NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 6

ILIPOISHIA:
“Niambie mwanangu, kama kuna jambo lolote baya tuliokutendea au ndugu zako?”
“Hakuna.”
“Sasa nini tulizungumza na kuelewana? Nini tena kimekukumba?”
SASA ENDELEA...
“Nilikuwa nataka kuosha vyombo, nilikashangaa wazo la kujiua likiniijia, ndipo nilipoingia ndani nitafute fedha, nikanunue sumu ya panya ninywe. Bahati nzuri sikuiona, nikapata wazo lingine la kujiua kwa kamba, ndipo nilipotafuta na kuifunga.”
“Naelewa kichwani mwako pepo mchafu wa kifo bado anakusumbua, unatakiwa maombi. Sijajua kwenye dini yenu mnafanya nini lakini kwenye dini yetu unaombewa na pepo mchafu wa kifo anakutoka.”
“Niliwahi kusikia mtu mwenye matatizo anasomewa dua, yanaisha.”
“Lakini mwanangu pale kanisani kwetu nimewaona hata waislamu wakija kuombewa bila kuhama dini zao.”
“Basi nipeleke maana nina imani ninapoelekea ni kubaya zaidi, leo umeniwahi kesho nitafanya kitu kingine.”
Tulikubaliana jioni ya siku ile nipelekwe kanisani nikaombewe, jioni ilipofika nilifika kanisani kuombewa. Watu walikuwa wengi sana walipita mbele kwa ajili ya kuombewa matatizo yao. Mchungaji alizungumza maneno mengi kabla ya kuanza kumpitia mmoja mmoja na kumshika kwenye paji la uso huku akikemea mapepo. Kila aliyeshikwa alianguka kwa nyuma na kudakwa na wasaidizi wake mchungaji au yule ambaye pepo alikuwa mgumu kutoka alimkemea kwa sauti ya juu mpaka lilipotoka na kutulia chini baada ya muda alisimama akiwa mzima.
Katika watu waliotoka mbele, kama sikosei nilikuwa mtu wa kumi na aliponifikia alisema kwa sauti ya juu akiwa amenishika kwenye paji la uso:
“Kwa jina la Yesu, pepo mchafu ondoka ndani ya mwili wa binti huyu, mwache huru, mwache huru, toka, toka, tokaaaa.”
Baada ya kusema vile, nilijisikia kama nimepigwa shoti ya umeme na kuangukia kwa nyuma ambako kulikuwa na watu walionidaka. Nililazwa chini nikiwa sijifahamu. Baada ya muda nilinyanyuka na kuruhusiwa kwenda kukaa. Usiku mama Solomoni alinieleza:
“Sasa mwanangu umekuwa kiumbe kipya.”
“Nashukuru sana mama kwa msaada wako mkubwa.”
“Najua ulikuwa katika wakati gani, siku zote mwanadamu aliyevamiwa na shetani huwa na kiza kizito mbele yake hata ayafanyayo huwa mabaya kwa vile hajui akifanyacho kutokana na kiza kilicho mbele yake.”
“Ni kweli huwezi kuamini, sasa hivi moyo na mwili wangu umekuwa mwepesi, siwazi tena vitu vibaya zaidi ya kuyatamani maisha ambayo kwa kweli sasa ndiyo nayaona matamu.”
Baada ya mazungumzo tulikwenda kulala kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana. Asubuhi ya siku ya pili ilikuwa mpya kwangu kwani kila dakika niliyokuwa peke yangu, nilitubu makosa yangu kwa Mungu kwa kuamini nilichotaka kukifanya hakikuwa sahihi.
Tokea siku hiyo, nilijikuta nami nampokea Yesu taratibu, japo si kwa asilimia kubwa kutokana na dini yangu ya kuzaliwa ya uislamu, kanisani sikwenda, lakini sala za nyumbani nilishiriki ikiwemo kusali kwa kupiga magoti. Siku zilikatika, afya yangu iliimarika siku hadi siku.
Katika maisha yangu sitamsahau mama Solomoni kwa kunipa mapenzi ambayo yalinihamisha katika mawazo mabaya na kujiona nimezaliwa upya. Japo maisha yake yalikuwa ya kawaida, lakini upendo ulitawala ndani ya nyumba yake huku wanaye wakiniona kama ndugu yao wa kuzaliwa. Baada ya miezi saba kukatika nikiwa kwa mama Solomoni. Siku moja walikuja wageni ambao walikuwa ndugu wa mama Solomoni wanaokaa mjini.
Katika kuwaandalia chakula na vinywaji, ndugu yake alinishangaa kwa heshima niliyoionesha muda wote toka walipofika mpaka muda ule. Nilimsikia yule mama akiuliza kwa kilugha:
“Mama Solomoni, huyu mtoto mwenye heshima umemtoa wapi?”
“Ni habari ndefu.”
“Ya nini?”
“Salha,” mama Solomoni aliniita.
“Abee mama,” niliitikia kwa unyenyekevu.
“Hebu kamalizie vile vyombo naona ndugu zako wanafanya mchezo.”
“Hakuna tatizo.”
Nilijibu huku nikitoka nje, wakati natoka nilimsikia akisema kwa kilugha kwa kuamini siijui kwa vile hakuwahi kunisikia nazungumza toka nitoke mjini.
“Nimemtoa kijanja ili tuzungumze sipendi asikie kwani nitamtonesha kidonda ambacho naamini kimepona.”
Sikutaka kusimama kwa kuamini japo nataka kuzungumziwa mimi, lakini yalikuwa hayanihusu. Nilipofika nje, kweli niliwakuta akina Rose wanapiga stori wamesahau kuosha vyombo.
“Jamani mama kanituma niwasaidie kumaliza kuosha vyombo.”
Nami sikutaka kuosha kwa haraka, niliosha taratibu ili kuvuta muda wa mazungumzo ya ndani. Hata baada ya kumaliza kuosha, sikuingia ndani kusubiri niitwe. Baada ya nusu saa nikiwa nimekaa chini ya mti, niliitwa ndani.
“Da Salha unaitwa ndani na mama.”
Bila kujibu nilinyanyuka na kuingia ndani na kumkuta mama amekaa karibu na mama mkubwa. Waliponiona naingia, wote waligeuza sura na kuniangalia
Salha ameitiwa nini?
Kwa vile nilikwishajua wanazungumzia nini, nilikwenda mpaka kwa mama na kuitika kwa unyenyekevu.
“Abee mama.”
“Mama yako mkubwa anakuita.”
“Abee mama mkubwa,” nilimgeukia mama mkubwa.
“Salha,” mama mkubwa aliniita.
“Abee mama.”
“Kwanza pole sana mwanangu kwa yote yaliyokukuta.”
“Asante mama.”
“Nimesikia yaliyokusibu lakini mtangulize Mungu kwa kila jambo.”
“Sawa.”
“Sasa ni hivi, kwanza nimevutiwa na tabia yako ambayo ilinitia wasiwasi na kuamini huenda ni kwa ajili ya kuwaona wageni, lakini nimeambiwa hii ni tabia yako ya asili. Sasa mwanangu nitaondoka na wewe kwenda mjini ambako utanisaidia kazi zangu ndogondogo huku nikikulipa fedha kidogo ambazo zitakusaidia kufanya mambo yako mengine bila kunitegemea.”
“Mama amekubali?”
Japo habari za kuhamia mjini zilikuwa nzuri, lakini sikutakiwa kuonesha nimefurahia sana, nilitakiwa kuonesha bado namhitaji mama Solomoni.
“Kwa vile dada yupo peke yake nina imani utakuwa mtu wa kumtoa upweke, dada yako mkubwa muda mwingi anakuwa chuoni, kurudi kwake ni usiku hivyo muda wa mchana anahitaji msaada wa kazi ndogo ndogo.”
“Sawa mama, kama wewe umeridhia mimi sina kipingamizi.”
“Mama Solomoni na wanao wangekuwa kama huyu ungeringa.”
“Mungu hamnyimi mja wake, kamnyima walezi kampa tabia nzuri ambayo itamfanya aishi sehemu yoyote.”
Kwa vile walikuwa ndiyo wanajiandaa kurudi mjini nami nilielezwa nikaoge na kujiandaa kuhamia mjini. Nilikwenda kuoga na kujiandaa kusubiri kwenda mjini. Ilionesha maisha yao ni mazuri kwani walikuwa na gari la kutembelea lililowaleta kijijini.
Baada ya maandalizi kukamilika niliagana na mama Solomoni ambaye kwangu ndiye aliyekuwa mzazi wangu na wanawake walikuwa ni ndugu zangu. Kwa kweli hata wao walihuzunika kutengana nami, kwani tulikuwa tumeshazoeana. Niingia kwenye gari na kuelekea mjini.
Tulifika mjini majira ya saa moja jioni na kukaribishwa kwenye nyumba nzuri iliyokuwa na kila kitu ndani. Pamoja na ukubwa wa nyumba lakini familia ilikuwa ndogo, ilikuwa na watu wanne tu na mimi nilipoongezeka tukawa watano. Kabla ya mimi kufika, muda wote wa mchana mama Mather alikuwa peke yake mpaka jioni ambapo aliungana na familia yake. Nilijiuliza aliwezaje kuishi peke yake katika nyumba ile , maelezo niliyoyapata baadaye ni kwamba siku za nyuma alimchukua Rose mtoto wa mama Solomoni lakini alishindwana naye kutokana na muda mwingi kuwa kwenye ‘tivii’ huku kazi za usafi hazifanyiki.
Kwangu yote hayo sikuona kikwazo, kwani kufanya usafi yalikuwa maisha yangu tangu nilipobadilishwa kutoka mtoto wa familia na kuwa mfanyakazi, hata niliporudi kwa marehemu bibi bado niliendelea na kazi tena mara mbili zaidi, niliamini si tatizo.
Maisha ya makazi mapya yalikuwa mazuri sana ambayo yalinifanya nisahau mateso yangu ya siku za nyuma. Kwani sehemu niliyokuwa sikuwa msichana wa kazi bali ni sehemu ya familia.
Mchana nilifanya kazi na mama Mather na jioni Mather na Marry waliporudi nilipumzika na wao walifanya kazi za jioni.
Kwa muda mfupi nilinawiri na kupendeza machoni mwa watu, siku za mapumziko tulifanya kazi kwa kushirikiana ambapo kulikuwa na tofauti kubwa na kwa mama Solomoni kule kazi nyingi nilifanya mimi japo hazikuwa kubwa.
Makazi mapya walikuwa wacha Mungu, wote walikuwa wameokoka, pamoja na kuokoka lakini hawakunilazimisha kujiunga na dini yao, waliniacha na dini yangu hata vyakula ambavyo wao walikula lakini dini yangu ilivikataza waliviacha kwa ajili yangu ili isionekane wamenibagua.
Kila siku mama Mather alikaa chini na kunieleza habari za kumcha Mungu kitu ambacho kilibadili akili yangu na kuamini dini ni njia ya kumjua Mungu na Mungu ni mmoja. Mwenyewe kwa hiyari yangu baada ya kujifikiria kwa muda mrefu kutokana na malezi mazuri niliyopata kutokwa kwa familia ya mama Mather niliamua kubadili dini na kuwa Mkristo ambaye nilimpokea Bwana Yesu kama mkombozi na mwokozi wa maisha yangu na kupewa jina la Ester.
Nami nilihudhuria ibada kama kawaida, kutokana na tabia zangu za asili na nilivyompokea Bwana Yesu nilizidi kuwa kipenzi cha familia.
Baada ya mwaka kukatika mama Mather aliniuliza kama nitakuwa tayari kujiendeleza kielimu. Nilikubali mara moja kwani jambo hilo lilikuwa akilini mwangu.
Lazima niseme ukweli, naweza kusema niliweza kukufuru kwa kulaani tabia za mama za kukosa uaminifu pia kuzaliwa katika familia isiyo na mapenzi.
Niliamini kabisa sehemu niliyotakiwa kuzaliwa ni ndani ya nyumba ya mama Mather. Siku nazo zilikatika nami nilijengeka kimwili na kuonekana mama wa familia hata kama ningeachiwa nyumba ningeweza kuiendesha bila matatizo.
Katika nyumba ile baba mwenye nyumba, mzee Sifael alionesha mapenzi ya dhati kwangu hata kunipa zawadi za siri ambazo wenzangu na mama hawakuziona.
Nami nilizidisha utii na heshima kwa familia mpaka kuwa mfano wa kuigwa ndani na nje ya familia. Pia kanisani nilipata marafiki wengi wa kike na kiume, pia walitokea wachumba waliokuwa wapo tayari kunioa. Kila aliyeonesha kunihitaji kimapenzi nilimweleza aje awaone wazazi wangu.
Waswahili wanasema njiwa ukiona unapewa mtama mwingi ujue upo mtegoni, siku moja usiku, nikiwa nimelala chumbani kwangu, nilishtushwa na kitu kizito kikiwa kimenilalia juu yangu, nilitaka kupiga kelele lakini nilizibwa mdomo, kelele zilitoka kidogo ambazo hazikufika mbali.
Nilijitahidi kutembeza mikono kutafuta swichi ya kitandani, baada ya kuibahatisha niliwasha. Sikuamini kumuona baba, mzee Sifael akiwa juu yangu mtupu kama alivyozaliwa. Nilijitahidi kujitoa huku nikimpiga mateke na kumfinya lakini alining’ang’ania, ilionekana anamalizia shughuli yake.
“Samahani Ester nilizidiwa mwanangu lakini usimwambie mtu, ukimwambia mama yako utavunja ndoa yangu ya miaka 30 sasa.”
Alisema huku akiteremka kitandani na kunipigia magoti kwa kitendo chake cha kunibaka.
“Ester nipo tayari hata kukununulia nyumba na gari lakini ufiche siri hii, naomba nipo chini ya miguu yako usimwambie mama Martha atajiua, ana moyo mdogo sana yule.”
Sikumjibu lolote, nilikaa pembeni ya kitanda na kulia kilio cha kwikwi, na kujiona mimi ni kiumbe gani? Mtu aliyenichukua kwa ajili ya kunilea ndiye anayenibaka. Niliendelea kulia huku mzee Sifael akiendelea kuniomba msamaha mpaka machozi yakamtoka.
Nilijikuta nikiingiwa na huruma na kuamini walichonifanyia ni kikubwa kuliko alichonitendea. Lakini nilijiuliza nitamtazamaje mzee Sifael, mtu niliyemheshimu kuliko kitu chochote. Nilijikuta nikiyakusanya matukio yote tangu kukataliwa na baba, kutaka kuuawa na Samwel mpenzi wangu baada ya kunipa ujauzito na hili la kubakwa na mlezi wangu. Nilianza kuwaona wanaume ni wakatili na kuwachukia wote.
“Ester mama umenisamehe? Najua nimekutendea kitendo cha kinyama kukuingilia bila ridhaa yako. Ni shetani tu mama, naomba unisamehe sirudii tena,” mzee Sifael aliendelea kuniomba msamaha.
“Naomba uondoke,” nilimwambia kwa ukali.
“Lakini nakuomba mama usimwambie mke wangu.”
“Nimekwambia nakuomba uondoke,” nilirudia kwa sauti ya juu kidogo ili kumtisha aondoke.
“Ester chondechonde, usimwambie mama Martha.”
“Hebu niondokee acha kunitolea radhi, vaa nguo zako uondoke,” kwani muda wote alikuwa akiniomba radhi akiwa mtupu kama mwanga. Mzee Sifael alipitia taulo na kuonesha alijiandaa, wala hakuwa na nguo ya ndani, kabla ya kutoka alirudi na kunipigia magoti kuniomba nisimwambie mama.
“Mwanangu chonde ibakie siri yetu.”
“Sawa sitamwambia mama,” nilijibu bila kumtazama.
Mzee Sifael aliondoka na kuniacha nikiwa bado nimekaa pembeni mwa kitanda nisiamini kilichotokea, yaani mzee Sifael, mtu aliyeonekana mcha Mungu kunibaka. Nilipojishika sehemu za siri nilikuta mbegu zake za kiume kuonesha hata hakutumia kinga, nilijikuta nikilia mpaka presha ikanipanda
Macho yalivimba na kuwa mekundu, kichwa nacho kiliniuma kama kuna mtu anakichokonoa. Nilijiuliza kubakwa kule ni dalili za nini, kuambukizwa Ukimwi au nini? Nilimuomba mbali aepushie mbali. Alfajiri iliingia naiona na wakati huo nilikuja kuamshwa kwa ajili ya ibada ya alfajiri kabla ya kina Martha na baba hawajaenda kazini na shuleni.
Dada Martha alikuja chumbani kwangu kuniamsha, alishtuka kusikia sauti ya kilio cha kwikwi, ilibidi aingie chumbani kwangu. Aliponiona alishtuka sana, hali aliyonikuta nayo kwani hakunikuta na kitu mwilini, macho yalikuwa yamekaribia kufumba kutokana na kuvimba baada ya kulia kipindi kirefu bila kunyamaza.
Muda wote nilijiuliza alichonifanyia mzee Sifael pamoja na shetani kumpitia angekuwa mwanaye wa kumzaa angemfanyia vile?
“He! Ester vipi mbona hivyo, umekumbwa na nini tena mdogo wangu?”
Sikumjibu swali lake kwani lilikuwa kama kutonesha kidonda, nilijinyanyua na kwenda kujitupa kwenye kifua chake huku nikiendelea kulia.
“Mdogo wangu kulikoni, mbona unanitisha, nini kimekusibu tena?”
“Dada sina thamani ya kuendelea kuishi, nina imani nimekuja duniani kimakosa.”
“Kwa nini mdogo wangu, mbona yalikwisha, kipi tena kimekurudia?”
“Dada wee acha kwa nini kila siku niwe mimi tu, nikipata raha mara moja basi taabu miaka mia moja.”
“Una maana gani?” Martha aliona ngoma nzito kwani alishindwa kunielewa kabisa, ilibidi amwite mama kwa sauti kubwa.
“Mamaaa hebu njoo mara moja kwa Ester.”
Wakati akimwita nilijiuliza nitawaeleza kitu gani ambacho watanielewa, kusema nimebakwa na baba mbele ya mama na dada Martha niliona aibu, pia niliamini kauli yangu ingekuwa sawa na upanga mkali ambao ungetenganisha nyumba ya mzee Sifael iliyodumu kwa zaidi ya miaka 30.
Nini kitaendelea? Tukutane SIKU YA KESHO
Post a Comment