ad

ad

Kitanzi, Kisu au Bastola - 4


 

ILIPOISHIA
SALIMA alishtuka kutoka usingizini baada ya kuhisi alimsikia Dedan akitamka maneno ambayo hakuwa na uhakika nayo.
Akaamka kitandani na kumsikiliza kwa makini kama ni kweli Dedan ndiye aliyekuwa akiyatamka maneno yale. Akagundua kuwa kweli alikuwa yeye. SASA ENDELEA…
Alipomsikia mara ya pili na ya tatu, akagundua moja kwa moja kwamba, Dedan hakuongea maneno yale kwa bahati mbaya. Ni wazi kuwa alianza kurudiwa na kumbukumbu zake. Salima alifurahi kidogo alipomsikia kijana huyo kwa ufasaha zaidi akitamka ‘Caro,’ neno ambalo bila shaka lilikuwa jina la mwanamke.
“Caro!” Salima alistaajabu kimoyomoyo huku akimuangalia Dedan aliyekaza macho akiliangalia pazia lililokuwa likiyumbishwa kila upande na upepo uingiao ndani kupitia dirisha.
Awali, Dedan alikuwa akitamka neno moja tu, “mmm’’ kila alipokuwa akiulizwa swali. Ajabu ni kwamba neno hilo limebadilika ghafla kwa usiku mmoja na kuwa Caro. Kwa wakati huo kila alipokuwa akiulizwa kitu alitamka jina hilo huku machozi yakimtoka hali iliyosababisha Salima ahisi kuna uhusiano mkubwa kati ya Dedan na Caro.
“Labda ni ndugu yake,” aliwaza  kwa wasiwasi huku akishindwa kuzizuia hisia zake kwamba huenda Caro alikuwa ndiye chanzo cha Dedan kuwa katika hali ile na labda ilikuwa bora aendelee kukaa kimya tu asije akayaibua mambo mengi ambayo yalikuwa yametulia.
Salima alitambua kuwa ni lazima afanye utafiti binafsi kuhusu huyo mwanamke Caro. Aliamini lazima kutakuwa kuna kitu kati ya wawili hao.
Akawa kama anakumbuka kitu fulani, akainuka na kulivuta sanduku moja kutoka chini ya uvungu wa kitanda akafungua zipu yake na kulitazama ndani. Aliviweka pembeni vyeti na picha za Dedan na kupekuapekua kila upande akilenga kutafuta kiashiria chochote kuhusu namna gani Caro na Dedan walikuwa wakifahamiana.
Alitafuta mpaka akachoka, hakukuwa na cheti wala karatasi iliyokuwa na jina la Caro. Alitazama kila mahali akijitahidi kukumbuka kama kuna kitu cha Dedan alikiweka mahali pengine zaidi ya hapo, kwani tangu wahamie hapo alihakikisha kukitunza kila kitu cha Dedan bila ya kuvifungua ili kama mwenyewe atapona ampatie vitu vyake vikiwa salama.
Kwa wasiwasi aliokuwa nao alikubali kwa siku hiyo kuivunja kanuni aliyojiwekea na kupekua vitu vya Dedan bila ya ruhusa yake. Akainama na kulivuta furushi jingine. Ndani yake akatoa chaja, vifaa vya umeme, simu mbovu na nzima, vyote vikiwa ni vifaa vya dukani kwa Dedan.
 Alipoziona simu ndipo akaikumbuka simu ya Dedan ambayo wala hakuwahi kuifikiria kwa muda wa takriban miezi mitatu tangu Dedan alipoanza kuumwa. Akaiwasha na kushusha pumzi akisubiri utitiri wa meseji uanze kuingia.
***
Side alikuwa akimfuatilia kwa karibu sana msichana huyo aliyekuwa adimu sana kuonekana mitaani, alihakikisha anaijua vema nyumba aliyokuwa akiishi. Alipomwona akiingia chumba kimoja kati ya vile vya mkono wa kulia, akatabasamu na kuingia ndani ya gari lake aina ya Toyota Hilux na kuondoka eneo lile.
Huku akiendesha gari, Side aliipokea simu yake iliyokuwa inaita na kuiweka loudspeaker.
“Vipi? “ sauti nzito ilisikika kutoka kwenye simu.
“Bro, nimeshapajua anapokaa,” Side alijibu huku akitabasamu kana kwamba alikuwa amefanikisha jambo muhimu sana.
“Kweli?”
 “Huamini kesho nikupeleke?”
“Duh! Kweli dogo we ni noma aisee, njoo basi haraka unipe fulu stori.”
“Nipo njiani nakuja usiende sehemu yoyote kaka,” aliongea Side huku mikono yake ikiwa bize na kuzungusha usukani wa gari akikwepa vidimbwi vilivyojazana katikati ya barabara.
***
Baada ya muda, simu ya Dedan iliunguruma mara mbili kuashiria meseji mpya imeingia. Akatulia kimya asiifungue akitaka meseji zote ziingie kwanza ili aanze kuzisoma taratibu.
Alihesabu moja mpaka ishirini haikuingia meseji nyingine, akaamua kufungua na kuisoma. Cha ajabu haikuwa na jina la mtumaji na ilikuwa fupi sana isiyoonesha hali, dhamira wala jinsia ya mtumaji. Iliandikwa tarakimu ‘90’.
Salima aliisoma mara nyingi bila kuijua maana yake kiundani, akaipuuza na kuanza kuzisoma meseji nyingine zilizokuwepo ndani ya simu hiyo tangu awali. Akagundua meseji nyingi zilitumwa kwa namba ileile iliyotuma meseji muda ule. Akiwa haamini alichokigundua ghafla simu yake ikaanza kuita, alipoiangalia aliona namba ile
aliyotumiwa ujumbe.
Ilikuwa kama vile mpigaji alikuwa akiiangalia simu yake muda wote, maana kama isingekuwa hivyo angewezaje kujua kama ujumbe wake umefika kwa mtu aliyemtumia?
Salima alikuwa makini, alitafakari kwanza kabla ya kuipokea simu ile kwa vile ndiyo kwanza alikuwa ameanza kuzisoma meseji zilizokuwa zimejazana kwenye simu ya Dedan.
Aliamini kwamba ni vyema kama angejua kwanza jambo lolote kuhusu mpigaji simu huyo kabla hajaipokea na kuongea naye akihofia asije akajianika yeye na Dedan wake kwa watu wabaya ambao huenda kwa njia moja ama nyingine walishiriki kumfanya jamaa yake huyo kuwa katika hali ile.
Kwanza alimtazama mgonjwa wake ambaye alikuwa ameshaanza kusinzia kwa uchovu wa chai na mihogo ya kukaanga aliyokuwa amemlisha, kisha akaipokea ile simu na kusikilizia sauti ya mpigaji.
“Haloo!” sauti ya kike ilisikika…
“Halo Dedan!” mpigaji aliendelea kuita huku Salima akiwa amejikausha.
“Haloo, mimi ni Carolina. Najua nimekuumiza sana kwa yote niliyokufanyia, tafadhali naomba unisamehe mpenzi wangu, haikuwa dhamiri yangu kukuumiza. Please Dedan naomba unijibu basi,” aliongea msichana huyo kwa huzuni huku kwikwi na kilio vikisikika kwa mbali.
Baada ya kulisikia jina la Caro, Salima akahisi kama vile alikuwa akitaka kupasuka kwa jinsi alivyovimba kwa hasira. Ule uchizi na jazba alizokuwa nazo zamani zilianza kumpanda kichwani na kujikuta akishindwa kujizuia kwa ghadhabu alizokuwa nazo.
Msichana huyo akasonya na kukata simu kwa kuizima kabisa huku mishipa ya damu ikiwa imemsimama kichwani.
“Hakuwepo wakati unaumwa, leo anajifanya anakupigia simu akiomba msamaha. Kama yeye mwanamke kweli tutaona kama atakupata. Eti oooh! Mimi Carolina mpenzi wako, anajua nimekugharamia vingapi? Mbona hakujitokeza siku zote hizo. Anachezea moto, we muache tu!” Salima aliongea kana kwamba alikuwa akimwambia Dedan badala ya Carolina mwenyewe.
Kipindi chote hicho Dedan alikuwa amelala, lakini alipolisikia jina la Carolina likitajwa na Salima akashtuka na kukaa kitandani akimkazia macho bila kuyafumba huku akihema kwa kasi kama amekutana na jinamizi.
Salima aliogopa kumuona Dedan katika hali ile, akamfuata na kumbembeleza taratibu hatimaye akalala tena kitandani. Salima alishindwa kujizuia kustaajabu jinsi Caro alivyouteka moyo wa Dedan, yaani hata katika hali ile ya kutojielewa, lakini alimkumbuka vizuri kiasi cha kumtajataja kila mara.
***
Ilipofika saa tano juu ya alama, Side alikuwa tayari ameshafika kwa John Chakos kumpa kila kitu alichokuwa akikifuatilia asubuhi na mapema ya siku hiyo.
Ndani ya chumba kizuri katika Hoteli ya Toptown Wild Wind mwanaume mrefu mwenye rangi ya kitasha alitokea kutoka maliwatoni akiimba kwa mikogo huku akiwa na kitaulo tu.
Alimtazama Side aliyekuwa amekaa kwenye sofa bila wasiwasi akiitazama sehemu ya jiji zima la Dar kupitia dirisha kubwa la kioo kwa mwonekano wa juu. Ilikuwa ni ghorofa ya kumi na saba.
Mtu yeyote anayepanga vyumba vya hoteli hiyo kwa vyovyote vile huwa na utajiri wa mabilioni ya fedha kiasi kwamba haimuumi kulipa laki sita kwa siku moja kama gharama ya kukaa hotelini hapo.
Japo Side ni mtoto wa mjini kiasi cha kulijua vyema Jiji la Dar na vichochoro vyake, lakini siku hiyo alikubali kutolewa ushamba kwa kuingia katika hoteli yenye hadhi kama hiyo.
John  Chakos ni mmoja kati ya matajiri wachache walionufaika kwa  kuwatumia wasichana wachache wa tabaka la chini kwa biashara ya ngono. Kwa mujibu wa uchunguzi wake, Side alibaini kuwa wasichana wachache walioonekana warembo, hupangiwa kulala na wageni mbalimbali wa kiume wajao nchini kwa malipo ya kiasi fulani cha fedha.
Kwa donge nono, Side alipewa kazi ya kuhakikisha kila mara alikuwa akiwatafuta wasichana hao kutoka mitaani. Alianza kazi yake taratibu na sasa amekuwa mzoefu na mwenye mafanikio makubwa.
Alikuwa akipiga picha za wasichana kadhaa na kuzinadi kwa bosi wake, ikiwa picha ya mrembo mmoja ilikubaliwa basi lilikuwa ni jukumu lake kumfuatilia na kumpeleka kwa bosi wake kwa kumlaghai kwa pesa kidogo.
Siku hiyo Side alikuwa amekwenda kukabidhi ripoti ya uchunguzi wake wa awali kuhusu mmoja wa wasichana warembo aliyekuwa akimfuatilia kwa muda mrefu. Tofauti na wasichana wengine ambao Side alikuwa akiwapeleka kwa bosi wake, msichana huyo alionekana kuzitawala fikra za bosi wake, Mr. John Chakos. Alimuulizia kila mara na kumtaka aharakishe kukamilisha ripoti yake na kumpelekea chumbani mwake tofauti na utaratibu wa kawaida.
Kiasi fulani machale
yalimcheza Side na kuanza kuhofia juu ya hatima ya msichana huyo aitwaye Salima Rajab.

Itaendelea siku ya kesho.

No comments

Powered by Blogger.