ad

ad

Niliishi dunia ya peke yangu - 3


ILIPOISHIA Jumamosi:
Siku zilikatika huku nami nikiingia katika dunia ya wakubwa, bila kutarajia nilijikuta nimepachikwa ujauzito bila kutegemea. Kutokana na malezi mazuri ya mwanaume wangu niliamini atailea ile mimba. 
SASA ENDELEA...


BAADA ya kupata uhakika kuwa nimenasa,  siku moja nikiwa nyumbani kwake ambako kila siku nilipokuwa nikitoka kazini usiku ilikuwa ni lazima  niende na  usiku wa manane anirudishe nyumbani kwa kuwa hali ya bibi haikuniruhusu kukaa naye mbali muda mrefu.
Tukiwa chumbani na mpenzi wangu ambaye naye alikuwa ndiyo kwanza anaanza maisha, akiwa na kitanda cha mbao cha futi nne kwa sita na godoro chakavu la sponji na sturi moja. 

Kwa kweli ndiyo alikuwa akianza maisha, baada ya mchezo wetu nilimweleza nilivyo:
“Samweli mwenzio ni mjamzito.”
“Ati?” alishtuka.
“Ina maana umenisikia au...?” nami nilimuuliza baada ya kuonesha ameshtuka.

“Lazima nishtuke kama hutanii.”
“Ninachokisema ni kweli mimi ni mjamzito.”
“Mmh!” Samwel aliguna.
“Mbona sikuelewi?” ilibidi niwe mkali kidogo.

“Si kwamba sikuelewi, bado sijajua nitafanya nini.”
“Kufanya nini kivipi?” nilimuuliza nikiwa nimemkazia macho.
“Si unaona maisha yangu ndiyo nayaanza na mtoto akija unafikiri itakuwaje?”

“Nina imani ulijua utafanya nini, haya nilikueleza toka awali kuwa kufanya mapenzi bila kinga kuna madhara ulichojua kwenda kupima vvu tu ukasahau mimba leo unashangaa nini?”
“Ni haraka sana kuwa na mtoto.”
”Sasa tutafanya nini wakati mtoto yuko njiani?”

“Lazima tuitoe.”
”Ha! Tuitoe?” Nilishtuka.
“Hatuna jinsi, acha hii tuitoe ili tujipange kwa mimba itakayokuja tutakuwa tumepiga hatua.”
“Lakini nasikia kutoa mimba mtu anaweza kupoteza maisha.”
“Kuna wataalamu wa kutoa mjini, tutakwenda kuitoa na tutarudi bila mtu kujua kama umetoa mimba.”

“Samwel katika vitu nilivyokatazwa na bibi ni kutoa mimba,kwani mama yangu mdogo aliyekuwa akimfuata marehemu mama yangu mzazi alikufa kwa kufanya kitu kama hicho.”
“Hiyo ilikuwa zamani, siku hizi hakuna vifo vya kutoa mimba, kuna vifaa vya kisasa. Unamuona shoga yako Silivia, unajua kama amekwishatoa mimba mbili?”

“Ha! Utani mimba mbili?” nilishtuka kusikia vile.
“Eeh! Ukimuangalia utajua?  mimba hiyo ya pili ametoa hata wiki mbili hazijapita.”
“Mmh! Ngoja nitamuuliza.”
“Hawezi kukueleza ukweli ile ni siri kati yake na mpenzi wake na mimi nimejua kutokana na ukaribu wangu na Sosi.”

Nilikubaliana na mpenzi wangu kwamba Ijumaa ya siku ile twende mjini alfajiri ili nikatoe mimba  na kunifanya niwahi kurudi kumhudumia bibi. Usiku wa kuamkia siku ya kwenda kutoa ujauzito nilipatwa na ndoto nyingi za kutisha ikiwemo ya kujiona nimo ndani ya jeneza, kwa kweli ndoto zile ziliniogopesha sana na kujiuliza zilikuwa na maana gani. Wasiwasi wangu mkubwa huenda ulitokana na kutaka kuitoa mimba kuwa ndiyo ingekuwa sababu ya mauti yangu.

Nilipanga asubuhi nimkatalie Samwel kwa kuamini kwamba ndoto zile zilikuwa na ujumbe wa kweli kwa kitendo nilichotaka kukifanya. Kwa hofu ya ndoto kujirudia kila wakati niliamua kumaliza usiku kwa kukaa kitandani mpaka alfajiri na kuwa wa kwanza kuamka kwa ajili ya kufanya usafi.

Nikiwa bado naendelea na usafi Samwel alifika kuonesha amejiandaa.
“Vipi bado tu,” aliniuliza.
“Sam mbona mapema sana?”

“Salha tuwahi mapema ili uwahi kurudi si unajua usafiri shida.”
“Najua, lakini siwezi kuondoka bila kumuandalia uji bibi.”
“Basi fanya haraka.”

Kwa vile chungu kilikuwa jikoni nilifanya kazi nyingi kwa wakati mmoja baada ya muda nilimaliza usafi na wakati huo uji ulikuwa umeiva.
Nilimpatia bibi aliyekuwa amekwisha amka, nami nilijiandaa kwa kuoga kisha nilimuaga bibi kwa kumdanganya kuwa nilikuwa nakwenda kufuata cheti changu cha shule ambacho kingenisaidia kwa kazi yoyote pale kijijini. 

Bibi alinieleza niwahi kurudi kwani hali yake niliijua, kwa vile usiku tulipika viazi nilijua atakula mchana kama nitachelewa.
 Baada ya makubaliano yangu na bibi nilimpitia Samwel aliyekuwa akinisubiri njiani na kuelekea kituo cha basi, tulikuta gari limejaa ilibidi nasi tuingie kutokana na basi la alfajiri kuwa moja, mengine  yangefika saa mbili au tano na la mwisho ni saa kumi ambalo huwa halirudi mpaka kesho yake.

Tulifika mjini saa mbili na nusu asubuhi, kabla ya kwenda tulipita sehemu kupata kifungua kinywa kisha tulipanda daladala kuelekea huko kwenye hiyo hosptali. Tuliteremka sehemu kisha Samwel alisema nimfuate, tulipita kwenye kichochoro na kutokea kwenye nyumba yenye geti.

Alinieleza pale ndipo hospitali iliyoonekana kama nyumba ya mtu, tuliingia ndani ya nyumba hiyo kupitia mlango wa uani, moyoni sikupendezwa na uamuzi aliochukua mpenzi wangu wa kuitoa ile mimba.
Ndani tulipokelewa na dada mmoja ambaye alituuliza shida yetu, nilimueleza akaniomba fedha ya kutolea mimba. Samwel alimpa baada ya kumpa nilipelekwa kwenye chumba cha ndani ambacho kilikuwa na vifaa vya matibabu.

Baada ya kupokelewa Samwel alitoka na kuniacha ndani ya chumba na kaka mmoja wa umri wa kati ya miaka 28 mpaka 30. Alinielekeza nivue nguo na kupanda kitandani, nilifanya kama alivyonieleza. Alichukua vifaa na kuanza kunitoa mimba.

Ilikuwa tofauti na nilivyoelezwa kuwa kutoa ujauzito ni muda mfupi, tena rahisi.

Nilishangaa kuona muda ukikatika huku nikimuona yule kaka akitokwa na jasho na uso wake ukionesha wasiwasi.

Kwa vile nilikuwa mgeni kwenye mambo yake sikujua nini kinaendelea.

 Nilisikia maumivu makali kupita kiasi, nikauma meno.

Damu ilinitoka kwa wingi na kumuona akihangaika kuniweka pamba kuzuia wingi wa damu, kila dakika ilivyozidi kwenda ndivyo nilivyoanza kuhisi kizunguzungu.

Yule kaka alihangaika sana mpaka mwisho jasho likawa linamtoka chapachapa.

Taratibu nilianza kupoteza uwezo wa kuona, nikawa kama nimo ndani ya maji.

 Baada ya muda nilipoteza fahamu, sikujua  kilichoendelea mpaka niliposhtuka na kujikuta nimo kwenye mtaro wa maji huku mvua ikininyeshea.

Kwa kuwa kulikuwa na giza sana, sikujua pale ni wapi.

Nilijitahidi kunyanyuka na kutoka kwenye mtaro, muda huo bado mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha.

Nilipojaribu kutembea baada ya kutoka mtaroni nilihisi maumivu makali chini ya kitovu, hivyo kunifanya nitembee taratibu kwa kuinama.

Niliziona taa za umeme kwa mbali sana. Nilijiuliza pale nipo wapi na nilifikaje lakini sikupata jibu.

 Pia nilijiuliza mpenzi wangu Samweli yupo wapi na mbona nimejikuta sehemu  ile peke yangu? Kwa kweli nilikosa jibu.

Nilitembea taratibu kufuata sehemu zinapoonekana taa.
 Nilijikuta nimetokea kwenye barabara ya lami, mvua nayo haikuwa na huruma, iliendelea kuninyeshea.

 Magari makubwa yalipita, nikajitahidi kupunga mkono lakini hakuna lililosimama, nikahisi labda nilikuwa nimesimama pembeni, tena gizani.

Maumivu ya tumbo yalikuwa makali kiasi cha kusababisha nishindwe kuendelea kusimama.

Nilijiuliza lile ni balaa gani ambalo liliongeza maumivu moyoni mwangu, nikaamini kabisa yaliyonitokea ni laana ya mama na bibi ya kukatazwa kutoa mimba.

Nilijua kama ni kweli ni laana ya kutoa mimba basi ningekufa, lakini si kwa mateso kama yale.

Kutokana na maumivu makali ya tumbo huku baridi kali ya mvua ikinichanyata, taratibu niliteremka chini na kukaa huku nikitamani mtoa roho atokee pale ili anipunguzie mateso.

 Lakini haikuwa vile kizunguzungu nacho kilijirudia, nikajitahidi kushindana nacho lakini nilishindwa, nikaamua kulala kwenye maji huku mvua nayo ikiendelea kuninyeshea.
                                                                            *****

Nilizinduka na kujikuta nimelala kwenye kitanda cha hospitali.

Nikiwa natafakari pale ni wapi, muuguzi aliingia na kuja moja kwa moja kwenye kitanda nilichokuwa nimelala.

“Vipi mdogo wangu?”
“Sijajua dada yangu.”
“Pole sana.” 
“Asante.”
“Vipi unaendeleaje?”
“Sijambo kidogo.”
“Eti ilikuwaje?” 
“Kwa kweli sijua kitu dada yangu, naona kama njozi ya giza na nilipoamka asubuhi nikajishangaa kujikuta hapa.”
“Unakaa wapi?”
“Kijijini.”
“Ilikuwaje ukaokotwa sehemu mbaya kama ile.”
“Kwa kweli dada sijui, naona kama miujiza.”

“Hebu nilieleze ilikuwaje, maana inaonekana ulikuwa unatoa mimba, kwa nini mdogo wangu?”
Kwa kweli sikuwa na jinsi niliamua kumueleza ukweli kwani sikuwa na la kuficha, ilionesha yule dada ambaye alikuwa mtu mzima anajua mengi kwani suala la kutoa mimba alilijua kirahisi.

Nilimueleza kwa ufupi jinsi nilivyoshawishiwa na mpenzi wangu kutoa mimba na kumweleza mara ya mwisho nilikuwa kwenye kitanda cha hospitali nikitoa mimba na hali iliyonitokea na nilivyojikuta kwenye mtaro wa maji sehemu ambayo nilikuwa siijui.
“Mpenzi wako yupo wapi?”
“Hata sijui.”
“Umesema unakaa na bibi yako, mama na baba yako wapo wapi?”
“Mama alifariki miaka minne iliyopita.”
“Baba yako?”
“Sina baba.”
“Alifariki?”
“Simjui.”
“Ooh! Pole sana.”
“Sijapoa kwa vile sijajua hatima ya maisha yangu.”
“Unafikiri kwa nini ulitupwa?”
“Hata najua! Kwani nani alinileta hapa?”
“Polisi wa doria.”
“Mungu wangu! Walinikuta wapi?”
“Kwa maelezo yao wakati wanapita waliona mwili wako umelala pembeni ya barabara huku ukiendelea kunyeshewa na mvua.

Wao walijua umefariki, walikuchukua mpaka hapa na kutaka upelekwe mochwali lakini mganga mkuu alisema huwezi kupelekwa chumba cha maiti bila kufanyiwa uchunguzi, ndipo ilipogundulika kuwa hujafa bali umepoteza fahamu.”

“Mungu wangu!” nilishika mdomo baada ya kusikia habari mbaya kama zile za kutaka kupelekwa chumba cha maiti.

Itaendeleasiku ya kesho.

No comments

Powered by Blogger.