ad

ad

Kitanzi, Kisu au Bastola - 01 & 2





Kitanzi, Kisu au Bastola -01
ANATEMBEA akiwa anapepesuka kwa ulevi uliomjaa kichwani. Amelewa chakaliii, pombe zikimdanganya na kumfanya asiwe na hofu hata kidogo kukatiza kona hatari za mitaa ya Songasonga.
Laiti kama angekuwa na akili zake timamu asingediriki hata kuwaza kupita peke yake usiku huo kwa kuwa anazijua vema sifa za mtaa wake.
Roba za mbao, ubakaji na mara nyingine kesi za mauaji ndiyo mambo makubwa yanayozifanya hata serikali za mitaa na wilaya ziuangalie kwa jicho la tatu pekee mtaa huo. Lakini usiku wa leo, saa nane hiyo, Dedan Magesa anapita bila wasiwasi wowote,  mkononi akiwa amekumbatia kopo la pombe ya kienyeji maarufu kama mataputapu.
“Muuuvu bichii geliatu weiii. Muuuvu bichii geliatu weiii,” alijiimbia wimbo wake aliokuwa akiurudiarudia kiitikio tu tena kwa sauti mbaya ya kilevi kinachotia kichefuchefu hata kukisikiliza.
Taratibu Magesa aliyoyoma akipita karibu kabisa na kona na vichochoro kadhaa vyenye sifa mbaya sana za uhalifu. Kama vile mkono wa Mungu ulikuwa juu yake siku hiyo, alifika nyumbani salama salimini. Akafungua na kufunga mlango wa chumba chake kwa umakini mkubwa kisha akajitupa kitandani kwa nguvu na kulala fofofo  akiwa na viatu na nguo zake zote. Kwa mbali kabisa,  moyo wake ulilia na kuomboleza.
“Uko wapi mpenzi wangu, kwa nini umeniacha peke yangu leo? Ina maana hukunipenda hata kidogo kiasi cha kuamua kunifanyia hivi?
“Najua sitampata msichana mwingine mzuri kama wewe...Ooh Carolina! Nini nimefanya hadi kustahili adhabu hii?”

***
Asubuhi iliyofuata, Dedan aliamka kama kawaida yake na kufungua ofisi yake, kibanda kidogo pembezoni mwa nyumba kubwa aliyopanga, akiuza vifaa vya simu, kuchajisha simu, kutengeneza na kuingiza nyimbo kwenye simu kwa kutumia kompyuta.
Kwa maisha ya kujinyima na kutopenda starehe, kazi yake hii ilimnufaisha kiasi cha angalau kujikimu kimaisha na pengine kumfanya hata asiwaze kabisa kufikiria kufanya kazi nyingine yoyote.
Tofauti na siku nyingine, siku hiyo ilianza vizuri sana kwa upande wake,  alipata wateja wengi kupita kiasi. Kama mjasiriamali mwingine mzoefu, alifanya kazi zake kwa umakini mkubwa na kuhakikisha wateja wake wanavutiwa na huduma zake kwa kuongeza ukarimu na kuongea lugha yenye bashasha na hata ikamlazimu kuwajua na kuwaita kwa majina wateja wake ambao walijipanga kwa michapo ya hapa na pale huku akiendelea kuwahudumia.
Hakika mtu yeyote alijisikia huru kukaa kwenye benchi dogo lililopo pembeni ya kibanda cha Dedan,  akipiga soga na kupoteza muda, akinywa kahawa au pengine akijiunga na kikundi cha vijana wachache kwenye vikao visivyo rasmi wakibadilishana mawazo ya siku.
Ndiyo, kila mtu hulalamikia ugumu wa maisha wa siku hizi, kiasi cha furaha au jambo jema kutokea kwa nadra sana na pengine lisitokee kabisa hata kufikia mtu kukushirikisha walau punje ya neema yake.
Umasikini ulisababisha kila mtu ajifungie peke yake kwa uchoyo akila matunda ya kazi zake. Hivyo, iwe asubuhi,  mchana au jioni, wakazi wa Mtaa wa Songasonga hukutana kwa unyonge si kwa jambo lingine, bali kuzungumzia mawazo dhaifu ya siasa za kupindua nchi na mara nyingine wakisimuliana hadithi za nani kafanya nini, lini na wapi!
Kwa kifupi Dedan alikuwa ndiyo kitovu cha mkusanyiko wa watu katika mtaa mzima wa Songasonga. Kwa sababu hiyo na sifa nyingine kedekede, alitokea kupendwa na kila rika kiasi cha kujulikana vizuri na kila mtu mtaani kwake.
Japokuwa alionekana mwenye furaha kubwa machoni mwa watu siku hiyo, ndani ya moyo wake kwa  kificho alikuwa amebeba maumivu makali kiasi kwamba kama hali hiyo ingemkuta mtu mwingine kwa hakika asingekuwa hata na nguvu ya kusimama na kuongea kwa furaha mbele za watu.
Siku zote Dedan aliamini katika kuyamaliza matatizo yake yeye mwenyewe bila kuathiri mwenendo wa shughuli zake au wa watu wengine. Akaamua kutowashirikisha kabisa ndugu wala marafiki zake majonzi na matatizo yake. Mara nyingine aliweza hata kulala na njaa bila kusema wala kuomba msaada kwa mtu yeyote.
Huenda misimamo hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomfanya ajikaushe muda wote huo, akiigiza kucheka na watu hali moyoni akilia kwa sauti akimuwaza mpenzi wake, hapana, aliyekuwa mpenzi wake, zamani
“...ooh! Carolina,  maisha gani nitaishi bila wewe? Naumia…naumia, ee… Mungu naomba nirudishie Caro wangu.”
Tenzi  zilipokwamia hapo alitamani kupiga kelele na kulia kwa nguvu. Huenda angepunguza maumivu walau kwa kiasi kidogo, si ndiyo wanavyosema hao wanaojiita wanasaikolojia, eti kulia kunapunguza msongo wa huzuni na kulainisha mrundikano wa dukuduku lililofungamana rohoni. Waongo wakubwa!
Kinyume na wote hao yeye aliamini kulia si punguzo wala suluhisho la matatizo yake, hasahasa tatizo la mapenzi. Alihakikisha kwamba hatoi mwanya wa hata chozi moja kumdondoka wala kumlengalenga kutoka machoni mwake. Mwanaume rijali hamlilii demu bwana!

Kitanzi, Kisu Au Bastola-2

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
TARATIBU zimwi la upweke likamzonga na kuushinda kirahisi ustahimilivu wa moyo wa Dedan. Kama mfungwa kwa mawazo yake akajikuta hajielewi kabisa. Kichwani akiwaza mara ya kwanza alipoongea na Caro kwa njia ya simu…
ENDELEA SASA...
“Mungu wangu! Msichana mrembo wa ajabu huyu,” alisema moyoni Dedan. Akakumbuka pia alipoamua kumfungulia kurasa mpya za mapenzi ndani ya kuta za moyo wake.
Alikumbuka vyema kila zuri walilofanya pamoja, wakicheza baharini na kurushiana mito kitandani. Walilishana chakula na kubusiana kimahaba.
Lakini hayo yote yalitoweka ghafla baada ya kukumbuka sauti kali ya Carolina kwenye simu ikimtosa bila huruma na pasipokuwa na sababu yoyote. Akasikia sauti nyingine ya mwanaume wake wa sasa ikimchimba mkwara kwamba atakiona cha mtemakuni endapo atajipendekeza kwa hali yoyote ile kumtafuta Carolina.
“Hapana,” alijishtukia akiweweseka kwa sauti ya ukali mbele ya mteja wake mkubwa, Salima ambaye muda mwingine alikuwa akimsemesha huku akimkabidhi simu yake ya mkononi kwa ombi la huduma ya kuchajisha lakini bila mafanikio.
“Ooh! Samahani sana Salima, ulikuwa unasema nini?” Dedan aligutuka kutoka katika vita ya nafsi na kushusha pumzi ndefu akimwomba Salima arejee maongezi yake ya awali.
“Dedan, mzima kweli leo wewe?” Salima aliuliza baada ya kugundua hali ya kubabaika ya Dedan.
“Mi mzima tu...lete stori,” kwa uchangamfu Dedan aliongea kiasi cha kumshawishi Salima aamini kwamba kila kitu kilikuwa sawasawa.
“Hata hivyo, siku zote ni nzuri kwa Dedan, ni kama anaishi katika ulimwengu wa pekee, japo ni maskini mwenzangu, anaonekana haumizwi na kitu. Shida hizi anazichukulia kama changamoto kwa kupigana kwa nguvu zake zote kupata maendeleo tofauti na vijana wengi wa rika lake.
“Kweli ninatamani  sana niwe na mwanaume kama huyu. Hapana si kama, bali ni huyu huyu…Mh! Lakini namwogopa kumuanza, sijui atanichukuliaje? Mtu mwenyewe ni mwingi wa shughuli! Ila nitamwambia kesho asubuhi nikija kuchukua simu yangu.
“Nitamtumia meseji nzuri ya mapenzi. Nimejaribu kumfanyia mambo mengi ilimradi azisome hisia zangu, lakini mtu mwenyewe wala haoni,” aliwaza Salima huku akiwa amesimama na kujichekesha na kuweka tabasamu pana mbele ya Dedan aliyekuwa akimtazama tu bila kuona chochote.
Mawazo yake yalikuwa mbali, kama vile ana macho lakini haoni na ana masikio lakini hasikii.
“Usiku mwema Dedan,” aliongea Salima kwa huruma na upole baada ya kugundua ameshindwa kulinasa windo lake kwa siku hiyo.
Mbinu alizofundishwa na kungwi wake, Bi. Hamdani wa Masasi hazikufua dafu mbele ya Dedan.
Alitamani amrukie na kumbusu kwa nguvu ili amjulishe hisia zake, lakini alihofia akiamini ataonekana msichana malaya kama si aliyekosa maadili mema.
“Nitasubiri nafasi yangu, sitaki niharibu yote niliyoyaanza. Kwa Dedan nitakuwa mwanamke mstaarabu, mwema na mwaminifu daima naamini atanipenda tu,” alijiapiza na kujiondokea zake moyoni akilia na kumlaumu mwanaume huyo kwa kutojua windo lake.
“Usiku mwema Dedan…usiku mwema mpenzi wangu...” chochote asichokisema kwa sauti kumwambia Dedan moja kwa moja, aliamua kukimalizia kwa kuongea kwa sauti ndogo akitumaini ipo siku atamjibu na kumuuliza mambo mengi  wakiwa kama mke na mume.
Baada ya kuhakikisha amemaliza na kuweka vizuri kila kitu, Dedan aliitazama saa juu ya kioo cha simu yake iliyoonesha namba ishirini na moja, ikiashiria saa tatu usiku kwa urekebisho wa saa ishirini na nne za siku moja.
Alifunga vyema ofisi yake kisha akatokomea huko vichochoroni ambako aliwahi kusikia vinauzwa hivyo vinavyopoteza mawazo, eti pombe!
“Hakuna muda mzuri wa kuamua kuwa chakari kama huu,” Dedan alijisukuma kwa mara ya kwanza kwenye vilabu vya pombe za kienyeji.
Aliamini atalewa kwa gharama ndogo sana huku akifanikiwa angalau kuvuka makali ya upweke kwa usiku huo wa kwanza akilala akiwa anajua kabisa hataishi na Caro wake tena.
***
Asubuhi aliamka na kujinyoosha na kupiga miayo mfululizo. Alionekana mwingi wa uchovu kutokana na pombe kali za jana yake. Ghafla alijishangaa machozi yakimbubujika.  Alitaka kuamka, lakini akashindwa. Jasho jingi lilimtoka mwilini huku mapigo ya moyo yakienda kwa kasi ya ajabu. Kama mzigo alidondoka chini na kupoteza fahamu.
Itaendelea Siku ya kesho.

No comments

Powered by Blogger.