PLUIJM: TAMBWE, SHERMAN WATAONGOZA MAANGAMIZI
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm.
Na Said AllyKOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm ametamka wazi kuwa ataendelea kutumia mfumo wa kutumia mastraika watatu katika michezo mbalimbali ya timu hiyo kama alivyofanya katika mchezo dhidi ya Azam FC kutokana na kuhitaji kikosi hicho kupata ushindi wa mabao mengi katika kila mchezo wake.
Yanga ilionekana kucheza kwa kufanya mashambululizi mengi katika mechi dhidi ya Azam, wikiendi iliyopita ambapo aliwatumia washambuliaji watatu katika kikosi cha kwanza ambao ni Amissi Tambwe, Kpah Sherman na Danny Mrwanda.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Pluijm ambaye ametua nchini kuchukua mikoba ya Marcio Maximo aliyetimuliwa hivi karibuni, alisema ataendelea kutumia mfumo huo wa kuwaanzisha kwa kuwa nia yake ni kupata mabao mengi bila kujali aina ya wapinzani.
“Niliamua kuanzisha washambuliaji watatu katika mchezo ule dhidi ya Azam kwa ajili ya kuifanya timu kupata ushindi na mabao mengi, japo tuliishia kwa sare ya mabao 2-2.
“Lakini mfumo huo naweza kuutumia tena katika michezo mbalimbali ili kuifanya timu kuwa na uhakika wa kuibuka na ushindi katika kila mchezo,” alisema Pluijm. Yanga inatarajiwa kukipiga na Taifa ya Jang’ombe katika mechi ya Kundi A, kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar leo.
Post a Comment