaye zoezi hilo la kuchosha lilimalizika kwa Salima na kuvaa nguo moja iliyombana sana kisha wakaelekea kwenye mgahawa kwa ajili ya chakula cha mchana.
Kila kitu kilikuwa kipya sana kwa Salima, akafundishwa jinsi ya kuketi kistaarabu, jinsi ya kula kwa kutumia uma na kisu, akafundishwa jinsi ya kufungua shampeni na kuzungumza kwa staha na haiba za kike. Yote alionekana kuyashika haraka sana kiasi cha kumfurahisha Madam Flaviana.
“Mama yangu!” Salima alishtuka baada ya kugundua kuwa muda mrefu ulikuwa umepita tangu amuache Dedan peke yake. Akasimama na kutaka kuondoka kama mtu aliyechanganyikiwa.
“Salima nini tatizo?” aliuliza Madam Flaviana baada ya kugundua kubadilika ghafla kwa hali ya Salima.
“Nimemuacha mgonjwa peke yake tangu asubuhi nilipokuja huku, nilipitiwa na kumsahau kabisa, sijui hali yake itakuwaje maana hawezi hata kusimama na kula mwenyewe.”

“Usihofu sana, hii ni saa nane tunaweza kumuwahi kwa gari langu. Twende  haraka,” aliongea Madam Flaviana kisha wote wakaondoka.
SONGA NAYO…
Wasiwasi ulimjaa sana Salima, akaona hata gari lenyewe lilikuwa halikimbii kwa kasi aliyokuwa akiitaka, lakini alijikaza na kuvumilia bila kuteremka. Kimoyomoyo alisali sala zote bila kujali dini wala lugha aliyoitumia ilimradi tu sala hizo ziweze kumfanya Dedan awe mzima mpaka saa atakayofika.
“Usihofu Salima, utamkuta tu akiwa mzima,” alisema Madam Flaviana kwa huruma huku akiuzungusha usukani na kuongeza spidi kila ilipompasa kufanya hivyo.
“Madam, hujui tu Dedan ana umuhimu gani kwangu ndiyo maana unasema kirahisi hivyo,” aliongea Salima huku machozi yakimtoka bila kujua kama alilitaja jina la Dedan kimakosa katika maneno yake aliyoyasema.
“Kwani mgonjwa wako anaitwa Dedan? Mmm...ni nani yako?” Madam Flaviana alimuuliza maswali mfululizo Salima.
“Aahh...ni mpenzi wangu tu,” aliongea Salima kwa kigugumizi baada ya kujishtukia kwamba alilitaja jina la Dedan kimakosa.
“Oooh! pole sana, kwani anaumwa nini?”
Kwa swali hilo Salima akawa kimya akijishauri kumwambia au kutomwambia Madam Flaviana, hata hivyo aliamua kumsimulia ukweli wote kwani kwa hali ilivyokuwa asingeweza kuyazuia maswali kutoka kwa mwanamke huyo kwa wakati huo kwa kuwa alijikoroga mwenyewe kwa kumtaja Dedan mbele yake. Alihisi asingekuwa muungwana kwa kuficha kila kitu mbele ya Madam Flaviana ambaye alijitolea kumpeleka kwa gari lake mpaka nyumbani kwake bila hiyana.
Basi Salima alijikuta akimsimulia Madam Flaviana mwanzo mpaka mwisho kuhusu Dedan na yeye. Akamwambia kila kitu bila kuficha. Akabainisha pia hata dhumuni la kuamua kufanya kazi katika kampuni hiyo, ilikuwa ni kwa ajili ya mpenzi wake aliyekuwa akihitaji tiba na matunzo.
Madam Flaviana alishindwa kulizuia chozi lisimdondoke mara baada ya Salima kuhitimisha simulizi yake kwa kusema alikuwa akimpenda sana Dedan kiasi cha kufanya kitu chochote ili awe naye.
Madam Flaviana alimuonea huruma sana msichana huyo mdogo ambaye maisha hayakuwa mazuri sana kwa upande wake. Akaishia kumwangalia tu moyoni akitamani amuokoe na janga ambalo yeye pamoja na kampuni yake walikuwa wamemwandalia, lakini akasita na kuamua kumuacha tu katika bumbuwazi alilokuwa nalo kwa kuhofia kuwa kama angemwambia angesababisha hata uhai wake yeye mwenyewe kuutia mashakani kwani alimjua vyema Mr. John Chakos. Mwanaume mtanashati sana ambaye ukatili wake ulijificha vyema nyuma ya uzuri wa sura na umbo lake.
Madam Flaviana mwenyewe alikuwa kama mmoja wa wasichana waliokuwa wa kwanza kabisa kuuzwa katika biashara hiyo, ndiyo maana hakukuwa na mtu wakumshangaa kwa nini alikuwa mrembo sana.
Tuseme bahati tu ilikuwa upande wake. Uzuri wake ulimletea mafanikio makubwa na kujuana na watu wengi kutoka nchi mbalimbali. Pengine hiyo ndiyo ilikuwa salama yake kwani kampuni ingepata hasara kubwa kama ingemwachisha kazi baada ya umri wake kumtupa mkono kwa kuhofia kupoteza mtandao wa marafiki na wateja ambao Madam Flaviana aliutengeneza. Kwa kugundua hilo wakampandisha cheo na kuitwa ‘Madam’ ama ‘Bibi Mkuu,’ kazi yake ikiwa ni kuwafunza ustaarabu mabinti wapya na kuhakikisha wanatii sheria na taratibu zote za kazi yao huku akiripoti maendeleo ya kila msichana aliyekuwa akiishi kwenye lile jumba.
Kwa miaka kumi na mbili aliyoishi katika kampuni ya ‘Serenity’ alipata kushuhudia mambo ya kutisha sana yakiwatokea wote ambao walikuwa wakikaidi kanuni za kazi na kutaka kutoa siri za kampuni hiyo nje.
Kwa kifupi hata yeye mwenyewe alishapoteza marafiki wengi sana aliokuwa nao katika jumba la ‘Serenity’.
Hakuna mtu wa nje aliyekuwa akifahamu vizuri nini kilichokuwa kikiendelea ndani ya kuta za jengo hilo ambalo yeye aliliona kama ‘Danguro la kimataifa.’
“Kwa hiyo vipi! Kama Caro atakuja kumfuata bwana ‘ake, wewe utafanyaje?” aliuliza Madam Flaviana huku akikata kona ya kuingia vibarabara vya uswahilini.
“Sipo tayari kumuachia, labda nisiwe hai,”
“Nilishawahi kupenda kama wewe Salima, sishangai hata kido…”
“Ishia hapohapo!” Salima alisema  akimkatiza usemi Madam Flaviana na kushuka haraka akikimbilia moja kwa moja hadi ndani ya nyumba. Macho yake yakakutana na mlango wa chumba chake ukiwa wazi huku kila kitu ndani ya chumba chake kikionekana isipokuwa Dedan.
Itaendelea siku ya kesho.

No comments

Powered by Blogger.