NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU -2
ILIPOISHIA:
Kwenda kukaa kwa bibi nilikataa kwani maisha yake aliyajua mwenyewe.
Mwanzo niliamini huenda ni hasira za baba lakini siku zilivyokuwa zikikatika ilionesha kuwa ni kweli baba alikuwa ameamua.

Sikuruhusiwa kwenda shule zaidi ya kuwepo nyumbani bila shughuli ya kufanya.
SASA ENDELEA...
Tokea hapo niligeuka kuwa mfanyakazi wa ndani na si mtoto wa nyumba ile tena, kwa vile niling’ang’ania mwenyewe kukaa, wafanyakazi wote walifukuzwa na kubaki peke yangu kama mfanyakazi wa ndani, kazi ya watu watatu nilizifanya peke yangu.
Kwa kweli roho iliniuma sana, baada ya kukatishwa kwa ndoto zangu, nilipokosa uvumilivu muda mwingi nilikuwa nikilia na kumkumbuka mama, kitu kilichonituma kunywa sumu ili nife kwani sikuuona mwelekeo wa maisha.
Siku zote nilimlilia mama yangu mzazi kwani pamoja na makosa yake, bado alionesha mapenzi ya dhati kwangu na kama Mungu asingemchukua, basi nami ningetimiza malengo yangu kama bibi alivyonieleza kwamba mama yangu alikuwa akinijali.
Kila nilipomkumbuka mama nililia sana, baada ya uvumilivu kunishinda siku moja niliamua kunywa sumu ya panya ili nimfuate mama yangu.
Baada ya kuikoroga niliinywa na kwenda kujilaza chumbani kwangu. Maumivu makali ya tumbo yalinifanya nipoteze fahamu, niliposhtuka nilijikuta hospitali huku wadogo zangu wakiwa pembeni ya kitanda wakilia.
Nilipata huduma nzuri na kuruhusiwa kutoka hospitali baada ya siku tatu, niliporudi nyumbani sikuruhusiwa kuingia ndani.
Nilikuta vitu vyangu vyote vikiwa nje na kuelezwa kuanzia siku niliyotaka kuwaingiza kwenye matatizo sikutakiwa tena pale.
Nilipewa nauli ya kwenda kuishi kwa bibi kijijini.
Pamoja na kumuomba msamaha baba lakini ilikuwa ni kazi bure, kwani alikataa katakata.
“Pamoja na upumbavu alionifanyia marehemu mama yako wa kuniletea mtoto wa haramu, bado umeona haitoshi unadiriki kunywa sumu ijulikane nimekuua ili nikafie jela wanangu wateseke?.
“Naomba kuanzia leo nyumba hii uione kituo cha polisi na muuza bangi.”
“Nisamehe ba...ba...nimechanganyikiwa mzazi wangu,” nilipiga magoti kuomba radhi.
“Nani baba yako? Sitakusamehe milele tena umetonesha donda la miaka kumi na saba aliloniumiza mama yako.
Naomba uondoke mimi siyo baba yako nenda ukamfuate baba yako siyo mimi,” baba alisema maneno yaliyonikata maini.
“Lakini si ulimueleza mama utanilea?” nilimuuliza kutokana na kauli yake muda mfupi kabla mama hajafariki.
“Siwezi kufuga adui yangu, leo umekunywa sumu kesho utatuua nyumba nzima. Naomba uondoke mbele yangu,” baba bado alikuwa na roho ya kikatili.
Pamoja na wadogo zangu kuniombea msamaha, baba hakuwa tayari kunisamehe zaidi ya kunifukuza kama mbwa.
Mmh! Mtoto wa kike jaribio langu la kwanza la kujiua lilishindikana na kufukuzwa. Lakini sikukata tamaa kwani niliamini bado nina nafasi ya kutimiza lengo langu la kujiua popote si lazima pale.
Nilikwenda kijijini kwa bibi na kupokelewa, nilimueleza nimefukuzwa lakini sikumueleza kama kisa ni baada ya jaribio langu la kutaka kujiua kushindikana.
Bibi pamoja na maisha yake kuwa ya kubahatisha alinipokea kwa mikono miwili.
Kumbe taarifa za kutaka kujiua kwangu zilishamfikia, siku moja baada ya chakula cha usiku aliniuliza:
“Salha mjukuu wangu kwa nini ulitaka kujiua?”
“Ha! Nani?” Nilishtuka kwani niliamini ilikuwa siri.
“Hapa nazungumza na nani?”
“Nani kakwambia?” niliuliza swali badala ya kujibu.
“Si muhimu kujua nani kaniambia, nataka uniambie kwa nini ulitaka kujiua?” bibi alikuwa mkali na majibu yangu ya kupindisha.
“Bibi kwa kweli sina faida ya kuendelea kuishi, hebu angalia uingiaji wa mimba yangu, pia msukukosuko tangu nikiwa tumboni.
“Ni wazi hata kuja kwangu duniani nimekuja kimakosa,” nilijibu huku nikilia kwa uchungu, swali lake lilikuwa ni sawa na kutonesha kidonda kilichoanza kupona.
“Mjukuu wangu wewe si wa kwanza kutokewa na matatizo kama haya, hebu mtangulize Mungu mbele, yeye ndiye anayejua nini makusudia yake kwa kila kiumbe aliyemleta duniani.
“Pia kujiua ni kosa kubwa kwani ni kufuru, ni sawa na kuingilia kazi yake kwa vile hakuna binadamu atakayeishi milele, kila mwanadamu ana siku zake za kuishi duniani na mwisho atakufa.
“Vitabu vya dini vinasema unapojiua ukizikwa tu unaanza kupewa mateso mpaka siku ya kiama, hebu achana na mawazo ya kijinga.
Wewe umekataliwa na baba yako si walimwengu, hebu angalia hapa kijijini kwetu kuna watoto wangapi wazazi wao walikuwepo lakini kwa bahati mbaya walikufa kwa ukimwi au magonjwa mengine na wapo wanaishi, kwani wamepungukiwa nini?”
“Lakini hawakutengwa na wazazi wao?”
“Nimekueleza mama yako alikupenda kuliko ndugu zako wote, hasa lilipotokea tatizo kama hilo.”
“Na baba yangu yupo wapi?”
“Mmh! Kuna habari zisizo rasmi kuwa baada ya kufukuzwa kazi aliokotwa akiwa amekufa na tuhuma zilikwenda kwa baba yako kuwa ndiye aliyefanya kitendo hicho cha kikatili baada ya kujua aliihujumu ndoa yake.”
“Kama kamuua baba yangu wa kweli sasa alitaka niende kwa baba yupi?” niliuliza kwa uchungu na kujikuta nikianza kujenga chuki ya kweli kwa baba.
“Hizo zilikuwa habari za juu juu japo hazikuwa na uhakika mkubwa. Naamini marehemu mama yako alikuwa akijua mambo mengi, kama angekuwepo angekueleza kila kitu.”
“Sasa nitajuaje baba yangu yupo hai au amekufa, kama yupo hai nitampenda na kumheshimu hata kama hana kitu kwa vile ndiye mzazi wangu, hakuna mwingine.”
“Hilo ndilo lililobakia, achana na mawazo mabaya ya kujiua.”
“Sasa nitamuona wapi?”
“Kwa vile unamhitaji baba yako tutafanya utaratibu wa kumtafuta.”
“Kwani mara mwisho kumuona ilikuwa lini?”
“Toka alipofukuzwa kazi baada ya kufumaniwa na mama yako sijamuona tena.”
“Kuhusu habari zake?”
“Kwa kweli baada ya kifo cha mama yako ndipo niliposikia taarifa za kifo chake, sasa sijui habari zile zina ukweli gani juu ya kifo chake.”
“Sasa bibi mbona sikuelewi baba yangu yupo hai au amekufa?”
“Mmh! Hapo kidogo pananichanganya.”
“Au nikamuulize baba?”
“Amekukataza usifike kwake hebu achana naye kama yupo siku moja Mungu atamleta na utamuona.”
Niliyaanza maisha mapya ya kijijini ya kwenda shamba na kuchota maji kisimani pia kupikia kuni, maisha ambayo mwanzo niliyafanya kwa hamu ya kumsaidia bibi. Lakini yalibadilika na kuwa maisha yangu ya kudumu, nilizoea kulala kwenye nyumba ya umeme, maji ya bomba, kupikia mkaa na jiko la gesi, tena kazi hiyo niliianza baada ya kugeuzwa mfanyakazi wa ndani na si mtoto wa pale.
Lakini kwa bibi tulitumia kibatari na siku nyingine tulilala giza kutokana na kukosa fedha ya kununua mafuta ya taa. Tulilala sehemu nzuri kwani marehemu mama alijitahidi kumkumbuka mama yake.
Maneno ya bibi yalinipa moyo na kuamini ule ulikuwa muda wangu wa kumsaidia bibi ambaye umri ulikuwa umemchukua sana. Hali ya bibi ilifuta wazo langu la kutaka kujiua kwa mara ya pili. Nilimlea bibi kwa kufanya kazi zote ngumu huku tukisaidiana kazi za shamba.
Nilijikuta nikikomaa kiakili japo umri wangu ulikuwa mdogo, uliotakiwa niwe chini ya uangalizi wa wazazi wangu. Maisha yalikuwa magumu sana kwani tulitegemea shamba na kuuza kuni ambazo tulikuwa tukizifuata porini na kuziuza.
Wakati wa mvua hali ilikuwa mbaya kwani tulikosa biashara na kujikuta tukiishi maisha ya kubahatisha, siku nyingine tukilala bila kula. Kwa kweli mateso yale yalinirudisha katika dhamira yangu mbaya ya kutaka kujiua. Lakini hali ya bibi ilinizuia kwa kuamini kufanya vile nitakuwa nimefanya ukatili wa hali ya juu.
Nilijiuliza mimi mwenye nguvu nipo lakini tunalala njaa, kama bibi akibakia peke yake, tena katika kipindi ambacho afya yake ilikuwa mgogoro itakuwaje? Nilikubali kuendelea kupambana na matatizo kwani hali ile ilikuwa fasheni pale kijijini. Wasichana kama mimi walipunguza ukali wa maisha kwa kutembea na wanaume wenye unafuu wa maisha.
Lakini siku zote nilikumbuka wosia wa marehemu mama ambaye pamoja na sifa mbaya ya kukosa uaminifu katika ndoa yake pamoja na bibi waliniusia nisijiingize kwenye ngono katika umri mdogo kwani kama nitaukwaa naweza kupoteza malengo yangu.
Kauli zile zilikuwa zikijirudia kichwani kila nilipotongozwa na kunifanya niwe mgumu tofauti na wasichana wa rika langu ambao kila mmoja alikuwa na bwana zaidi ya mmoja. Kingine kilichonitisha, msichana mmoja alibebeshwa mimba na bwana kumkimbia, matokeo yake aligeuka kuwa ombaomba.
Siku zilivyozidi kukatika hali ya bibi nayo ilizidi kuzorota, akawa wa kusaidiwa kila kitu. Kutokana na ugumu wa maisha huku nikihitaji matumizi muhimu mimi na bibi, nilijikuta nikiangukia kwa kijana mmoja muuza chipsi ambaye kwa kweli alinisaidia mambo mengi sana ikiwemo fedha ya kumnunulia bibi dawa.
Siku zilikatika huku nami nikiingia katika dunia ya wakubwa, bila kutarajia nikajikuta nimepachikwa ujauzito. Kutokana na malezi mazuri ya mwanaume wangu niliamini atailea hiyo mimba.
INAENDELEA HAPA
Post a Comment