NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 19 NA NI MWISHOO

ILIPOISHIA...
NILIJIULIZA kitu gani tena hicho shoga yangu anataka kuniambia ambacho kilionekana kumsumbua moyoni mwake.
Kila nilipomuuliza alichotaka kuniambia alisema nivute subira.
“Shoga mbona unanipa mtihani.”
“Najua nitakuchanganya lakini ni jambo la heri.”
“Jambo gani si unidokeze hata kidogo.”
“Ikifika siku nitakueleza,” Ilham bado alifanya siri.
SASA ENDELEA...
KWA kweli nilikuwa na maswali mengi juu ya kitu alichotaka kunieleza na kuniomba nikubali.
Wazo langu lilikimbilia kwenye ndoa nikahisi labda kuna mtu amevutiwa na mimi na amemwambia kuwa aniambie ili anioe.
Kauli ile ilinifanya niongeze umakini japokuwa nilikuwa nakisia bila kuwa na uhakika.
Ilionesha mtu anayenitaka huenda anafuatilia nyendo zangu kupata uhakika na kile alichokuwa akikiona kwangu.
Niliamini tabia ya utulivu ilikuwa tabia yangu ya asili na hasa baada ya kufiwa sikuwa na wazo la kuwa na mwanaume tena.
Niliamini kuwa baada ya matatizo nilikongoroka mwili na hakuna hata mtu mmoja aliyenitazama kwa jicho la matamanio.
Baada ya kutuliza akili huku nikifuatilia mawaidha ya masheikh mbalimbali yaliyotuelezea masahibu yaliyowakuta maswahaba enzi ya Mtume Muhammad (SAW), matatizo yangu niliyaona madogo na kuendelea kumuomba Mungu anipe faraja ya duniani na ahera.
Siku zote nilisali swala za usiku na kufunga suna ili kumuomba Mungu katika hilo ninaloliwaza kama kweli basi nipate mume mwema mwenye kumjua Mungu.
Siku moja nikiwa nimekaa kitandani kabla ya kulala mlango uligongwa, sikunyanyuka nilimuuliza mgongaji nikiwa bado nimekaa palepale kitandani.
“Nani?”
“Mimi,” ilikuwa sauti ya Ilham.
Nilinyanyuka hadi mlangoni na kuufungua mlango.
“Karibu.”
“Asante, ushalala?”
“Wala, nilikuwa nimejiegemeza nikiwaza ya dunia kabla ya kulala.”
“Basi samahani kwa kukukatisha mawazo yako,” Ilham aliniomba radhi.
“Mbona kawaida, karibu.”
“Asante,” Ilham aliitikia huku akisogea na kukaa kitandani.
Kwa ujaji ule nilijua kuna kitu, nami nilikaa pembeni yake kusubiri kusikia kilichomleta chumbani kwangu usiku ule.
“Salha,” aliniita bila kunitazama.
“Abee dada.”
“Kuna kitu nataka nikuambie, najua utashangaa lakini naomba unikubalie.”
“Kitu! Kitu gani dada yangu?” Nilishtuka.
“Huwezi kuamini nimejigeuza mshenga wa pande mbili, kwa muoaji na muolewaji.”
“Una maana gani?” Mawazo yangu yalikuwa sahihi kuna mwanaume anataka kunioa.
“Salha huwezi kuamini tabia yako imenigeuza sana kimaisha, umekuwa mwanamke tofauti na wanawake wengi. Kutokana na matatizo uliyokumbana nayo yangeweza kukuyumbisha na kuishi maisha mengine, lakini siku zote umekuwa mtu wa msimamo.
“Huwezi kuamini tangu nilipokuwa na wewe niligundua nini thamani ya mwanamke na faida ya msimamo.”
“Umekuwa siku zote ukiamini kile unachokijua, pia kutokuwa na tamaa kama wanawake wengine wanapopatwa matatizo hukimbilia kujidhalilisha.
“Kabla ya kukutana na wewe siwezi kukuficha nilikuwa na mabwana nisiowajua idadi yake hiyo ilitokana na kazi niliyokuwa nikiifanya. Kazi ya baa na ugumu wa maisha ni hatari kubwa sana kwetu wanawake. Mshahara mdogo na lazima umkubali bwana yeyote atakayekuja mbele yako ili kupunguza makali ya maisha.
“Salha ndugu yangu, sikupenda ila hali ndiyo ilinifanya niwe vile, ukimkataa bwana utakula mawe?
“Hivyo kila aliyekuja mbele yangu alikuwa ni halali yangu, hatari kubwa ilikuwa katika ugonjwa wa ukimwi kutokana na wanaume wengine niliokutana nao kutotaka kutotumia kinga. Unajijua kabisa kwamba unakikimbilia kifo lakini utafanyaje, kwa vile njaa ndiyo inayonisukuma kukuubali kuchezea umeme kwa mikono, namshukuru Mungu mpaka nakutana na wewe nilikuwa salama.
“Nina imani mwanzo tulipokutana nilikueleza historia yangu kwa kifupi japokuwa kuna mengi nilikuficha, hata kupatikana kwa mwanangu aliyekosa baba kulitokana na kutembea na wanaume bila mpangilio.
“Kuja kwako kulikuwa kama ukombozi kwangu, kwa muda niliokaa na wewe nilijifunza vitu vingi vikiwemo mavazi ya heshima, tabia na msimamo. Baada ya kufuata nyenzo zako niliweza kuonekana mbele za watu hata kumpata mume niliyenaye leo.
“Pia ulikuwa na moyo wa huruma na mtu mwenye maono ya mbali japo moyo wako tayari ulikuwa umekata tamaa. Kila lililokupata moyoni mwangu maumivu yalikuwa mara mbili. Sikuwa na kitu lakini nilimuomba Mungu usiku na mchana akuepushe na matatizo huku nikumuomba amfungulie mume wangu riziki ili niweze kukulea rafiki yangu.
“Kwa kweli Mungu alisikiliza kilio changu na wakati wa matatizo yako nilikuwa angalau na kitu cha kuweza kukusaidia. Salha umeyabadili maisha yangu, bila wewe sijui ningekuwa wapi sasa hivi kama sio kudhalilika mbele ya wanaume wapenda ngono.
“Ulichokuwa nacho wakati Mungu kakupa neema ulikitoa bila ajizi, wakati wa neema niliringa na kuamini nina sehemu ya kukimbilia na nilipofika ulinitatulia mara moja.
“Matatizo yangu uliyapokea kama yako na kuhakikisha navuka salama wakati wa matatizo. Salha umeijenga nyumba yangu kwa mikono yako umekuwa mshauri katika lililokosa jibu kwangu na leo hii nimesimama mwenyewe. Matatizo ni sehemu ya maisha, najua kiasi gani ulivyoumizwa na msululu wa matatizo yenye historia ndefu isiyotakiwa kurudiwa.
“Namshukuru Mungu kukuondolea mawazo mabaya na kuweza kumkimbilia yeye kwa kila jambo. Nashukuru pia bado umeendelea kuwa mwalimu wangu mwema hata katika mambo ya dini. Baada ya kuwaza yote yaliyopita kuna kitu kilinijia, siamini ni wazo langu bali kama ufunuo ambao kila siku umeniumiza akili yangu.
“Kama nilivyokueleza Salha, una sifa ya kuwa mwanamke wa mfano, pia unafaa kuwa mke wa mtu mwenye kujua nini thamani ya mwanamke mstaarabu. Kabla ya kukueleza nilichokikusudia siku ya leo naomba uniambie ukweli, maisha ya hapa unayaonaje?” Ilham aliniuliza swali akiwa ananitazama usoni.
“Kwa kweli nimeishi na watu wengi lakini mliyonitendea wewe na mumeo ni Mungu pekee wa kuwalipa. Umekuwa nguzo yangu imara iliyopigana usiku kucha kunisimamisha. Nilishakata tamaa lakini ulijitoa kwangu kwa hali na mali kuhakikisha sipotei ndugu yako. Sina cha kuwalipa ila Mungu pekee atawalipa,” nilijikuta nikisema kwa uchungu mpaka machozi yakanitoka.
“Unamuonaje shemeji yako?”
“Kumuona kivipi?” sikumuelewa kidogo.
“Maisha ninayoishi naye.”
“Maisha mnayoishi yananikumbusha jinsi marehemu mama yangu alivyoishi na baba japo mama yangu hakuuthamini upendo wa baba na kuamua kuwa mwingi wa habari. Tofauti ya baba na mumeo ni ndogo, baba hakuwa na moyo wa huruma, lakini mumeo ana moyo wa huruma. Kwa kweli maisha mnayoishi ndiyo wanayotakiwa kuishi wanandoa.”
“Nashukuru kuliona hilo, nina imani hata wewe unatamani kuishi maisha kama haya?”
“Ni kweli, kila mwanadamu hupenda kuishi kwa maelewano na masikilizano na mwenzake.”
“Vizuri, sasa ni hivi naomba unisikilize kwa makini.”
“Nipo makini dada,” nilimjibu huku nikimtazama usoni.
“Katika maisha yangu sijawahi kumuona kiumbe kama wewe, mtu ambaye kila kukicha humuomba Mungu anipe moyo na tabia zako. Japo nitakachokueleza utaona kama utani lakini amini ni kitu cha kweli kabisa,” Ilham alitulia na kumeza mate kisha aliendelea.
“Miezi minne iliyopita nilikutazama sana na kupata maswali ambayo yalinisumbua sana kupata jibu. Nilimuomba Mungu anipe jibu la maswali yangu, nilitamani sana kukaa na wewe na tutenganishwe na kifo. Lakini nilipata ugumu. Je, akitokea mtu anataka kukuoa itakuwaje?
“Wakati nikijiuliza vile, siku hiyo mume wangu aliniletea taarifa kuwa rafiki yake kipenzi amevutiwa na wewe anataka kukuoa, bila hata kujiuliza nilimjibu kuwa tayari una mchumba,” majibu ya Ilham yalinishtua na kujiuliza nina mchumba? Mbona huyo mchumba mimi simjui?
“Najua utashangaa kusema una mchumba usiyemjua, ni kweli nilimjibu kwa vile bado sikutaka tutengane japo hukuwa na mchumba yeyote. Baada ya jibu lile alishukuru Mungu na kusema haikuwa riziki ya rafiki yake na kuongeza chumvi kwenye kidonda cha moyoni mwangu kwa kusema kuwa atakayekuoa hakika atapata mwanamke wa kweli.
“Baada ya kuachana naye nilibakia na siri iliyoutesa moyo wangu, nitawezaje kuwa na wewe kwa kipindi kirefu? Siku moja nikiwa nimelala usiku niliota ndoto moja kuwa wewe ni mke mwenzangu tunayeelewana sana. Nilishtuka usingizini nilitawadha na kuswali rakaa mbili na kumuomba mwenyezi Mungu njozi ile iwe ya heri.
“Baada ya hapo ilipita tena wiki nikilifanyia kazi suala la ukewenza kwa kuulizia kwa mashehe hata kwa wanawake walioolewa ukewenza. Wapo walioukataa kwa kusema ukewenza ni vita ya ndani. Lakini wapo walionieleza ukewenza ni mzuri hasa mkiwa na mioyo ya kumuogopa mwenyezi Mungu na kupendana kama ndugu.
Itaendelea Risasi Jumatano.
Kitabu cha Nililala na Maiti ili Niolewe kipo mtaani, pata nakala yako kwa Tshs 3000.
“Baada ya kuridhika na upembuzi wangu, nilikaa na mume wangu na kumueleza uamuzi wangu wa kutaka wewe uwe mke mwenzangu.”
Moyo ulinipiga pa! Nilishika mikono kifuani na kusema:
“Ha! Ilham!”
“Tulia basi, unisikilize sijamaliza mbona unashtuka?”
“Haya dada.”
“Nilipomueleza mume wangu naye alishtuka na kuniulizia kuhusu yule mchumba wako kaishia wapi.
“Nilimueleza kama nilivyokueleza juu ya kutaka kukaa na wewe siku zote za maisha yangu.
“Nilimpa sababu zilizoshiba na akaniuliza kama utakubali? Nilimweleza kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu utakubali. Basi shoga ombi langu kwa usiku huu ni hilo, nakuomba ukubali tuolewe pamoja ili tuuendeleze udugu wetu.”
Kabla ya kujibu nilishusha pumzi nzito na kutulia kwa muda huku nikilifanyia kazi ombi lake.
Katika maisha yangu sikuwaza kumuudhi Ilham hata siku moja. Kwa kuwa niliamini ukewenza unaweza kuwa chanzo cha uadui na kufikia hatua ya mimi na yeye kuwa chui na paka.
“Dada nimekusikia, lakini naogopa udugu wetu utakuja kugeuka kuwa uadui, sipendi kukuudhi, wewe ni mtu muhimu sana kwangu,” nilimjibu kwa upole.
“Salha mpaka nalitamka hili mbele yako tayari nimeshalifanyia kazi kubwa na nakuhakikishia, moyo wangu hautakuwa radhi kukufanyia kitu chochote kibaya na kama itatokea hivyo, basi Mungu siku hiyohiyo anigeuze kuwa mbwa au nguruwe.”
“Dada mbona umefika mbali.”
“Siyo mbali, nakupenda sana Salha.”
Sikuwa na pingamizi, nilimkubalia baada ya kufikisha majibu kwa mumewe mipango ya ndoa ilipangwa na nikaolewa na bwana Swamadu na kuwa mkemwenza wa shoga yangu kipenzi Ilham.
Nashukuru maisha yetu Mungu ametuangazia kwani upendo umetawala kwa kuwa tumemtanguliza Mungu kwa kila jambo.
Sasa hivi nina watoto wawili kwa mzao mmoja uliokuwa wa mapacha na mzao mmoja mwingine mtoto hakuwa riziki kwani alifariki akiwa na miezi sita.
Namshukuru Mungu nami leo nacheka na kusahau yote, ambayo nimekuwa nikiyazungumza yamebakia kama historia.
Mimi na mke mwenzangu tunaishi kama ndugu wa tumbo moja, lake langu na langu lake.
Japokuwa maisha yanaendelea lakini huu ndiyo mwisho wa simulizi hii ambayo najua imekuliza na kukuumiza moyoni.
Lakini yote kwa yote namshukuru Mungu kwa yaliyotokea kwa imani yangu yote ni mipango yake. Nachukua fursa hii kuwashukuru wote waliosafiri pamoja nami tangu mwanzo wa simulizi hii mpaka leo imefika mwisho.
Simulizi hii ni moja na mitihani tunayokutana nayo wanadamu na kufikia hatua ya kuamini dunia tunayoishi huenda siyo yetu na kuona tunaishi dunia ya peke yetu. Nakuombeni wote mnaokutwa na matatizo mrudieni Mungu bila kuchoka kwa vile neema zake hazina siku wala saa,msikate tamaa kwani hakuna mwingine ila Allah, muombe atakupa.
Nakutakieni maisha marefu yenye furaha na wenye matatizo Mungu awaepushie.
MWISHO.
Post a Comment