ad

ad

YANGA GONGA GONGA, ZANZIBAR


Wachezaji wa Yanga wakishangilia ushindi.
Na Sweetbert Lukonge, Unguja
TIMU ya Yanga imeendeleza ubabe kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kupata ushindi wa pili kwa kuifunga Polisi Zanzibar mabao 4-0, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.


Katika mechi ya kwanza Yanga ilipata ushindi kama huo wa mabao 4-0 yakifungwa na Simon Msuva aliyepiga hat trick na Mliberia, Kpah Sherman.Kwa ushindi huo Yanga itakuwa inaongoza kwenye kundi lake ambalo kuna timu za Shaba, Taifa Jang’ombe, Polisi Zanzibar na Yanga yenyewe.

Katika mechi ya jana Mbrazili, Andrey Coutinho ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao kwa kufunga katika dakika ya 27 kisha Sherman akaongeza la pili katika dakika ya 33.
Kutokana na mashambulizi ya kila wakati kwenye goli la Polisi Zanzibar, mabeki wao walianza kucheza rafu na kusababisha Abdallah Hassani na Frank Ikobela kupewa kadi za njano katika dakika ya 42 na 43.
 

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm alifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kumtoa Nizar Khalfani na kuingia Hassani Dilunga ambaye alichangia kuongeza kasi ya timu hiyo na kupata bao la tatu katika dakika ya 56 kupitia kwa Coutinho.

Coutinho alifunga bao hilo kwa njia ya faulo nje ya 18 aliyoipiga na kujaa wavuni moja kwa moja baada ya Tambwe kuchezewa vibaya na beki wa Polisi.Polisi Mafunzo ilifanya shambulizi kubwa dakika ya 65 kupitia kwa Ikobela aliyepiga shuti kali lililopanguliwa na kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’.

Yanga iliitimisha idadi ya mabao ya manne kupitia kwa Msuva baada ya kumchambua kipa wa timu pinzani ndani ya 18 akiunganisha pasi ya Salum Telela katika dakika ya 80.
Yanga ilifanya mabadiliko kadhaa kwa kumtoa Sherman na kuingia Danny Mrwanda kisha Coutinho akatoka na kuingia Mrisho Ngassa, Telela alitoka akaingia Said Juma, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ naye alimpisha Rajab Zahir.

Mara baada ya ushindi, Msuva anayeongoza kwa ufungaji akiwa amefunga mabao manne katika michuano hiyo alisema: “Nitafanya jitihada za kutosha kuhakikisha ninachukua ufungaji bora wa michuano hii, ninaamini nitafanikiwa kutokana na ushirikiano wa wachezaji wenzangu.”
CHANZO: CHAMPIONI

No comments

Powered by Blogger.